Vita kati ya Israeli na Palestina Inabomoa Matumaini ya Amani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 14 Mei 2023 amezungumzia kuhusu vita inayoendelea kati ya Waisraeli na Wapalestina, hali ambayo imepelekea watu wasiokuwa na hatia kupoteza maisha yao, wakiwemo wanawake na watoto. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, makubaliano ya kusistisha vita kati ya Israeli na Palestina kwenye Ukanda wa Gaza yaliyofikiwa tarehe 13 Mei 2023 yataheshimiwa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kwa njia ya mtutu wa bunduki amani na utulivu havitaweza kupatikana na matokeo yake maafa na uharibifu vitaendelea kushamiri kiasi hata cha kubomolea mbali matumaini ya amani. Hali ya kutoaminiana kati ya Waisraeli na Wapalestina na hivyo kudhoofisha matarajio ya kupata suluhu ya kisiasa.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, anapongeza jukumu muhimu la Misri katika kumaliza uhasama, pamoja na juhudi za Qatar, Lebanon na Marekani kufikia usitishaji mapigano kati ya Israeli na Palestina. Anatoa wito kwa pande zote kuheshimu usitishaji vita," Stéphane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu amesema katika taarifa kwa niaba ya mkuu wa Umoja wa Mataifa. Katibu Mkuu anasisitiza dhamira ya Umoja wa Mataifa ya kufikia suluhisho la Mataifa mawili kwa kuzingatia maazimio husika ya Umoja wa Mataifa, sheria za Kimataifa na makubaliano ya hapo awali, inasisitiza taarifa hiyo. Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ni suluhu ya kisiasa pekee kupitia majadiliano inayoweza kuleta amani ya kudumu na kukomesha daima "mizunguko ya vurugu" yenye uharibifu. Aidha Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa rambirambi zake kwa familia za watu waliofariki au kujeruhiwa katika siku zilizopita kutokana na mapigano katika Ukanda wa Gaza.