Tafuta

Baba Mtakatifu akiwa njiani kurejea kutoka nchini Hungaria, alipata nafasi ya “kuchonga” na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake, kwa kujibu maswali matano. Baba Mtakatifu akiwa njiani kurejea kutoka nchini Hungaria, alipata nafasi ya “kuchonga” na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake, kwa kujibu maswali matano.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Hungaria: Mahojiano na Waandishi wa Habari

Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kurejea kutoka nchini Hungaria, alipata nafasi ya “kuchonga” na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake, kwa kujibu maswali matano yaliyohusu: Mtazamo wake kuhusu Hungaria; Ukarimu na upendo kwa wakimbizi na wahamiaji; Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni, Jimbo kuu la Lisbon, Ureno kuanzia tarehe 1 – 6 Agosti 2023na hatimaye, majadiliano ya kiekumene na kitamaduni, pamoja na hija zake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya 41 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Hungaria kuanzia tarehe 28 hadi tarehe 30 Aprili 2023 imenogeshwa na kauli mbiu “Kristo ndiye wakati wetu ujao.” Ni hija ambayo imejikita katika mihimili mikuu mitatu: Baba Mtakatifu Francisko kama hujaji wa amani katikati ya Bara la Ulaya, ambako misimamo mikali ya utaifa na kampeni za vita zikiendelea kupamba moto! Hii ni hija iliyopania pamoja na mambo mengine, kukoleza ari na moyo wa ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji nwanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Ni hija ambayo ilipania kuwaimarisha watu wa Mungu nchini Hungaria katika imani, matumaini na mapendo, kwa kukazia dhamana na wajibu wa familia na ukarimu unaopata chimbuko lake katika maisha ya watu wa Mungu nchini Hungaria. Baba Mtakatifu akiwa njiani kurejea kutoka nchini Hungaria, alipata nafasi ya “kuchonga” na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake, kwa kujibu maswali matano yaliyohusu: Mtazamo wake kuhusu Hungaria; Ukarimu na upendo kwa wakimbizi na wahamiaji; Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni, Jimbo kuu la Lisbon, Ureno kuanzia tarehe 1 – 6 Agosti 2023 na hatimaye, majadiliano ya kiekumene na kitamaduni. Baba Mtakatifu Francisko anasema, anao uzoefu na mang’amuzi chanya kuhusu watu wa Mungu nchini Hungaria, kwani amewahi kufanya utume wake nchini humo, uhusiano wake na Masista wa Bikira Maria wa Ward, waliokuwa wanaishi uhamishoni, kiasi kwamba alionja adha ya kuishi uhamishoni. Alibahatika kufahamiana kwa karibu na Kardinali Mindszenty na kwamba, watu wa Mungu nchini Hungaria wamebahatika kuwa na utamaduni unaogusa maisha ya watu wote, mtindo wa maisha ambao katika maisha yake amebahatika kuufahamu.

Baba Mtakatifu Francisko anawasifu watu wa Mungu nchini Hungaria
Baba Mtakatifu Francisko anawasifu watu wa Mungu nchini Hungaria

Baba Mtakatifu akiwa nchini Hungaria ameitaka Jumuiya ya Kimataifa kufungua malango ya ubinafsi na uchoyo kwa wakimbizi na wahamiaji. Amani ya kweli inajengeka kwa watu kukutana na kuzungumza katika msingi wa ukweli na uwazi. Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji linapaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, kwani kwa sasa wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji linashughulikiwa zaidi na nchi tano yaani: Cyprus, Ugiriki, Malta, Italia na Hispania. Umoja wa Ulaya unapaswa kuunganisha nguvu, ili kukabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji. Wimbi la wakimbizi na wahamiaji lina uhusiano pia na idadi ndogo sana ya watoto wanaozaliwa kwa mfano nchini Hispania na Italia, changamoto hii ni tishio. Lakini Uswis ni nchi ambayo imeonesha mfano mzuri wa kuigwa katika sera na mikakati yake kwa wakimbizi na wahamiaji. Baba Mtakatifu alipata nafasi ya kukutana kwa faragha na Askofu mkuu Hilarion Alfeyev wa Jimbo kuu la Volokolamsk ambaye pia ni Mjumbe wa Sinodi Takatifu na Mwenyekiti wa Idara ya Mahusiano ya nje ya Kanisa la Kiorthodox la Urussi na Moscow nzima. Baba Mtakatifu anasema, huyu ni kiongozi mwenye akili na busara na daima mazungumzko yao yamejikita katika majadiliano ya kiekumene. Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameambatana na Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo, Jumatano jioni tarehe 16 Machi 2022 alipata nafasi ya kuzungumza kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya jamii na Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Urussi nzima. Patriaki Cyril alikuwa ameambatana pia na Askofu mkuu Hilarion Alfeyev wa Jimbo kuu la Volokolamsk ambaye pia ni Mjumbe wa Sinodi Takatifu na Mwenyekiti wa Idara ya Mahusiano ya nje ya Kanisa la Kiorthodox la Urussi na Moscow nzima. Kiini cha mazungumzo haya ni uvamizi wa kijeshi uliofanywa na majeshi ya Kirussi nchini Ukraine, dhamana na wajibu wa Wakristo na viongozi wao katika kuhamasisha majadiliano katika ukweli na uwazi, ili haki, amani na maridhiano viweze kushika mkondo wake.

Majadiliano ya kiekumene ni muhimu
Majadiliano ya kiekumene ni muhimu

Baba Mtakatifu Francisko alitumia fursa hii kumshukuru na kumpongeza Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Urussi nzima kwa kushiriki katika mazungumzo haya kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya jamii. Kama viongozi wa Makanisa wanasukumwa kuonesha dira na mwongozo unaopaswa kufuatwa na waamini wao, katika mchakato wa kutafuta amani; huku wakiendelea kujikita katika kusali na kuombea haki, amani na maridhiano kati ya watu, ili hatimaye, vita iweze kukoma na amani kutamalaki. Kanisa linapaswa kutumia lugha ya Kristo Yesu, yaani upendo na wala si lugha ya wanasiasa. Baba Mtakatifu alikumbusha kwamba, wao ni viongozi wa watu wanaomwamini Mungu, Fumbo la Utatu Mtakatifu na Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa. Ni katika muktadha huu, viongozi wa Makanisa hawana budi kushikamana na kuungana kwa pamoja ili kutafuta amani, kuwasaidia wale wanaoteseka kutokana na vita pamoja na kuongeza juhudi za kusitisha vita. Viongozi hawa wakuu wa Makanisa wamekazia umuhimu wa majadiliano katika ukweli na uwazi kama njia ya kufikia amani ya kweli na ya kudumu. Hii inatokana na ukweli kwamba, wanaoathirika na mashambulizi haya ya kivita ni watu wa kawaida na wanajeshi wa Urussi wanaojikuta wakipoteza maisha yao kutokana na vita.

Waathirika wakuu wa vita ni raia wasiokuwa na hatia
Waathirika wakuu wa vita ni raia wasiokuwa na hatia

Makanisa hayana budi kuwa karibu zaidi na watu wa Mungu wanaoendelea kuteseka kutokana na vita. Baba Mtakatifu anasema “dhana ya vita ya haki na halali” kwa sasa imepitwa na wakati kama ilivyo pia kwa adhabu ya kifo kwani inakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu, utakatifu na zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anapinga kwa nguvu zote utamaduni wa kifo! Vita ni kielelezo cha kushindwa kwa siasa na utu na inabaki kuwa ni aibu kwa Jumuiya ya Kimataifa. Kwa sasa kuna uelewa na kiu kubwa ya kutaka amani na watu wamekwisha kujifunza madhara ya vita. Makanisa yanapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kujenga msingi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu. Kuna watoto, wanawake na wazee wasiokuwa na hatia wanaoendelea kupoteza maisha yao kutokana na uvamizi wa kivita nchini Ukraine. Roho Mtakatifu anayewaunganisha katika huduma kama viongozi wakuu wa Makanisa anawataka wawasaidie waathirika wa vita. Baba Mtakatifu anasema, kulikuwa na mpango kwa viongozi wakuu wa Makanisa haya mawili kukutana mjini Yerusalemu mwezi Juni au Julai, 2022 lakini kutokana na vita kati ya Urussi na Ukraine, mkutano huu ukafutwa. Askofu mkuu Hilarion Alfeyev wa Jimbo kuu la Volokolamsk na Baba Mtakatifu kwa pamoja wamezungumzia masuala ya amani kati yake na viongozi wa Kanisa la Kiorthodox na Urussi katika ujumla wake.

Majadiliano ya kidini kwa ajili ya ujenzi wa haki na amani
Majadiliano ya kidini kwa ajili ya ujenzi wa haki na amani

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni, Jimbo kuu la Lisbon, Ureno kuanzia tarehe 1 – 6 Agosti 2023, ni hija ya maisha ya kiroho, changamoto na mwaliko kwa waamini lakini hasa vijana wa kizazi kipya, kuguswa na moyo wa unyenyekevu, sadaka na majitoleo kwa wengine kama alivyofanya Mtakatifu Yosefu. Awe ni mfano bora wa ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya udugu wa kibinadamu katika maisha! Baba Mtakatifu anawataka vijana kujisikia kuwa ni sehemu muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaosimikwa katika huduma ya upendo! Hija ya Kitume nchini Ureno ni kati ya changamoto zilizoko mbele ya Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu, sanjari na afya yake ambayo anapaswa kuipatia kipaumbele cha kwanza. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano Alasiri, tarehe 29 Machi 2023 alipelekwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, iliyoko mjini Roma kufanyiwa uchunguzi na kubainika kwamba, alikuwa anakabiliwa na changamoto katika mfumo wa hewa na kwamba, huu si Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Madaktari wakalazimika kumlaza Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya uchunguzi wa kiafya na matibabu zaidi, zoezi lililohitaji siku kadhaa na muda wa mapumziko. Matibabu yalikwenda vyema na mwili ukaitikia vizuri matibabu na hatimaye, akaruhusiwa kutoka Hospitalini na kuendelea na utume wake. Baba Mtakatifu ametia nia ya kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni, Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno. Bado hija yake ya kitume Marsiglia na Mongolia ziko pale pale.

Papa Francisko ametia nia ya kushiriki Siku ya Vijana Duniani 2023
Papa Francisko ametia nia ya kushiriki Siku ya Vijana Duniani 2023

Katika siku za hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko amerejesha mali kale kutoka kwenye Jumba la Makumbusho ya Vatican kwenda nchini Ugiriki. Usiibe! Amri ya Saba yakataza kuchukua na kuwa na mali ya jirani bila haki na kumtendea ubaya kwa namna yoyote kuhusiana na mali yake. Inaamuru haki na mapendo katika kutunza mali ya kidunia na matunda ya kazi ya watu. Kwa ajili ya manufaa ya wote, inadai kujali lengo la wote la mali na heshima ya haki ya mtu kumiliki mali yake. Maisha ya Kikristo yafanya juhudi kupanga mali za ulimwengu huu kwa ajili ya Mungu na kwa ajili Ya upendo kwa jirani. Rej. KKK 2401. Kumbe, kurejesha mali kale nchini Ugiriki ni tendo la haki na kwamba, Vatican inaendelea kufanya mang’amuzi kwa kila tukio na kwamba, Vatican iko mbioni kurejesha mali kale za wazawa wa Canada kama sehemu ya utakaso dhidi ya ubaya waliotendewa watu hawa enzi ya ukoloni. Pale inapowezekana kurejesha mali kale, Vatican itafanya hivyo katika ukweli na uwazi, kamwe kusijengeke tabia ya kuiba mali ya wengine. Kwa njia ya diplomasia Vatican imeendelea kuchangia kutafuta suluhu ya vita kati ya Urussi na Ukraine, kwa kusaidia mchakato wa mabadilishano ya wafungwa wa kivita. Kumbe, juhudi za kuwarejesha watoto wa Ukraine waliochukuliwa kwa nguvu na Urussi ni tendo la kibinadamu na kiungwana. Jambo kama hili wanapaswa kutendewa hata wanawake na wasichana wanaokimbilia nchini Italia, Hispania, Poland na Hungaria. Utu, heshima na haki zao msingi zinapaswa kulindwa na kuthaminiwa. Wakimbizi na wahamihaji walindwe na kuheshimiwa!

Papa Mahojiano Hungaria

 

01 May 2023, 13:36