Tafuta

Ukarimu kama sehemu ya vinasaba na utambulisho wa Wakristo tangu Kanisa la mwanzo Ukarimu kama sehemu ya vinasaba na utambulisho wa Wakristo tangu Kanisa la mwanzo   (Vatican Media)

Injili ya Upendo Katika Huduma Ni Sehemu ya Vinasaba na Utambulisho wa Wakristo

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, amegusia umuhimu wa kumwilisha Injili ya upendo katika huduma, ukarimu kama sehemu ya vinasaba na utambulisho wa Wakristo tangu Kanisa la mwanzo na upendo wa Kanisa kwa maskini na wahitaji zaidi. Kwaresima iwe ni fursa ya toba, wongofu wa ndani, maisha ya sala na matendo ya huruma kiroho na kimwili kwa wahitaji zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 24 Februari 2023 amekutana na kuzungumza na wanachama wa Chama Cha Kitume cha Mtakatifu Petro kwa ajili ya kusaidia utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro: "Pro Petri Sede," kama sehemu ya hija ya maisha ya kiroho inayofanyika kila baada ya miaka miwili. Hii ni fursa ya kupyaisha tena maisha na utume wao na hivyo kuendelea kujichotea huruma na upendo wa Kristo Yesu kwa ajili ya waja wake, tayari kutweka hadi kilindini katika utekelezaji wa shughuli za uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Hija hii ni fursa kwa wanachama kuwasilisha mchango wao kwa ajili utekelezaji wa Injili ya upendo katika huduma sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amegusia umuhimu wa kumwilisha Injili ya upendo katika huduma, ukarimu kama sehemu ya vinasaba na utambulisho wa Wakristo tangu Kanisa la mwanzo na upendo wa Kanisa kwa maskini na wahitaji zaidi. Wanachama hawa ni kielelezo makini cha urithi wa ushuhuda wa upendo ambao uko tayari kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wanaoteseka kutokana na vita, dhuluma, nyanyaso na ubaguzi; maskini wa hali na mali. Kwa namna ya pekee kabisa hija hii ya kiroho inafanyika mwanzoni kabisa mwa Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2023. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2023 unanogeshwa na kauli mbiu “Toba ya Kwaresima na Mchakato wa Sinodi.”

Mashuhuda wa upendo na ukarimu wa Kanisa
Mashuhuda wa upendo na ukarimu wa Kanisa

Ni ujumbe unaochota amana na utajiri wake kutoka katika tukio la Kristo Yesu kugeuka sura mbele ya wanafunzi wake Petro, Yakobo na Yohane nduguye, baada ya kuwa ametangaza Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu, jambo ambalo lilionekana kuwa ni kashfa kwa Mtume Petro, kiasi cha kuambiwa na Kristo Yesu, alikuwa ni Shetani, kikwazo kwake kwani alikuwa hawazi yaliyo ya Mungu bali ya wanadamu. Rej Mt 16:23. Kipindi hiki cha Kwaresima, anasema Baba Mtakatifu ni mwaliko wa kupanda juu Mlimani ili kupata mang’amuzi ya maisha ya kiroho, ili kuzama zaidi katika Fumbo la maisha ya Kristo Yesu kama utimilifu wa Sheria na Unabii. Ni mwaliko wa kumsikiliza Kristo Yesu kwa umakini mkubwa kama mtindo wa maisha ya Kanisa la Kisinodi. Waamini wapambane na changamoto za maisha na utume wao kwa ari, ujasiri na moyo mkuu, ili kwamba, Fumbo la Msalaba liwasaidie kukuza imani, matumaini na mapendo, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa Kanisa la Kisinodi.

Wajenzi wa kanisa la Kisinodi
Wajenzi wa kanisa la Kisinodi

Baba Mtakatifu anakaza kusema, tangu mwanzo wa Kanisa, waamini walitangaza na kushuhudia Injili ya upendo katika huduma kwa kuonesha ukarimu, miongoni mwao na mshikamano wa upendo na wale wote waliokuwa wanawazunguka. “Na jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja; wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu cho chote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na vitu vyote shirika. Na Mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote. Wala hapakuwa na mtu mmoja miongoni mwao mwenye mahitaji; kwa sababu watu wote waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta thamani ya vitu vile vilivyouzwa.” Mdo 4:32-34. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, wao wamewekwa kuwa ni mawakili wa mali za dunia, kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Kumbe, hii ni huduma wanayopaswa kuitekeleza kwa moyo wa ukarimu kama ambavyo Mwenyezi Mungu alivyowakirimia katika maisha yao.

Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi kwa kusikilizana
Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi kwa kusikilizana

Huu ni ni mwaliko wa kuwathamini na kuwapenda watoto wadogo; watu wasiokuwa na ulinzi; wanaotelekezwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu Francisko anatambua fika mchango wao katika maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mwishoni mwa hotuba yake, amewaweka wanachama ndugu na jamaa zao na wote wanaowawezesha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria na Mtakatifu Petro na hatimaye, kuwapatia baraka zake ya Kitume. Itakumbukwa kwamba, Chama Cha Kitume cha Mtakatifu Petro kwa ajili ya kusaidia utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro: "Pro Petri Sede," tarehe 27 Novemba 2021 kiliadhimisha kumbukumbu ya Jubilei ya Miaka 150 tangu kuanzishwa kwake Jimbo kuu la Brussels nchini Ubelgiji na maadhimisho haya kufanyika kwenye Kanisa kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu Koekelberg, Jimbo kuu la Brussels. Hiki ni kielelezo cha huduma ya Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma inayotangwa na kushuhudiwa kama kielelezo cha mshikamano wa udugu wa kibinadamu dhidi ya uchoyo, ubinafsi na tabia ya baadhi ya watu kutaka kujimwambafai.

Huduma ya upendo kwa wahitaji zaidi ni sehemu ya vinasaba vya Kanisa
Huduma ya upendo kwa wahitaji zaidi ni sehemu ya vinasaba vya Kanisa

Na tarehe 24 Februari 2020, Baba Mtakatifu alikutana na kuzungumza na wanachama wa chama hiki na alitumia fursa hiyo kuwashukuru kwa mchango wao mkubwa kwake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, katika kukabiliana na changamoto mamboleo zinazomsibu mwanadamu na mazingira yake. Kuna kilio cha watu wanaoteseka kutokana na vita, kwa kukosa makazi bora, umaskini pamoja na uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote. Kuna haja ya kusimama kidete ili kusitisha kabisa tabia ya unyonyaji wanayofanyiwa maskini na wanyonge ndani ya jamii. Umefika wakati wa kuondokana na vita, kinzani na nyanyaso mbalimbali zinazopelekea makundi makubwa ya watu kuzikimbia nchi na makazi yao. Baba Mtakatifu alikazia umuhimu wa kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote, kwa kujizatiti katika wongofu wa kiikolojia. Maisha ya wanachama wa Chama Cha Kitume cha Mtakatifu Petro kwa ajili ya kusaidia utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ni ushuhuda wa maisha ya Kikristo yanayofumbatwa katika moyo wa ukarimu kwa kwa kuwajali na kuwathamini watu wote. Huu ni mwaliko wa kufyekelea mbali ubinafsi na uchoyo, tabia ya kutowajali na kuguswa na mahangaiko ya jirani; hali inayohatarisha amani kati ya watu wa Mataifa pamoja na mazingira. Baba Mtakatifu anawataka wanachama hawa kujizatiti kikamilifu na kujikita zaidi katika imani ili waweze kuwa kweli ni miale ya moto wa matumaini kwa watu wa nyakati hizi. Kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro Mtume, wanachama hawa wanapaswa kuwa na ujasiri na uthubutu wa kuwashirikisha wengine huruma na upendo wa Kristo Yesu uliofunuliwa kwao. 

Pro Petri Sede
25 February 2023, 14:33