Tafuta

Katekesi: Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Hungaria: Muhtasari ya Yaliyojiri

Papa amekazia mambo makuu mawili: mizizi na madaraja. Hija hii ilijikita katika historia ya watu wa Mungu inayosimika mizizi yake kati ya watakatifu, mashuhuda na raia wa kawaida, lakini wachapakazi. Huu ni ushuhuda ambao Baba Mtakatifu amefanya mang’amuzi juu yake alipokutana na kuzungumza na Kanisa mahalia na vijana, lakini ni watakatifu wa Mungu waliosadaka maisha yao kwa ajili ya ndugu zao; ni watakatifu ambao wametangaza na kushuhudia Injili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya 41 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Hungaria kuanzia tarehe 28 hadi tarehe 30 Aprili 2023 imenogeshwa na kauli mbiu “Kristo ndiye wakati wetu ujao.” Ni hija ambayo imejikita katika mihimili mikuu mitatu: Baba Mtakatifu Francisko kama hujaji wa amani katikati ya Bara la Ulaya, ambako misimamo mikali ya utaifa na kampeni za vita zikiendelea kupamba moto! Hii ni hija iliyopania pamoja na mambo mengine, kukoleza ari na moyo wa ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Ni hija ambayo ilipania kuwaimarisha watu wa Mungu nchini Hungaria katika imani, matumaini na mapendo, kwa kukazia dhamana na wajibu wa familia na ukarimu unaopata chimbuko lake katika maisha ya watu wa Mungu nchini Hungaria. Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 3 Mei 2023 imenogeshwa kwa sehemu ya Maandiko Matakatifu yasemayo: “Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu; tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka. Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa kwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali; ili kwamba kujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo (1Pet. 1:3.4.6-7). Baba Mtakatifu anawashukuru wale wote waliojisadaka kwa ajili ya kuandaa na hatimaye, kufanikisha hija yake ya kitume nchini Hungaria.

Papa Francisko anawashukuru wote waliofanikisha hija yake nchini Hungaria
Papa Francisko anawashukuru wote waliofanikisha hija yake nchini Hungaria

Katika tafakari yake amejikita katika mambo makuu mawili: mizizi na madaraja. Hija hii ilijikita katika historia ya watu wa Mungu inayosimika mizizi yake kati ya watakatifu, mashuhuda na raia wa kawaida, lakini wachapakazi. Huu ni ushuhuda ambao Baba Mtakatifu Francisko amefanya mang’amuzi juu yake wakati alipokutana na kuzungumza na Kanisa mahalia na vijana, lakini ni watakatifu wa Mungu waliosadaka maisha yao kwa ajili ya ndugu zao; ni watakatifu ambao wametangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika upendo, wakawa ni mwanga angavu wakati wa giza nene la maisha ya watu wa Mungu nchini Hungaria, changamoto na mwaliko wa kuondokana na woga na wasiwasi wa kesho, kwa kukumbuka kwamba, “Kristo ndiye wakati wetu ujao.” Mizizi ya Kikristo ya watu wa Mungu nchini Hungaria ilipitia changamoto pevu, wakati wa madhulumu na nyanyaso dhidi ya Kanisa kwa miaka 1900, viongozi wa Kanisa wakauwawa kinyama na wengine kunyimwa uhuru kabisa. Watesi wao wakajaribu kuukata mti wa imani, lakini mizizi ikabaki salama salimini! Hili ni Kanisa lililokuwa mafichoni, wakleri wake wakiwa wanapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa kificho; wakatangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu huku wakiwa wamefungwa magerezani, wakiwa wanafanya kazi viwandani na wazee wakaendelea kuwainjilisha wajukuu zao.

Mashuhuda wa imani na matumaini nchini Hungaria.
Mashuhuda wa imani na matumaini nchini Hungaria.

Utawala wa Kinazi na Kikomunisti, ulipelekea dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wayahudi, lakini kuna baadhi ya wananchi waliojitoa mhanga kwa ajili ya kuwalinda na kwa hakika mizizi yao ikawa imara na hatimaye imani thabiti ya watu wa Mungu ikasaidia kuwarejeshea watu uhuru wao. Hata leo hii, Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, uhuru wa watu wa Mungu uko hatarini kutokana na ulaji wa kupindukia na baadhi ya watu kumezwa na malimwengu, kiasi cha kuhatarisha mizizi ya watu wa Mungu Barani Ulaya. Leo hii ni vigumu sana kwa Bara la Ulaya kujisikia kuwa ni jumuiya inayosimikwa katika uzuri sanjari na uundaji wa familia. Huu ni mwaliko wa kulinda na kudumisha mizizi ili hatimaye, iweze kuzaa matunda yanayokusudiwa. Kumbukumbu hai iwasaidie waamini kulinda mizizi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wake.

Mammbo makuu mawili: Mizizi na madaraja ya kuwakutanisha watu
Mammbo makuu mawili: Mizizi na madaraja ya kuwakutanisha watu

Baba Mtakatifu anasema, kielelezo cha pili ni madaraja ya kuwakutanisha watu. Mji wa Budapest ulianzishwa takribani miaka 150 iliyopita na huu ni muungano wa miji mikuu mitatu inayounganishwa na madaraja, changamoto na mwaliko kwa viongozi wa kisiasa na kidiplomasia kuhakikisha kwamba, wanajenga madaraja ya amani kati ya watu wa Mungu na kwamba, Bara la Ulaya lina dhamana ya kuhakikisha kwamba, linajenga madaraja ya amani, kwa kukubali na kupokea tofauti zinazojitokeza pamoja na kuonesha ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji. Hili ni daraja la ubinadamu ambalo linajengwa na idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji kutoka nchini Ukraine. Baba Mtakatifu anatoa pongezi kwa Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini Hungaria. Hii ni nchi ambayo inapaswa pia kujenga madaraja kwa ajili ya siku za usoni; kwa kujikita katika ikolojia fungamani; kwa kujenga madaja kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee. Hii ni changamoto endelevu inayowataka watu wa Mungu nchini Hungaria kupyaisha imani yao na kuendelea kumgundua Kristo Yesu kila kukicha. Baba Mtakatifu anakumbuka kwa heshima na taadhima maadhimisho yote ya Liturujia Takatifu, Vipindi vya Ibada na Sala vilivyowashirikisha waamini wa Kanisa la Wakatoliki wa Kigiriki. Hapa kulijengeka daraja kati ya waamini wa madhehebu na dini mbalimbali.

Papa Francisko amevutiwa na Liturujia, Sala na Ibada mbalimbali
Papa Francisko amevutiwa na Liturujia, Sala na Ibada mbalimbali

Dominika tarehe 30 Aprili 2023, waamini wa madhehebu na Makanisa mbalimbali walishiriki katika Ibada ya Misa Takatifu, kilelelezo cha maridhiano, amani na utulivu miongoni mwa watu wa Mungu nchini Hungaria. Jambo la msingi kwa kila mwamini ni kujiuliza ikiwa kama mwamini mmoja mmoja, au familia na Parokiani kwao wanajibiisha kuwa wajenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu, ili kujenga na kudumisha amani, maridhiano na umoja? Baba Mtakatifu anasema ameguswa sana na umuhimu wa Muziki katika safari hii, kiasi kwamba, muziki umekuwa ni chombo cha ujenzi wa: utulivu, udugu wa kibinadamu ambao kimsingi ni chimbuko la matumaini na furaha ya maisha. Baba Mtakatifu Francisko anasema, mwanzoni mwa Mwezi Mei, watu wa Mungu nchini Hungaria wanautolea mwezi huu kwa heshima ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Malkia ambaye tangu Mtakatifu Stefano alipowaweka wakfu watu wake kwa Bikira Maria, Malkia. Mwishoni mwa katekesi yake, Baba Mtakatifu Francisko aliwaweka watu wote wa Mungu nchini Hungaria chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Malkia wa amani, anawaaminisha watu wote wa Mungu katika mchakato wa ujenzi wa madaraja Ulimwenguni, ili hatimaye waweze kuzamisha mizizi yao katika upendo kwa Mwenyezi Mungu.

Papa Hungaria
03 May 2023, 14:52

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >