Papa kwa Mkuu ya Kiyahudi Skorka:imani na haki za binadamu hazipingani!
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 10 Mei 2023 amependa kumpongeza kwa barua Mkuu wa Kiyahudi Abraham Skorka, kutoka Argentina, ambaye katika Kitivo cha Taalimungu cha Chuo Kikuu cha Trnava kinachoongozwa na Wajesuit, nchini Slovakia, kimemtunukia shahada ya heshima ya udaktari kwa mchango wake katika kuendeleza mazungumzo kati ya Wayahudi na Wakristo na watu wa dini mbalimbali na kwa ajili ya kukuza uvumilivu katika nyanja za sayansi na elimu. Katika ujumbe uliosomwa wakati wa afla hiyo Baba Mtakatifu Francisko anatoa shukrani kwa rafiki yake wa zamani kwa kujitolea kwake na kwa ushawishi mzuri, katika miaka 42 ya shughuli za ufundishaji na kitaaluma, vizazi viwili vya wakuu wa wayahudi pamoja na wataalimungu Kikatoliki na Kiprotestanti, wakiheshimu kikamilifu vipengele vya kitaaluma vya taalimungu. “Kwa hiyo suala la kutoweza kuhudhuria sherehe hiyo adhimu ana kwa ana, ninachukua fursa hii kuwasalimu kwa maneno haya kwa furaha.
Papa anaeleza uhusiano wa muda mrefu
Baba Mtakatifu anaandika kuwa "Tumefahamiana kwa miaka mingi, na nimekuwa nikishukuru kila wakati kwa kujitolea kwako kwa mazungumzo, haswa kati ya Wayahudi na Wakristo. Katika miaka arobaini na miwili ya shughuli yako ya ufundishaji na kitaaluma umeathiri vyema vizazi viwili vya marabi, pamoja na wanatheolojia wa Kikatoliki na Kiprotestanti, ukiheshimu kikamilifu vipengele vya kitaaluma vya taalimungu.” Katika suala hilo, Papa amebainisha alivyoona zawadi yake ya urafiki na hekima, ambayo anamshukuru Bwana. “Hasa nakumbuka nyakati tulizotumia pamoja katika mazungumzo ambayo yalitutajirisha sana, pamoja na tafakari ulizochapisha kuhusu urafiki katika mazungumzo baina ya dini.
Papa amekumbuka ziara ya kitume huko Slovakia
Askofu wa Roma anaandika kuwa "Mawazo yangu pia yanakwenda kwenye ziara ya kukumbukwa nchini Slovakia mwaka wa 2021 na mkutano na jumuiya ya Wayahudi huko Uwanja wa Rybné, huko Bratislava, ambako Wakatoliki wengi pia walihudhuria”. “Mikutano kama hiyo Papa anaendelea katika barua hiyo ambayo imesomwa, hufungua mlango wa ukuzaji wa uhusiano wenye matunda”. Ni muhimu kwamba heshima hiyo ya juu ya kitaaluma inatolewa kwake na Chuo Kikuu cha Trnava, kilichoanzishwa katika karne ya kumi na saba na Wajesuit wenzake, ambao bado wanafanya kazi huko, ingawa katika hali tofauti. Kwa kuwa Trnava ni jiji lenye historia chungu kwa Wayahudi, uwepo wake hapo kwenye hafla hiyo ni ishara ya kukaribisha sura mpya ya historia, ambayo ulimwengu wetu unahitaji sana, Amesisitiza Papa.
Imani imetumiwa vibaya kufikia lengo la kisiasa
Baba Mtakatifu Francisko anabainisha kuwa kiukweli, kwa karne nyingi imani imetumiwa vibaya ili kufikia malengo ya kisiasa au ya kiuchumi, ambayo yanaweza tu kupunguza uthamini wa maadili ya kidini. Maisha yake yote yamejaribu kusisitiza kwamba kuishi kwa uhalisi mila ya kidini na kuheshimu haki za binadamu kusiwe na migogoro. Zaidi ya hayo, amejaribu kwa haki kuonesha kwamba watu wa imani tofauti wanaweza na lazima watetee haki za binadamu katika hali zote za maisha. Ni matumaini yake Papa kwamba kujitolea kwa majadiliano haki na kuishi pamoja kwa amani kutazidi kubainisha uhusiano kati ya wanaume na wanawake wote, bila kujali dini zao. Katika kueleza hisia hizo, Papa Francisko amemwakikishia maombi yake na kwamba tukio hilo furaha itaimarisha hasa majadiliano kati ya Wayahudi na Wakristo na mazungumzo ya kidini, na kwa furaha amwombea baraka nyingi za kimungu.