Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 20 Aprili 2023 amekutana na kuzungumza na viongozi wa kidini na wanasiasa mashuhuri kutoka Manchester, Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 20 Aprili 2023 amekutana na kuzungumza na viongozi wa kidini na wanasiasa mashuhuri kutoka Manchester,   (ANSA)

Papa Francisko: Utunzaji Bora wa Mazingira ni Wajibu wa Kimaadili na Kiutu Kwa Watu Wote

Viongozi wa kidini na kisiasa wanapaswa kujizatiti vyema kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, kwani mazingira ni sehemu muhimu sana ya kazi ya uumbaji, kumbe kwa viongozi wote huu ni wajibu wa kimaadili. Hii ni changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 20 Aprili 2023 alipokutana na kuzungumza na viongozi wa kidini na wanasiasa mashuhuri kutoka Manchester, waliomtembelea mjini Vatican. Mazingira ni kazi ya uumbaji

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume kuhusu utunzaji bora wa mazingira, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote anasema, mazingira ni kito cha thamani kwa ajili ya wote na kwamba, mazingira yana uhusiano wa pekee na maisha ya binadamu. Ongezeko la kiwango cha joto duniani linaendelea kusababisha ongezeko la kina cha maji ya bahari; ukame na mafuriko; dhoruba pamoja na majanga asilia. Hapa mwanadamu anahamasishwa kubadili mtindo wa maisha na maendeleo, kwa kuambata teknolojia rafiki kwa mazingira. Madhara ya mabadiliko ya tabianchi anasema Baba Mtakatifu yamepelekea baadhi ya watu kutumbukizwa katika utamaduni wa kutopea kwa imani, kutukuzwa kwa malimwengu na ubaridi wa imani mambo yanayoendelea kusababisha baadhi ya watu kutumbukizwa katika utumwa mamboleo na kazi za suluba; tatizo la kuwatelekeza wazee na kuwanyanyasa watoto, kwa mafao ya mtu binafsi. Maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni kundi ambalo linaathirika sana kutokana na mabadiliko ya tabianchi, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa ni kutumia vyema maendeleo ya sayansi na teknolojia katika mapambano dhidi ya umaskini; kwa kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani, haki na amani pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwa kudhibiti uchafuzi wa mazingira kutokana na uzalishaji wa hewa ya ukaa. Ni katika muktadha huu, viongozi wa kidini na kisiasa wanapaswa kujizatiti vyema kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, kwani mazingira ni sehemu muhimu sana ya kazi ya uumbaji, kumbe kwa viongozi wote huu ni wajibu wa kimaadili. Hii ni changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 20 Aprili 2023 alipokutana na kuzungumza na viongozi wa kidini na wanasiasa mashuhuri kutoka Manchester, waliomtembelea mjini Vatican.

Utunzaji bora wa mazingira ni wajibu wa wote
Utunzaji bora wa mazingira ni wajibu wa wote

Manchester ni Jiji ambalo linafungamanishwa sana na Mapinduzi ya Viwanda, likabahatika kuwa na maendeleo makubwa ya kiufundi na kiuchumi; mambo yaliyoambatana pia na athari kwa maisha ya binadamu na mazingira yake. Jitihada za kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote hazina budi kuwa ni sehemu pana zaidi ya utunzaji wa ikolojia, utu na heshima ya binadamu wote kwa kutambua kwamba, waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi ni maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi.” Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, kuna uhusiano mkubwa kati ya mazingira na binadamu, kwa sababu binadamu ni sehemu ya maumbile, anahusishwa na kushirikiana nayo. Kumbe, kuna haja ya kutafuta suluhu inayohusiana na mfumo wa maumbile yenyewe na mifumo ya kijamii. Sera na mikakati kuelekea ufumbuzi wa migogoro inadai njia halisi za kupambana na umaskini, kurejesha utu, heshima na haki msingi za watu waliotengwa na jamii sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Rej. Laudato si, 139. Ulaji wa kupindukia na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani ni kati ya changamoto zinazopaswa kuvaliwa njuga katika mwanga wa mafao ya wengi. Viongozi wa kidini na wanasiasa mashuhuri kutoka Manchester, ni kundi linalojipambanua kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema kama sehemu ya utambulisho wake katika mchakato wa kulinda na kutunza mazingira kama sehemu muhimu sana ya kazi ya uumbaji, kiasi cha kuchangia wongofu wa kiikolojia, kama njia ya kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, mshikamano na mafungamano ya kibinadamu, kwa ajili ya ustawi wa jamii mbalimbali kwa sasa na kwa siku za usoni. Baba Mtakatifu anawapongeza kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya; kwa kuwasaidia kuona sera bora za mazingira nyumba ya wote!

Papa Laudato si
21 April 2023, 16:45