Tafuta

Papa Francisko: Nguzo kuu za Kipindi cha Kwaresima, kama sehemu ya mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Papa Francisko: Nguzo kuu za Kipindi cha Kwaresima, kama sehemu ya mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.   (Vatican Media)

Papa Francisko: Nguzo Kuu za Kipindi Cha Kwaresima: Wongofu na Utakatifu wa Maisha

Kwaresima ni kipindi cha kuimarisha na kuboresha imani, matumaini na mapendo kwa: kufunga na kusali; kwa kufanya toba na malipizi ya dhambi; kwa kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa; Kwa kusoma, kutafakari na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma, kielelezo makini cha imani tendaji. Lengo ni kujitakasa na kuambata utakatifu wa maisha, ili hatimaye, kushiriki furaha ya Kristo Mfufuka wakati wa Sherehe ya Pasaka ya Bwana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kwaresima ni kipindi cha safari ya Siku 40 katika jangwa la maisha ya kiroho na kiutu, kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani tayari kuadhimisha kiini cha Fumbo la Wokovu wa mwanadamu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu yaani Fumbo la Pasaka. Kipindi cha Kwaresima kinasimikwa katika nguzo kuu nne: yaani; Sala, Kufunga, Neno la Mungu na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2023 unanogeshwa na kauli mbiu “Toba ya Kwaresima na Mchakato wa Sinodi.” Ni ujumbe unaochota amana na utajiri wake kutoka katika tukio la Kristo Yesu kugeuka sura mbele ya wanafunzi wake Petro, Yakobo na Yohane nduguye, baada ya kuwa ametangaza Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu, jambo ambalo lilionekana kuwa ni kashfa kwa Mtume Petro, kiasi cha kuambiwa na Kristo Yesu, alikuwa ni Shetani, kikwazo kwake kwani alikuwa hawazi yaliyo ya Mungu bali ya wanadamu. Rej Mt 16:23.

Kwaresima ni kipindi cha toba, wongofu na utakatifu wa maisha
Kwaresima ni kipindi cha toba, wongofu na utakatifu wa maisha

Kipindi hiki cha Kwaresima, anasema Baba Mtakatifu ni mwaliko wa kupanda juu Mlimani Tabor ili kupata mang’amuzi ya maisha ya kiroho na kiutu, ili kuzama zaidi katika Fumbo la maisha ya Kristo Yesu kama utimilifu wa Sheria na Unabii. Ni mwaliko wa kumsikiliza Kristo Yesu kwa umakini mkubwa kama mtindo wa maisha ya Kanisa la Kisinodi. Waamini wapambane na changamoto za maisha na utume wao kwa ari, ujasiri na moyo mkuu, ili kwamba, Fumbo la Msalaba liwasaidie kukuza imani, matumaini na mapendo, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa Kanisa la Kisinodi. Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake kuhusu: “Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya Mwamini: Wito wa Utume. Rej. Mt 9:9-13” aliyoitoa Jumatano tarehe 22 Machi 2023 mjini Vatican.

Kwaresima ni kipindi cha kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari
Kwaresima ni kipindi cha kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari

Kipindi cha Kwaresima iwe ni fursa ya kuamsha na kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwakumbuka na kuwaombea wainjilishaji wote, ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa kile wanacho amini, kufundisha na kuadhimisha. Iwe ni fursa ya kugundua na kutambua kwamba, wao kama waamini ni Mitume wa Yesu, changamoto na mwaliko wa kutafuta na kuambata mapenzi ya Mungu katika maisha. Kwaresima ni kipindi cha kuimarisha na kuboresha imani, matumaini na mapendo kwa: kufunga na kusali; kwa kufanya toba na malipizi ya dhambi; kwa kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa; Kwa kusoma, kutafakari na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo makini cha imani tendaji. Lengo ni kujitakasa na kuambata utakatifu wa maisha, ili hatimaye, kushiriki furaha ya Kristo Mfufuka wakati wa Sherehe ya Pasaka ya Bwana.

Nguzo Kwaresima
22 March 2023, 15:30