Tafuta

Papa Francisko na Patriaki Toawdros II. Papa Francisko na Patriaki Toawdros II. 

Papa na Tawadros pamoja kwa kumbukumbu ya miaka 50 ya mkutano wa Paulo VI na Shenouda III

Patriaki wa Kiorthodox wa Kikoptic atashiriki katika Katekesi ya tarehe 10 Mei. Siku itakayofuata kutakuwa na wakati wa sala ya pamoja na Papa Francisko.Dominika tarehe 14 Mei,Patriaki Tawadros ataadhimisha Liturujia ya Ekaristi kwa waamini wa Kikoptic katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yohane huko Laterano.

Na Angella Rwezaula,- Vatican.

Patriaki Tawadros II, Papa wa Alexandria na mkuu wa Kanisa la Kikoptic Kiorthodox la Misri, amefika Roma tarehe 9 Mei 2023 kwa ziara ya siku sita. Tarehe 10 na 11 Mei - kama ilivyooneshwa katika ujumbe wa Twitter kutoka Sekretarieti ya Vatican, Patriaki ataadhimisha pamoja na Papa Francisko kumbukumbu ya miaka hamsini ya mkutano wa kihistoria wa watangulizi wao,Mtakatifu Paulo VI na Papa Shenouda III,ambao ulifanyika mnamo Mei 1973. Katika hafla hiyo, Patriaki Tawadros atashiriki katika Katekesi ya  Jumatano tarehe  10 Mei. Siku ya Alhamisi tarehe 11 Mei 2023  atakuwa na mkutano wa faragha na Baba Mtakatifu Francisko, ambaye atakuwa na muda wa kusali naye, kisha atakwenda katika  Baraza la Kipapa la kuhamasisha Umoja wa Wakristo. Patriaki pia atakutana na waamini wa jumuiya ya Kikoptic wanaoishi Roma, ambao kwao ataadhimisha Liturujia ya Ekaristi tarehe 14 Mei katika Kanisa la Kipapa la Mtakatifu Yohane huko Laterano.

Katika mahojiano na vyombo vya habari vya Vatican mwezi wa Aprili mwaka 2022 na Padre Hyacinthe Destivelle, ofisa wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Kikiristo alionesha ziara hiyo muhimu, iliyofafanuliwa kama hatua muhimu katika safari ya kiekumene. Padre Destivelle alikumbuka Azimio la Pamoja lililotiwa saini na Papa Montini (Paulo VI) na Patriaki Shenouda III mnamo tarehe 10 Mei 1973, ambalo lilikuwa kielelezo cha makubaliano sawa na Makanisa mengine ya Kiorthodoksi ya Mashariki, ambayo yanatambua Mabaraza matatu ya kwanza. Kwa hiyo, alisisitiza kwamba ziara pia hufanyika miaka 10 baada ya mkutano wa kwanza kati ya Papa Francisko na Tawadros.

Katikati ya mkutano wa maombi ya  tarehe 11 Mei kutakuwa na mada ya uekumeni wa damu, kwa kumbukumbu ya mashahidi wengi wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo: Kwa Baba Mtakatifu Francisko alisema Padre Destivelle  kuwa damu ya mashahidi ni mbegu ya umoja.  Wafia imani tayari wamekusanyika mbinguni, Papa daima anasema, hawauawi kwa sababu ni Wakatoliki, Waorthodoksi au Waprotestanti bali kwa sababu wao ni Wakristo. Kwa hiyo tayari wamekusanyika katika utukufu wa Mungu kwa sababu wameteseka kwa ajili ya jina la Kristo. Damu ya mashahidi inalia zaidi kuliko migawanyiko yetu. Kanisa la Kikoptic Kiorthodox la Misri kama ilivyoripotiwa  kwenye tweet kutoka kwa Sekretarieti Vatican ni moja ya ukweli muhimu zaidi katika Mpango wa  kikanisa wa Mashariki ya Kati, ambapo, katika siku za hivi karibuni, jumuiya za Kikristo zimejikuta zikikabiliwa na hali ngumu sana.

Kwa hafla hiyo Baraza la Kipapa kwa ajili ya kuhamasisha Umoja wa Wakristo litachapisha kitabu cha ukumbusho kiitwacho: "Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox la Kikoptic. Maadhimisho ya Miaka 50 ya Mkutano kati ya Papa Paulo VI na Papa Shenouda III (1973-2023).  Kitabu hicho kina nyaraka kuu zinazoshuhudia ukaribu kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodoksi la Kikoptic tangu Mtaguso wa Pili wa Vatican, ukitanguliwa na dibaji ya pamoja ya Papa Francisko na Papa Tawadros II. Imechapishwa na Nyumba ya uchapishaji ya kitabu cha tatu katika mfululizo mpya wa “Ut Unum Sint”, yaani “ili wawe  na umoja”, wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo.

Mkutano wa Papa Francisko na Patriaki Tawadros katika afla ya miaka 50 ya mkutano kati ya Paulo VI na Shenouda III
09 May 2023, 16:14