Tafuta

Jumatano ya Majivu mwanzo wa safari ya Siku 40 katika jangwa la nyoyo zetu ili kwa kuongozwa na sala, tafakari, kufunga na hatimaye matendo ya huruma, ili tupate wongofu wa ndani. Jumatano ya Majivu mwanzo wa safari ya Siku 40 katika jangwa la nyoyo zetu ili kwa kuongozwa na sala, tafakari, kufunga na hatimaye matendo ya huruma, ili tupate wongofu wa ndani.  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Mambo Msingi Katika Kipindi cha Kwaresima

Kipindi cha Kwaresima, iwe ni fursa ya: Kufunga, toba na wongofu wa ndani; nafasi ya kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma kama kielelezo cha imani tendaji. Iwe ni nafasi kwa waamini kushiriki katika Njia ya Msalaba na kuendelea kuboresha mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu kwa njia ya: Sala, Neno na Sakramenti za Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2023 unanogeshwa na kauli mbiu “Toba ya Kwaresima na Mchakato wa Sinodi.” Ni ujumbe unaochota amana na utajiri wake kutoka katika tukio la Kristo Yesu kugeuka sura mbele ya wanafunzi wake Petro, Yakobo na Yohane nduguye, baada ya kuwa ametangaza Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu, jambo ambalo lilionekana kuwa ni kashfa kwa Mtume Petro, kiasi cha kuambiwa na Kristo Yesu, alikuwa ni Shetani, kikwazo kwake kwani alikuwa hawazi yaliyo ya Mungu bali ya wanadamu. Rej Mt 16:23. Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Katekesi yake, Jumatano ya Majivu, tarehe 22 Februri 2023 amewatakia waamini na watu wote wenye mapenzi mema, mwanzo mwema wa Kipindi cha Kwaresima, iwe ni fursa ya: Kufunga, toba na wongofu wa ndani; nafasi ya kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji.

Kwaresima ya Kisinodi, kutembea na kusikilizana
Kwaresima ya Kisinodi, kutembea na kusikilizana

Iwe ni nafasi kwa waamini kushiriki katika Njia ya Msalaba, pamoja na kuendelea kuboresha mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu kwa njia ya: Sala, Neno na Sakramenti za Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa na kwamba, Kanisa linawategemea sana. Vijana wawe na ujasiri pamoja na moyo wa ukarimu kama sehemu ya maadhimisho ya Kipindi cha Kwaresima kinachofikia ukomo wake kwa maadhimisho ya Fumbo la Pasaka. Waamini wamwombe Roho Mtakatifu Mfariji aweze kuwakirimia neema ya kuwa ni mashuhuda na vyombo vya faraja kwa wale wote wanaoteseka: kiroho na kimwili, tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa msingi wa haki, amani na maridhiano katika jamii.

Rais Samia atuma sala na heri kwa Wakristo wakati wa Kwaresima 2023
Rais Samia atuma sala na heri kwa Wakristo wakati wa Kwaresima 2023

Wakati huo huo, Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Wakristo wanapoanza mfungo wa Siku 40 za Kipindi cha Kwaresima kwa Jumatano ya Majivu, 22 Februari 2023, anawaalika Wakristo kuiombea Tanzania na Dunia nzima amani na upendo. Majivu katika paji la uso yawakumbushe ubinadamu wao na kumrudia Mwenyezi Mungu, wakiomba ulinzi wake kwa watu wake wote.

Kipindi cha Kwaresima

 

22 February 2023, 15:00