Mfuko wa Kumbukumbu ya Sinema za Kikatoliki, MAC, Mbioni Kuanzishwa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa Kitume wenye mfumo wa Barua Binafsi “Motu Proprio” “Cura vigilantissima,” yaani Sheria Kuhusu Kumbukumbu ya Kiti Kitakatifu, alikazia umuhimu wa kulinda kumbukumbu za Kiti Kitakatifu popote pale zilipo kwa ajili ya kurithisha amana na utajiri huu kwa vizazi vijavyo hasa kwa kuendelea kutumia njia na mifumo mipya katika mchakato wa kuhifadhi kumbukumbu hizi kadiri ya maono yaliyokuwa yanatolewa na Mababa watakatifu. Huu ni urithi mkubwa wa vyanzo vya kihistoria unaopaswa kurithishwa kwa vizazi vijavyo bila kubadilika. Nyaraka hizi zina thamani kubwa mintarafu historia, maisha na utume wa Mama Kanisa. Ni katika muktadha huu wa umuhimu wa kuhifadhi nyaraka hizi, Baba Mtakatifu Francisko ametuma ujumbe kwa mkutano wa kwanza wa Kamati ya Kisayansi ya Mfuko wa Kumbukumbu za Sinema za Kikatoliki “Foundation Audiovisual Memories of Catholicism.”
Baba Mtakatifu anasema, hii ni dhamana na wajibu wa Kanisa zima kulinda na kutunza amana na urithi huu mintarafu kanuni na vigezo vya kisayansi. “MAC Foundation Audiovisual Memories of Catholicism” iko chini ya usimamizi wa Monsinyo Dario Edoardo Viganò, Makamu Mkuu wa Taasisi za Kipapa za Elimu ya Sayansi na Sayansi jamii. Lengo la kuanzishwa kwa Mfuko huu ni kuitikia kwa haraka hitaji la upatikanaji, utunzaji na kuendelea kuthamanisha amana na utajiri wa nyaraka za Sinema mintarafu Ukatoliki. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko umesomwa Jumanne tarehe 2 Mei 2023 kwa niaba yake na Askofu mkuu Angelo Vincenzo Zani Mhifadhi mkuu wa Nyaraka za Kanisa na Mkutubi mkuu wa Maktaba ya Kanisa Katoliki, ambaye amakazia umuhimu wa Mfuko huu kushirikiana na Taasisi nyingine, ili kupata mwelekeo mpana, mbinu mkakati unaosimikwa katika wajibu, rasilimali na huduma ya kurithisha kumbukumbu ya Sinema hizi kwa vizazi vijavyo! Mkutano huu unalenga pamoja na mambo kuanza mchakato utakaopelekea kuanzishwa kwa Taasisi ya Hifadhi ya Kumbukumbu ya Sinema ya Vatican na Kanisa katika ujumla wake.