Tafuta

Kumbukizi ya Miaka 125 tangu Mtakatifu Antonio Maria Zaccaria atangazwe kuwa Mtakatifu kunako mwaka 1897. Kumbukizi ya Miaka 125 tangu Mtakatifu Antonio Maria Zaccaria atangazwe kuwa Mtakatifu kunako mwaka 1897.  (REMO CASILLI)

Kumbukizi ya Miaka 125 Tangu Mtakatifu Antonio Maria Zaccaria Atangazwe kuwa Mtakatifu

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 29 Mei 2023 amekutana na kuzungumza na wanashirika hawa kwa kukazia mambo makuu matatu: mahusiano na mafungamano yao na Kristo Yesu, Ari na Mwamko wa Kitume na Ujasiri wa ugunduzi. Mtakatifu Antonio Maria Zaccaria kama msingi wa maisha na utume wake, alijielekeza zaidi kwa Mwenyezi Mungu, kwa kufanya tafakari ya kina ya Neno la Mungu; akajizatiti zaidi kwa ajili ya kufundisha Katekesi na Utume wa Kipadre.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Antonio Maria Zaccaria, Padre na Daktari alizaliwa mwaka 1502 na kufariki dunia 5 Julai 1539. Papa Leo XIII akamtangaza kuwa Mtakatifu mwaka 1897. Ni muasisi wa Shirika la Mtakatifu Paulo, wanaojulikana zaidi kama “Barnabiti” kwa sababu makao yao makuu ya kwanza yalianzishwa kwenye Jimbo kuu la Milano kwenye Kanisa la Mtakatifu Barnaba. Kumbe mwaka 2023 Shirika hili ambalo lina Wanashirika Mapadre, Watawa na Wanafamilia wa kiroho wa Mtakatifu Antonio Maria Zaccaria wanaadhimisha kumbukizi ya Miaka 125 tangu alipotangazwa kuwa Mtakatifu sanjari na maandalizi ya mkutano mkuu wa Shirika. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 29 Mei 2023 amekutana na kuzungumza na wanashirika hawa kwa kukazia mambo makuu matatu: mahusiano na mafungamano yao na Kristo Yesu, Ari na Mwamko wa Kitume na Ujasiri wa ugunduzi. Mtakatifu Antonio Maria Zaccaria kama msingi wa maisha na utume wake, alijielekeza zaidi kwa Mwenyezi Mungu, kwa kufanya tafakari ya kina ya Neno la Mungu; akajizatiti zaidi kwa ajili ya kufundisha Katekesi, akazama zaidi katika maisha na utume wa Kikasisi hadi kuwa ni Muasisi wa Shirika la “Barnabiti.” Huu ni uzoefu unaopyaishwa kwa kufurahia urafiki na Kristo Yesu pamoja na ujumbe wake; kumfahamu, kumtafakari, kumwabudu na hatimaye kupata amani ya ndani na kwa njia ya Kristo Yesu mwamini anapata maana ya ndani ya maisha yake, kwa kuhisi uwepo wake wa daima katika kazi za kimisionari na hivyo kupata hamasa na upendo wa kuwashawishi wengine. Rej. Evangelii gaudium, 266.

Ushuhuda wenye mvuto ni msingi wa uinjilishaji mpya
Ushuhuda wenye mvuto ni msingi wa uinjilishaji mpya

Utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu unasimikwa katika ushuhuda wenye mvuto mashiko na wala si wongofu wa shuruti. Huu ni mwaliko wa kujitoa na kujisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo kwa jirani, ili kuwa ni mashuhuda wa furaha ya Injili, kwa kuwainjilisha walimwengu kwa kumpeleka Kristo Yesu aliye hai kati ya watu wa Mataifa, ni mwaliko wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Mfufuka. Ujasiri wa ugunduzi unawawezesha wanashirika kwa kuwa hali zote kwa watu wote,  ili kwa njia zote wapate kuwaokoa watu, bila kukata tamaa mbele ya vikwazo na magumu ya maisha. Hivi ndivyo alivyofanya Mtakatifu Antonio Maria Zaccaria akaanzisha Shirika lililoleta mageuzi makubwa katika maisha ya Mapadre na Watawa, kiasi cha kujisadaka katika mchakato wa uinjilishaji, huku wakiendelea kubaki waaminifu katika tunu msingi za Kiinjili, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa. Mtakatifu Antonio Maria Zaccaria alifanya mageuzi haya ndani ya Kanisa, akakubali kukosolewa na kutumia fursa zote alizojaliwa kufafanua sababu msingi zilizopelekea yeye kufanya maamuzi kama yale, huku akiendelea kujikita katika ushirika na utii. Baba Mtakatifu Francisko anawataka wanashirika hawa kushirikiana na kushikamana katika maisha na utume wao, kwa kuondokana na tabia ya uchoyo na ubinafsi, kama sehemu ya vinasaba vya maisha ya Kikristo, ili wote wawe wamoja. Huu ni mwaliko wa kufanya kazi kwa pamoja, kusali, kufurahi na kuteseka kwa pamoja na kama jumuiya wawaendee watu wa Mungu kwa ajili ya huduma kama alivyofanya Bikira Maria alipomtembelea binamu yake Elizabeti.

Papa Barnabiti

 

 

 

29 May 2023, 15:47