Tafuta

Kila mwaka ifikapo tarehe 19 Machi, Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Mtakatifu Yosefu, Mume wa Bikira Maria na Msimamizi wa Kanisa la Kiulimwengu. Kila mwaka ifikapo tarehe 19 Machi, Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Mtakatifu Yosefu, Mume wa Bikira Maria na Msimamizi wa Kanisa la Kiulimwengu.  

Sikukuu ya Mtakatifu Yosefu, Mume wa Bikira Maria na Mlinzi wa Kanisa la Kiulimwengu

Sifa kuu za Mtakatifu Yosefu: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali; mtu aliyebahatika kuwa na kipaji cha ubunifu na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika moyo wa unyenyekevu, Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha ya Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa busara na haki, alijiaminisha mbele ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kila mwaka ifikapo tarehe 19 Machi, Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Mtakatifu Yosefu, Mume wa Bikira Maria na Msimamizi wa Kanisa la Kiulimwengu. Lakini kwa Mwaka 2023 sikukuu hii inaadhimishwa, Jumatatu tarehe 20 Machi 2023. Mtakatifu Yosefu anaitwa mtumishi mwaminifu wa Mungu, kwani uaminifu wake huo, ndio ambao unamshirikisha kwa namna iliyositirika katika historia nzima ya wokovu. Matendo yake ya kiimani hayaonekani kwa wazi sana katika Maandiko Matakatifu lakini yanapaswa kupewa uzito wa pekee, mathalani kwa kuwa mtii katika hali ya ukimya wakati wa kuitikia sauti ya Mungu. “Huyu ndiye wakili mwaminifu na mwenye hekima na busara.” Hii ni siku pia kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, kwani ilikuwa ni tarehe 19 Machi 2013 alipoanza utume wake rasmi kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa kutoa kipaumbele cha kwanza katika ujenzi wa utamaduni wa amani, maskini na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwaalika waamini kumkimbilia na kumwomba Mtakatifu Yosefu, ili awe Mwombezi wa amani ambayo kwa sasa walimwengu wanaihitaji sana. Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu yalizinduliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 8 Desemba 2020 na kufungwa rasmi tarehe 8 Desemba 2021.

Mtakatifu Yosefu Msimamizi wa Kanisa la Kiulimwengu
Mtakatifu Yosefu Msimamizi wa Kanisa la Kiulimwengu

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu akisema kwamba ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Mtakatifu Yosefu ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ubunifu na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika moyo wa unyenyekevu, Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa busara na haki, alijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa na Malaika wa Bwana. Kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Baba Mtakatifu Francisko alianzisha mzunguko wa Katekesi Kuhusu Mtakatifu Yosefu ambaye kimsingi ni msaada, faraja na msimamizi. Baba Mtakatifu amegusia kuhusu: Mtakatifu Yosefu na mazingira alimoishi kadiri ya Maandiko Matakatifu; mjini Bethlehemu mahali alipozaliwa Kristo Yesu kama utimilifu wa Unabii. Nazareth ni mahali alipokulia Yesu. Hii ni miji miwili yenye uhusiano wa karibu sana na maisha ya Mtakatifu Yosefu.

Mtakatifu Yosefu alimlinda B.Maria na Mtoto Yesu
Mtakatifu Yosefu alimlinda B.Maria na Mtoto Yesu

Mwinjili Mathayo anawasaidia waamini kumwelewa Mtakatifu Yosefu, katika hali ya ukimya bila makuu, lakini, kiungo muhimu sana katika historia ya wokovu na moyo wa sala. Kimsingi, Baba Mtakatifu Francisko katika Katekesi kuhusu Mtakatifu Yosefu aligusia mazingira alimoishi Mtakatifu Yosefu; Wajibu na dhamana yake katika historia ukombozi. Amesema kwamba, Mtakatifu Yosefu alikuwa ni mtu wa haki na mchumba wake Bikira Maria. Alikuwa ni mtu mkiya sana, aliyejitahidi kujifunza kwa kusikiliza na hivyo kumwachia Neno wa Mungu nafasi ya kuendelea kukua na kukomaa. Huu ni ukimya uliogeuzwa na kumwilishwa katika matendo. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kristo Yesu alizaliwa katika mazingira duni na maskini na kwamba, unyenyekevu ndiyo njia inayowapeleka waamini kwa Mungu Baba wa mbinguni. Mtakatifu Yosefu alijisadaka sana ili kuokoa maisha ya Mtoto Yesu. Akalazimika kukimbilia nchini Misri na kukaa huko kama mkimbizi, kashfa inayoendelea kujitokeza hata katika ulimwengu mamboleo. Mtakatifu Yosefu alidhulumiwa, lakini alionesha ujasiri mkubwa kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Mtakatifu Yosefu anaonesha kwamba, kitendo cha kuasili watoto ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa kibaba na kimama. Baba Mtakatifu Francisko amemwelezea Mtakatifu Yosefu kuwa ni Baba Mwenye Huruma, shuhuda amini wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu; aliyejitaabiisha katika malezi, makuzi na elimu kwa Mtoto Yesu. Mtakatifu Yosefu alikuwa ni mtu wa ndoto, nyenzo iliyotumiwa na Mwenyezi Mungu kuwasiliana na waja wake. Kwa njia ya ndoto aliweza kutambulishwa kuhusu Fumbo la Umwilisho, akaokoa maisha ya Mtoto Yesu kwa kukimbilia Misri, kielelezo cha ujasiri wa wazazi unaosimikwa katika sala na kumtegemea Mwenyezi Mungu.

Mtakatifu Yosefu ni kielelezo cha wazazi na walezi bora
Mtakatifu Yosefu ni kielelezo cha wazazi na walezi bora

Baba Mtakatifu alichambua kuhusu Mtakatifu Yosefu na Ushirika wa Watakatifu mintarafu Maandiko Matakatifu, Sala na Ibada kwa Mtakatifu Yosefu, ambaye katika historia ya Kanisa amekuwa ni msaada mkubwa kwa watu wa Mungu. Ushirika wa Watakatifu “Sanctorum communio” ni sehemu ya kiri ya imani ya Kanisa kwa kutambua ushirika wa mema ndani ya Kanisa kunakofanyika kwa njia ya Sakramenti za Kanisa pamoja na kuchota katika hazina ya pamoja. Huu ni ushirika wa mambo matakatifu na ushirika kati ya watakatifu. Ni ushirika wa imani, Sakramenti za Kanisa, Karama katika mchakato wa ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Ni ushirika wa upendo unaosimikwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Ibada ya Kanisa kwa watakatifu wa Mungu, au visakramenti na hasa zaidi kwa Bikira Maria, ni kwamba, imani ya Kanisa inawaelekeza waamini kujenga na kudumisha uhusiano mwema na Kristo Yesu unaofumbatwa katika kiungo cha ushirika wa watakatifu. KKK 946-962. Kimsingi Kanisa ni Jumuiya ya watakatifu na wa dhambi wanaojitahidi kutubu na kumwongokea Mungu. Utakatifu ni matokeo ya huruma na upendo wa Mungu uliofunuliwa katika Kristo Yesu, anayetakatifuza kwa kuwapenda waja wake na hivyo kuwakomboa kutoka katika udhaifu wao wa kibinadamu. Kwa njia ya Kristo Yesu, wote wanafanyika kuwa ni sehemu ya viungo vyake. Kumbe, furaha, mateso na mahangaiko ya mwanajumuiya mmmoja ni mahangaiko na mateso ya Kanisa zima.

Ushirika wa Watakatifu ni muungano wa Kanisa lote la Mungu.
Ushirika wa Watakatifu ni muungano wa Kanisa lote la Mungu.

Ushirika wa watakatifu ni kiungo cha nguvu kiasi kwamba, hata kifo hakiwezi kuwatenganisha. Ushirika wa watakatifu ni muungano wa Kanisa la Mbinguni na Duniani. Kanisa lina Ibada ya pekee kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na kwa Mtakatifu Yosefu. Waamini wanakimbilia sana ulinzi na tunza ya Bikira Maria na ya Mtakatifu Yosefu kwa sababu ya dhamana na utume wao kwa Kristo Yesu. Ushirika wa watakatifu unawawezesha waamini kujisikia kwamba, wanao walinzi na waombezi mbinguni, wanaoweza kuzungumza nao mubashara. Watakatifu ni mifano bora ya maisha na tunu msingi za Kikristo, ndiyo maana waamini wanakimbilia, kuomba ulinzi na maombezi yao. Waamini wanapenda kuweka matumaini yao yote kwa Mtakatifu Yosefu, kwa kutambua kwamba, anaweza kila jambo kwa njia ya Kristo Yesu na Bikira Maria, changamoto kubwa kwa Mtakatifu Yosefu. Baba Mtakatifu alitumia fursa hii kusali kwa ajili ya kumwombea mtu mmoja aliyeonekana kuwa na changamoto za kiafya, kisaikolojia na kiimani, ili aweze kupata nafuu katika mateso yake. Sala ya pamoja ni ushuhuda wa ushirika wa watakatifu.

Mtakatifu Yosefu

 

19 March 2023, 16:00