Papa Francisko Sherehe ya Pentekoste: Pokeeni Roho Mtakatifu: Ushuhuda!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Sherehe ya Pentekoste: Wanafunzi wanamwona Kristo Yesu Mfufuka: Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu. Naye akiisha kusema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana. Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa. Yn 20:19-23. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, Sherehe ya Pentekoste, Dominika tarehe 28 Mei 2023 amesema, sehemu hii ya Injili inawaonesha Mitume walivyokuwa wamejifungia ndani kwa hofu ya Wayahudi, baada ya mateso na kifo cha Kristo Yesu, akawatokea na kuwapatia zawadi ya Roho Mtakatifu: “Pokeeni Roho Mtakatifu.” Kumbe, Roho Mtakatifu ndiye aliyewaondolea wanafunzi wa Yesu ule woga, na kuwakirimia neema ya kutoka nje ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa ujasiri na moyo mkuu. Mateso na kifo cha Kristo Yesu kiliwavuruga wanafunzi wake, kiasi cha kujifungia! Baba Mtakatifu amekita tafakari yake kwa kitenzi hiki cha “kujifungia ndani” akiuliza ni mara ngapi waamini wamejikuta wakijifungia ndani katika ubinafsi wao wanapokumbana na hali tete na magumu ya maisha binafsi au kifamilia?
Wakati wanakumbana na mateso na mahangaiko kiasi hata cha kukosa tena fadhila ya matumaini na ujasiri wa kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu, waamini wanajikuta wakijifungia katika undani wa maisha na wasi wasi wao. Hii ina maana ya kwamba, mwamini anatoa nafasi kubwa kwa woga na wasi wasi kumtawala na hivyo kujikuta akijifungia katika undani wake. Hofu ya kushindwa kutekeleza, hofu ya kumkuta mwamini akiwa pweke mbele ya mapambano ya maisha ya kila siku, hofu ya kubaki huku akiwa ameshindwa kumudu mapambano ya maisha au kufanya maamuzi tenge. Woga unaposhika kasi, unamkandamiza muhusika na hivyo kushindwa kujinasua na hivyo kujikuta akiwa mpweke: Hivi ndivyo inavyotokea hata kwa wageni au watu waliotafuti na wanavyofikiri na kutenda tofauti. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kunawezekana kukawepo na woga hata dhidi ya Mwenyezi Mungu, kwa kumwona kuwa ni katili anayeadhibu! Ikiwa kama waamini watatoa kipaumbele cha pekee kwa hofu, woga na wasi wasi wa namna hii kutawala, kwa hakika milango yao itakuwa imefungwa: nyoyo zao, jamii na hata mlango wa Kanisa kwao, utafungwa na hii ni hatari sana kwa maisha ya kiroho. Kristo Mfufuka anawapatia Mitume zawadi ya Roho Mtakatifu anayewaokoa kutoka katika kifungo cha hofu, woga na wasi wasi.
Mitume walipompokea Roho Mtakatifu siku ile ya Pentekoste ya kwanza, wakatoka kimasomaso kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Ni kwa njia ya Roho Mtakatifu, Mitume wanashinda hofu, woga na wasi wasi na malango yanafunguka, ili kuonja ukaribu na upendo wa Mungu unaofariji, unaoangaza, unaoshinda magumu, woga na hofu ya maisha. Baba Mtakatifu Benedikto XVI anasema Roho wa Mungu anapoingia anafukuzia mbali woga na kuwajalia waamini kujisikia kwamba, wako mikononi salama mwa Mwenyezi Mungu, mwingi wa upendo na hata chochote kile kikitokea lakini upendo wa Mungu utawalinda na kuwaokoa. Kumbe, waamini wanapokabiliwa na changamoto za hofu, wasiwasi na kutaka kujifungia katika ubinafsi wao, wamwombe Roho Mtakatifu kwa ajili yao wenyewe, kwa ajili ya Kanisa na kwa ajili ya ulimwengu mzima, ili Pentekoste mpya iwashukie na hivyo kufukuzia mbali hofu inayowasonga nyoyoni mwao, ili hatimaye, waweze kuishi ule moto wa upendo wa Mungu. Bikira Maria aliyekuwa wa kwanza kujazwa na Roho Mtakatifu, awaombee waamini.