Tafuta

Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi katika hija ya kitume: "Ad Limina Apostolorum" 17 Machi 2023 Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi katika hija ya kitume: "Ad Limina Apostolorum" 17 Machi 2023  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Hija ya Kitume ya Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi Mjini Vatican: Umuhimu wa Familia

Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi linasema, hija yake ya Kitume mjini Vatican na hatimaye, tarehe 17 Machi 2023 kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko imekuwa ni ya manufaa sana kwa ajili ya kukoleza kazi ya Kristo Yesu kwa ajili ya Kanisa lake sanjari na huduma kwa roho za waamini “Curam animarum.” Changamoto kubwa kwa wakati huu ni kusimama kidete katika mchakato wa ujenzi wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, utu wema na maadili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Papa Sixtus wa V kunako mwaka 1585 alianzisha hija za kitume zinazotekelezwa na Maaskofu Jimbo mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano, yaani “Ad Limina Apostolorum Visitatio” na kwa kifupi, “Ad Limina.” Kwa busara na hekima yake ya kichungaji akaamuru Maaskofu wote Katoliki kutembelea mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano. Hii ni nafasi ya kutembelea na kusali kwenye Kaburi la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu pamoja na kutoa taarifa ya Maandishi kwa Baraza la Kipapa la Maaskofu kuhusu mwenendo mzima wa maisha na utume wa Kanisa katika Jimbo husika. Ni fursa pia ya kujadiliana na wakuu wa Mabaraza ya Kipapa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo Yesu. Kipindi hiki cha Kwaresima, anasema Baba Mtakatifu ni mwaliko wa kupanda juu Mlimani ili kupata mang’amuzi ya maisha ya kiroho, ili kuzama zaidi katika Fumbo la maisha ya Kristo Yesu kama utimilifu wa Sheria na Unabii. Ni mwaliko wa kumsikiliza Kristo Yesu kwa umakini mkubwa kama mtindo wa maisha ya Kanisa la Kisinodi. Waamini wapambane na changamoto za maisha na utume wao kwa ari, ujasiri na moyo mkuu, ili kwamba, Fumbo la Msalaba liwasaidie kukuza imani, matumaini na mapendo, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa Kanisa la Kisinodi.

Ujenzi wa tunu msingi za kifamilia ni kipaumbele
Ujenzi wa tunu msingi za kifamilia ni kipaumbele

Ni katika hali na mazingira kama haya, Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi linasema, hija yake ya Kitume mjini Vatican na hatimaye, tarehe 17 Machi 2023 kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko imekuwa ni ya manufaa sana kwa ajili ya kukoleza kazi ya Kristo Yesu kwa ajili ya Kanisa lake sanjari na huduma kwa roho za waamini “Curam animarum.” Maaskofu wanasema, wamejadiliana kuhusu maisha ya Sakramenti za Kanisa na changamoto zake nchini Burundi; umuhimu wa uinjilishaji na urithishaji wa imani unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; huduma ya kiroho na kimwili kwa wakimbizi na wahamiaji; malezi na majiundo makini kama sehemu muhimu ya kukabiliana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa pamoja na dhana ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi nchini Burundi. Ni katika muktadha wa ujenzi wa familia ya Mungu Barani Afrika, Askofu Joachim Ntahondereye wa Jimbo Katoliki Muyinga nchini Burundi, katika mahojiano maalum na Radio Vatican anawahimiza watu wa Mungu ndani na nje ya Burundi kujenga na kudumisha misingi ya familia bora. Mababa wa Sinodi ya Kwanza ya Maaskofu Katoliki Barani Afrika iliyoadhimishwa kunako mwaka 1994, walikazia umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia na Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, ikawekwa kuwa ni kielelezo na chemchemi ya kiroho ya kila familia ya Kikristo.

Umoja, upendo na mshikamano ni muhimu sana
Umoja, upendo na mshikamano ni muhimu sana

Walikazia umuhimu wa wajibu na dhamana ya wanandoa na familia; umuhimu wa jukumu la ndoa kama Sakramenti na kwamba, walikuwa wanaitwa na kuhamasishwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia katika ulimwengu mamboleo. Kumbe, waamini walipewa wajibu wa kuokoa na kuendeleza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na hivyo kuwa tayari kushirikiana na familia nyingine. Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika Wosia wake wa Kitume “Africae munus” yaani “Dhamana ya Afrika” alikazia familia kwa kusema kwamba, familia ni hekalu la uhai, ni shule ya: Upendo, haki, amani, msamaha na upatanisho. Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Familia ni mahali pa kuinjilisha na kuinjilishwa.

Ad Limina Burundi

 

18 March 2023, 15:41