Sikukuu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro: Ushirika Katika Imani, Maadili na Utu Wema
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, katika Kanisa hili la Kristo Yesu, Kuhani Mkuu wa Roma, aliye mwandamizi wa Mtakatifu Petro, ambaye Kristo Yesu alimkabidhi kondoo na wanakondoo wake ili awachunge, kwa agizo la kimungu amepokea mamlaka ya juu kabisa, kamili na yanayojitegemea na ya jumla kwa ajili ya huduma ya roho za watu “Curam animalum”. Hivyo basi, kwa kuwa amewekwa kuwa mchungaji wa waamini wote, ili kukuza manufaa ya wote na ya Kanisa zima na pia ya Makanisa mahalia, anashika mamlaka ya juu ya kawaida juu ya Makanisa yote. Kwa upande mwingine na Maaskofu wamewekwa na Roho Mtakatifu kuwa waandamizi wa Mitume kama wachungaji wa watu, na pamoja na Baba Mtakatifu na chini ya Mamlaka yake, wanao utume wa kudumisha kazi ya Kristo Mchungaji wa milele, kwa sababu Kristo Yesu aliwapa Mitume na waandamizi wao agizo na mamlaka ya kuwafundisha mataifa yote, ya kuwatakatifuza watu katika ukweli na kuwachunga. Rej. Christus Dominum, n. 2-3. Mwenyezi Mungu katika huruma na upendo wake wa daima alitaka kuwakusanya watoto wake waliotawanyika ili wawe wamoja. Akamtuma Mwanaye wa Pekee Kristo Yesu, ili awe: Mwalimu, Mfalme na Kuhani wa watu wote. Akamtuma pia Roho Mtakatifu, Bwana na Mleta uzima, asili ya muungano na umoja wa Kanisa katika: fundisho la Mitume, Ushirika, Ekaristi Takatifu na Sala. Katika ushirika wa Kikanisa yapo pia Makanisa maalum (Ecclesiae particulares) yashikayo mapokeo yao wenyewe, bila kuathiri mamlaka kuu ya Kiti cha Petro Mtume kinachosimamia ushirika wote wa mapendo, hulinda tofauti za haki zilizopo na kuendelea kudumisha ushirika wa Kanisa la Kristo. Hivyo, watu wote wanaitwa kwenye ushirika huu wa Kikatoliki wa Taifa la Mungu, ambao huashiria na kuhamasisha amani timilifu, ili wote wanaoitwa kwa neema ya Mungu wapate wokovu. Rej. LG 13.
Ni katika muktadha huu, kila mwaka ifikapo tarehe 22 Februari, Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro, aliyemkiri Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu mwenyewe akamtibitishia Ukulu huu kwa kumwambia “Wewe ndiwe Petro na juu ya Mwamba huu nitalijenga Kanisa langu, wala milango ya kuzimu haitalishinda.” Mt. 16:18. Mtume Petro alikirimiwa neema ya pekee iliyomwezesha kumkiri Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu na hivyo kupewa funguo, kama Askofu wa kwanza wa Roma na baada yake wako waandamizi wake, waliopewa dhamana ya kutangaza na kushuhudia: huruma, upendo na msamaha unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Maadhimisho haya ni kielelezo cha umoja na mshikamano wa Kanisa chini ya uongozi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ambaye kwa sasa ni Baba Mtakatifu Francisko. Maadhimisho haya iwe ni fursa kwa ajili ya kuombea umoja, ushirika na mshikamano wa Kanisa katika masuala, imani, maadili na utu wema! Tumkumbuke na kumwombea kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, ili daima aweze kutekeleza mapenzi ya Mungu na kuendelea kusoma alama za nyakati kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu.
Sikukuu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro inaadhimishwa wakati ambapo Mama Kanisa anakazia kwa namna ya pekee dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Dhana ya Sinodi ni wazo lililotolewa na Mtakatifu Paulo VI, linaloihusisha Familia ya Mungu katika ujumla wake. Mtakatifu Paulo VI, Muasisi wa maadhimisho ya Sinodi mara baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican anasema, Sinodi ni chombo cha kimisionari na uinjilishaji mpya unaolisaidia Kanisa baada ya kutembea pamoja katika sala, tafakari, mang’amuzi na hatimaye, utekelezaji wake unaofanywa na watu wote wa Mungu kadiri ya wito na nafasi zao katika maisha na utume wa Kanisa. Sinodi ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Juhudi za kichungaji na kitaalimungu zisaidie kuimarisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu majadiliano ya kiekumene, kwa kumpokea Roho Mtakatifu ili kuweza kujifunza mengi kutoka kwa wengine na kuvuna kile ambacho Roho Mtakatifu amepanda ndani yao, ambacho kimekusudiwa kuwa ni zawadi kwa wengine.