Tafuta

Papa Francisko Kumbukumbu ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika, 25 Mei 2023. Papa Francisko Kumbukumbu ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika, 25 Mei 2023. 

Papa: Kumbukizi la Miaka 60 Tangu Kuanzishwa Kwa Umoja wa Afrika

Maadhimisho ya Siku ya Afrika kwa Mwaka 2023, kumbukizi ya Miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika, Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na watoto kadhaa kutoka Barani Afrika waliokuwa wamesindikizwa na Mabalozi, wazazi pamoja na walezi wao. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, amebainisha changamoto zinazolikabili Bara la Afrika kuwa ni pamoja na: vitendo vya kigaidi, rushwa na ufisadi wa mali ya umma,, lakini wasikate tamaa

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Umoja wa Afrika tarehe 25 Mei 2023 umeadhimisha kumbukizi ya Miaka 60 tangu kuasisiwa kwake kama Umoja wa Nchi Huru za Afrika, OAU na ambayo baadaye iligeuzwa na kujulikana kama Umoja wa Afrika. Hili ndilo chimbuko la Siku ya Afrika, ishara ya umoja, maendeleo na juhudi za kuleta uhuru na ukombozi wa kweli Barani Afrika. Ilikuwa ni Mwezi Mei 1963, wakuu 32 wa nchi huru za Kiafrika walipokutana mjini Addis Ababa, Ethiopia kusaini mkataba wa kuanzisha Umoja wa Nchi Huru za Afrika. Lengo likiwa ni kukoleza mapambano dhidi ya ukoloni, ili kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kuthamini amana na utajiri wa tamaduni za Kiafrika. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu Barani Afrika kuwa na ari na mwamko wa kutangaza na kushuhudia uzuri na ukarimu wa watu wa Bara la Afrika, katika huduma, ukweli na uwazi; kwa kuwa na ujasiri, msamaha pamoja na kuendeleza mapambano dhidi ya ukosefu wa haki kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; bila kusahau kuwa na upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, tayari kujenga na kudumisha urafiki wa kijamii.

Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi kutoka Barani Afrika
Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi kutoka Barani Afrika

Tarehe 9 Septemba, 1999 Wakuu wa nchi na serikali wa OAU walipitisha Azimio la Sirte huko Sirte nchini Libya. Umoja wa Afrika ukazinduliwa rasmi Julai 2002 huko Durban, Afrika Kusini. Maadhimisho ya miaka 60 ya Siku ya Afrika yamenogeshwa na kauli mbiu: “Afrika Yetu, Mustakbali wetu,” na maudhui ni “Kusukuma mbele Utekelezaji wa Afcfta (Taasisi ya kibiashara ya kieneo; Africa Continental Free Trade Area.) Ni katika muktadha huu wa Maadhimisho ya Siku ya Afrika kwa Mwaka 2023, kumbukizi ya Miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika, Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na watoto kadhaa kutoka Barani Afrika waliokuwa wamesindikizwa na Mabalozi, wazazi pamoja na walezi wao. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, amebainisha changamoto zinazolikabili Bara la Afrika kuwa ni pamoja na: vitendo vya kigaidi, rushwa na ufisadi wa mali ya umma, utawala mbovu, ukosefu wa fursa za ajira kwa vijana wa kizazi kipya; wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; vita, ukabila; athari za mabadiliko ya tabianchi sanjari na ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula, lakini pamoja na changamoto hizi zote, hakuna sababu ya kukata wala kukatishwa tamaa!

Vita, ukabila na vitendo vya kigaidi bado ni changamoto pevu
Vita, ukabila na vitendo vya kigaidi bado ni changamoto pevu

Baba Mtakatifu amewaambia watoto na vijana kutoka Barani Afrika kwamba, wamebarikiwa kuwa na karama na kwamba, wanayo ndoto kubwa, kamwe wasipate kishawishi cha kutaka kuzima na hatimaye kuzika ndoto zao, lakini waendelee kwa uvumilivu kufanya mang’amuzi, ili hatimaye, waweze kutambua wito wao halisi. Amana na utajiri mkubwa kutoka Barani Afrika ni kipaji cha akili. Jitihada zao katika masomo zisaidie kuendeleza mchakato wa maendeleo endelevu ya jamii. Baba Mtakatifu amewakumbuka watoto wanaopelekwa mstari wa mbele kama chambo vitani, watoto wanaoteseka kwenye vita na mipasuko ya kijamii sehemu mbalimbali za Bara la Afrika; wote hawa wanahitaji kuona ukaribu wao, ili kuwatia shime, wasikate tamaa na kujisikia kuwa wametelekezwa. Baba Mtakatifu amewataka watoto na vijana wa Afrika kujenga mahusiano na majadiliano ili kutambua asili yao. Changamoto kubwa ya maisha kwa sasa ni mapambano ya kutafuta haki, amani na maridhiano, kwani ukosefu wa amani unahatarisha mustakabali wa Jumuiya ya Kimataifa. Huu ni mwaliko kwa kukuza na kudumisha amani ndani yao na katika mazingira yanayowazunguka. Watoto na vijana wa Bara la Afrika wawe ni mabalozi wa haki na amani, ili ulimwengu uweze kugundua tena uzuri wa upendo, kwa kuishi pamoja katika ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu.

Papa Umoja wa Afrika

 

 

29 May 2023, 16:28