Tafuta

Mkutano wa Sita kati ya Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini na Taasisi ya Kifalme ya Mafunzo ya Imani Mbalimbali, "Royal Institute for Inter-Faith Studies Mkutano wa Sita kati ya Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini na Taasisi ya Kifalme ya Mafunzo ya Imani Mbalimbali, "Royal Institute for Inter-Faith Studies  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Mkutano Kati ya Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini na Taasisi ya Kifalme ya Mafunzo ya Imani

Baba Mtakatifu katika hotuba yake amemshukuru Mfalme El Hassan Bin Talal, mchango wa nchi ya Yordan huko Mashariki ya Kati, Amana na Urithi wa Kiarabu kwa Wakristo; Umuhimu wa majadiliano ya kidini kujikita katika msingi wa ukweli na uwazi pamoja na mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu nchini Uturuki na Siria kutokana na tetemeko la ardhi lililozikumba nchi hizi mbili hivi katibuni. Taasisi hii inapania kukuza Ibada, Moyo wa Sala, Kufunga na Hija.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkutano wa Sita kati ya Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini na Taasisi ya Kifalme ya Mafunzo ya Imani Mbalimbali, unanogeshwa na kauli mbiu “Ubunifu wa kawaida kati ya Ukristo na Uislamu." Washiriki wa mkutano huu, Alhamisi tarehe 4 Mei 2023 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amemshukuru Mfalme El Hassan Bin Talal, mchango wa nchi ya Yordan huko Mashariki ya Kati, Amana na Urithi wa Kiarabu kwa Wakristo; Umuhimu wa majadiliano ya kidini kujikita katika msingi wa ukweli na uwazi pamoja na mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu nchini Uturuki na Siria. Baba Mtakatifu amesema, mkutano huu umekuwa ni fursa ya kuelezea furaha yake ya ndani katika mchakato wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, kitamaduni na kiakili, kielelezo cha ujenzi wa urafiki unaosimikwa katika uaminifu, kati ya watu na uwajibikaji mpana unaopania pamoja na mambo mengine ujenzi wa udugu wa kibinadamu msingi wa mahusiano na mafungamano kati ya watu.

Papa Francisko asema majadiliano ya kidini: Ukweli na Uwazi
Papa Francisko asema majadiliano ya kidini: Ukweli na Uwazi

Baba Mtakatifu amemshukuru na kumpongeza Mfalme El Hassan Bin Talal, kwa mchango wake nchini Yordan na Mashariki ya Kati katika ujumla wake, hasa nyakati hizi ambamo vita, machafuko na ghasia zinaendelea kusikika huko Mashariki ya Kati. Ameonesha kwamba, Wakristo wanayo haki ya kuishi huko Mashariki ya Kati kama ilivyokuwa kwa wahenga wao. Taasisi ya Kifalme ya Mafunzo ya Imani Mbalimbali inayoongozwa na Mfalme El Hassan Bin Talal, kati ya malengo yake ni kuhifadhi na kulinda amana na utajiri wa Kikristo Uarabuni, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Wakristo; kwa kulinda na kuendeleza amana hii huko Mashariki ya Kati, inayosimikwa katika utajiri mkubwa wa kikabila, kidini, kitamaduni, lugha na mapokeo mbalimbali. Hii ni changamoto pale inapowezekana ya kujenga ushirikiano kati ya Taasisi za Kikristo na Kiislam zenye malengo kama hayo. Majadiliano ya kidini wanayoyatekeleza yanapaswa kusimikwa katika misingi ya ukweli na uwazi, kwa kutambua mwingiliano na tofauti zao msingi; kwa kukazia zaidi yale mambo yanayowaunganisha katika msingi wa maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili.

Papa anawakumbuka wahanga wa tetemeko la ardhi
Papa anawakumbuka wahanga wa tetemeko la ardhi

Taasisi hii inapania pamoja na mambo mengine, kutoa kipaumbele cha pekee kwa Ibada ya Kumwabudu Mungu mmoja; kuhimiza moyo wa sala, kufunga na kutoa sadaka; hija za maisha ya kiroho, matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na huduma kwa: watoto yatima, wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; wajane, wagonjwa, wazee, wakimbizi na wahamiaji. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, baada ya kifo, kuna maisha na uzima wa milele, mwishoni mwa maisha waamini watahukumiwa kadiri ya matendo yao, kwa kupata tuzo ya maisha ya uzima wa milele au kuhukumiwa. Lengo la waamini ni kupata maisha mazuri yanayomtolea Mwenyezi Mungu utukufu na kuwashirikisha furaha wale wote wanaokutana nao katika hija ya maisha yao hapa duniani. Baba Mtakatifu ameonesha masikitiko yake makuu kutokana na hali tete inayowakabili watu wa Mungu nchini Uturuki na Siria, walioathirika kutokana na tetemeko la ardhi lililosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Waamini na watu wenye mapenzi mema wajibidiishe kuwasaidia watu hawa. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu amewashukuru kwa kumtembelea na kuwatakia heri ili watu wote waweze kuishi kama ndugu wamoja katika misingi ya amani, usalama na utu!

Majadiliano ya Kidini
04 May 2023, 14:32