Tafuta

Watu wa Mungu nchini Hungaria wanamheshimu na kumpenda sana Baba Mtakatifu Francisko kama ilivyojionesha katika siku hizi tatu ambazo zimesheheni matukio, sala na ujumbe mbalimbali. Watu wa Mungu nchini Hungaria wanamheshimu na kumpenda sana Baba Mtakatifu Francisko kama ilivyojionesha katika siku hizi tatu ambazo zimesheheni matukio, sala na ujumbe mbalimbali.  (Vatican Media)

Kardinali Péter Erdő: Hungaria Wameonesha Heshima na Upendo Mkuu Kwa Papa

Kardinali Péter Erdő, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria katika mahojiano maalum na Vatican News, amegusia kuhusu mambo msingi yaliyopewa kipaumbele cha kwanza na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya Kitume nchini Hungaria: Amani, Wakimbizi na Wahamiaji pamoja Utamaduni wa watu kukutana! Watu wa Mungu nchini Hungaria wamemwonesha heshima na upendo mkuu Papa Francisko wakati wa hija yake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya 41 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Hungaria kuanzia tarehe 28 hadi tarehe 30 Aprili 2023 imenogeshwa na kauli mbiu “Kristo ndiye wakati wetu ujao.” Kardinali Péter Erdő, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria katika mahojiano maalum na Vatican News, amegusia kuhusu mambo msingi yaliyopewa kipaumbele cha kwanza na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya Kitume nchini Hungaria: Amani, Wakimbizi na Wahamiaji pamoja Utamaduni wa watu kukutana! Watu wa Mungu nchini Hungaria wanamheshimu na kumpenda sana Baba Mtakatifu Francisko kama ilivyojionesha katika siku hizi tatu ambazo zimesheheni matukio, sala na ujumbe mbalimbali ambao kwa hakika watu wa Mungu nchini Hungaria wanawajibika kikamilifu mbele ya Mungu. Kwa muda wa miaka miaka miwili, wamejiandaa kumpokea na kumkaribisha Baba Mtakatifu kwa ajili ya kufunga Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa. Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kitaifa na Kimataifa katika maisha na utume wa Kanisa ni katekesi endelevu inayogusa: Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwanga linalobubujika kutoka katika Neno la Mungu linalohitaji: kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo cha imani tendaji. Lina hitaji usikivu wa kiibada na ukimya wa kitafakari uwezeshao Neno la Mungu kugusa akili na mioyo ya watu. Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho na kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati ya waja wake. Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu. Maadhimisho ya Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “52nd International Eucharistic Congress” (IEC) kuanzia tarehe 5-12 Septemba 2021, huko Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, nchini Hungaria yaliongozwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako” Zab. 87:7.

Ushiriki wa watu wa Mungu Katika Ibada umetia fola
Ushiriki wa watu wa Mungu Katika Ibada umetia fola

Baba Mtakatifu Francisko alishiriki katika Ibada ya Misa Takatifu ya kufunga Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa hapo tarehe 12 Septemba 2021. Kongamano hili pamoja na mambo mengine lilipania: Kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene, kidini na kitamaduni ili kunogesha na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu nchini Hungaria. Wakati huu, Baba Mtakatifu amewatembelea katika Kipindi hiki cha Pasaka na hivyo kuwashirikisha Neno la Mungu! Watu wa Mungu wamejitahidi kujibu ujio wa Baba Mtakatifu kwa ukarimu wa kichungaji, kwa kutambua kwamba, Baba Mtakatifu ni Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kardinali Péter Erdő, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, anasema, kati ya mambo ambayo yameacha chapa ya kudumu katika akili na moyo wake ni pale Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuanza Ibada ya Misa Takatifu, Dominika tarehe 30 Aprili 2023 alipozunguka Uwanja wa Kossuth. Watu wengi walitamani Baba Mtakatifu awabariki watoto wao na kweli alifanya hivyo na kwa hakika watu wengi walionesha furaha yao. Mara baada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu aliposali mbele ya Picha ya Bikira Maria wa Miujiza, tukio ambalo linawarejesha watu wa Mungu wakati wa vita na jinsi ambavyo Kanisa kuu lilivyoharibiwa. Watu wengine wamejaliwa kupata miujiza kutoka katika Picha hii.

Picha ya Bikira Maria Wa Miujiza.
Picha ya Bikira Maria Wa Miujiza.

Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu amemwomba Bikira Maria awatazame watu wa Mungu nchini Ukraine na Urussi, ili waweze kukomesha vita, ili haki, amani na maridhiano yaweze kurejea tena. Baba Mtakatifu Francisko ametembelea Hungaria kama hujaji wa amani na kwamba, Hungaria daima imekuwa mstari wa mbele kwa ajili ya kuombea amani nchini Ukraine na Urussi, kwa kutambua kwamba, wote ni watoto wapandwa wa Bikira Maria, kumbe ni ndugu wamoja. Hungaria inatoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji milioni moja na nusu. Wamewapatia makazi, fursa za ajira, nafasi za watoto na vijana wao kuendelea na masomo. Baba Mtakatifu Francisko amepata fursa ya kukutana na kuzungumza na wakimbizi na wahamiaji kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Elizabeth wa Hungaria.

Kardinali Peter Erdo

 

01 May 2023, 13:11