Hija ya Kitume ya Papa Francisko DRC: Papa Akutana na Vijana na Makatekista: Amani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mama Kanisa katika mbinu mkakati wake wa shughuli za kichungaji anataka kuwajengea vijana matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi inayosimikwa katika: haki, amani; ustawi, maendeleo, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hija ya 40 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini DRC kuanzia tarehe 31 Januari 2023 hadi tarehe 3 Februari 2023 inanogeshwa na kauli mbiu “Wote wapatanishwe katika Yesu Kristo.” Baba Mtakatifu Alhamisi tarehe 2 Februari 2023 amekutana na kuzungumza na Makatekista pamoja na umati mkubwa wa vijana wa kizazi kipya kutoka nchini DRC, waliomkaribisha kwa ngoma, vifijo na bashasha kubwa kuonesha kwamba, wao ni jeuri ya Kanisa na DRC katika ujumla wake, licha ya magumu na changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo katika maisha. Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amewakumbusha vijana kwamba, wamepewa zawadi ya uhai kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya DRC, kumbe, wanapaswa kujikita katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki na amani; sala hai, jumuiya inayosimikwa katika ushuhuda wa ushirika, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Vijana na Makatekista wajenge na kudumisha mshikamano na wengine. Wajenge maisha yao katika ukweli na uwazi, washinde ubaya kwa kutenda mema, kama ilivyokuwa kwa kijana Floriberti Bwana Chui aliyeuwawa mjini Goma. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa upatanisho, tayari kuanza upya kwa neema ya Mungu na kwamba, watumie ujana wao kwa ajili ya huduma kwa jirani zao.
Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza Makatekista pamoja na vijana wa kizazi kipya kwa kujitokeza kwa wingi kusherehekea zawadi ya uhai waliokirimiwa na Mwenyezi Mungu, kwa sura na mfano wake, watu wote mbele ya Mungu wako sawa, lakini wanatofautiana na tofauti zao msingi ni amana na utajiri kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mwenyezi Mungu amewakirimia mikono inayoweza kutumika katika ujenzi, mikono hiyo hiyo inaweza kutumika kuchochea vita na kubomoa; kupenda au kuchukia, kumbe, vijana wanapaswa kufanya uamuzi wa hekima na busara, ili mikono yao isaidie mchakato wa ujenzi wa msingi wa haki, amani na maridhiano. Baba Mtakatifu anawataka vijana wawe ni watu wa sala, wajenge na kudumisha utamaduni wa kusoma, kutafakari na hatimaye kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu na Mitume wake. Msalaba wa Kristo Yesu ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma, upendo na msamaha wa kweli, daraja la ufufuko wa wafu. Huu ni mwaliko kwa waamini kujenga na kudumisha ujirani mwema na wale wote wanaoteseka: kiroho na kimwili. Hawa ni wale wanaohisi upweke hasi, wanodhulumiwa na kunyanyasika; wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii bila kuwasahau wale wasiokuwa na ulinzi.
Vijana wajifunze kutafakari mbele ya Msalaba, chemchemi ya nguvu, faraja, upendo na msamaha wa kweli, unaowawezesha waamini kushinda hofu na woga kwa kuwakirimia imani, matumaini na mapendo. Sala, Neno la Mungu na Msalaba, viwasaidie waamini “kumwagilia nyoyo zao kwa neema ya Mungu” tayari kusonga mbele katika hija ya maisha ya kila siku. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa ni wajenzi wa jumuiya inayosimikwa katika furaha na uaminifu kila mtu kadiri ya hali na wito wake na kamwe wasitafute njia ya mkato katika maisha kwa “kujichimbia kwenye imani za kishirikiana, kufakamia: pombe, matumizi haramu ya dawa za kulevya au burudani zinazowaachia utupu na upweke na machungu katika maisha.” Matokeo yake ni chuki, hasira na tabia ya kutaka kulipiza kisasi; kwa kupenda kujimwambafai mbele ya wengine na kutafuta mafanikio ya chapuchapu katika maisha. Vijana wandokane na maamuzi mbele au tabia ya kupenda kuwashambulia wengine na badala yake, wajenge urafiki na ujirani mwema na kuondokana na tabia ya kupenda vita. Wawe ni wasamaria mwema na wajenzi wa urafiki wa mtandao wa kijamii, ili kuambatana na kushikamana katika ukweli na upendo; kwa kushirikisha furaha, kwa kusikilizana na kuheshimiana; kwa kushauriana na kutiana shime katika kutenda mema; kwa kuthamiana na kujaliana katika hali na mali; ili kujenga jamii inayojaliana na kusumbukiana. Wawe ni washiriki na wadau wa historia kubwa ya DRC inayowadai kuwa ni wajenzi wa udugu wa kibinadamu wakiwa na ndoto ya ujenzi wa jamii inayoshikamana zaidi. Wajitahidi kuiga mfano wa Mwenyeheri Isidori Bakanja, Mwenyeheri Marie-Clementine Anuarite na Mtakatifu Kizito, wandani wa safari ya maisha ya kiroho, mashuhuda wa imani na wafiadini waliosimika maisha yao katika nguvu ya upendo na msamaha.
Vijana wajitahidi kujenga maisha yao katika ukweli, uwazi na uaminifu na kamwe wasikubali kutumbukizwa katika rushwa, wizi na ufisadi na zaidi sana wajitahidi katika ujana wao kushinda ubaya kwa kutenda wema. Rej. Rum 12:21. Na kamwe wasikubali kutumiwa na wanasiasa kama vichokoo vya kutekelezea tamaa zao mbaya. Waige mfano wa kijana mwenzao Floribert Bwana Chui aliyepambana na rushwa ya watu waliotaka kuwalisha wananchi wa DRC chakula kilichopitwa na wakati ambacho kingeweza kusababisha madhara makubwa, akauwawa kikatili, lakini akiwa na moyo mweupe dhidi ya rushwa na ufisadi. Vijana wajenge moyo wa kusamehe na kusahau, tayari kuanza upya kwa neema na baraka za Mungu kujikita katika huduma ya ujenzi wa DRC daima wakiwa na ujasiri wa kusonga mbele pasi na woga. Katika safari ya maisha, wajichotee nguvu na ujasiri katika: Neno la Mungu, Maisha ya Sala, Sakramenti za Kanisa na Nguvu ya Msalaba. Kwa upande wake, Askofu Timothée Bodika, PSS. Mwenyekiti wa Tume ya Walei Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, CENCO, katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kuzungumza na vijana pamoja na makatekista, amekazia umuhimu wa vijana kama jeuri ya Kanisa na DRC, ambao ni chachu ya mabadiliko katika jamii kwa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili, licha ya matatizo, changamoto na fursa mbalimbali wanazokabiliana nazo katika maisha. Mwenyeheri Isidori Bakanja ndiye Mlinzi na Mwombezi wa Waamini walei nchini DRC. Huyu ni Katekista aliyetumia muda wake wa ziada kwa ajili ya kuwafundisha vijana wenzake Katekesi, kweli za Kiinjili na amana na utajiri wa imani ya Kanisa Katoliki, hususan Sala ya Rozari Takatifu.
Wakati huo huo, David Bode Nguamba, Mwakilishi wa vijana nchini DRC amemwelezea Baba Mtakatifu matatizo, changamoto na fursa ambazo vijana wanakabiliana nazo nchini DRC, lakini zaidi madhara ya vita ambayo yamedhohofisha kwa kiasi kikubwa sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya jamii; mambo ambayo yamechangia kwa kiasi kikubwa kuyumba na kuporomoka kwa imani. Vijana wengi ni wahanga wa vita, ukabila, matumizi haramu ya dawa za kulevya na ulevi wa kupindukia, bila kusahau matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ambayo inawapotosha wengi kimaadili na kiutu, kwa kutokana na kukosa malezi makini na elimu ya kutosha. Vijana wanapenda kujihusisha na ujenzi wa nchi yao, lakini vita, kinzani na kuzorota kwa uchumi bado ni vikwazo. Wanawataka viongozi wa kisiasa kuweka kando mafao na masilahi binafsi na kuanza kujikita katika mchakato wa haki, amani na upatanisho. Huu ni wakati wa kuwekeza katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia chemchemi na kitalu cha miito mitakatifu sanjari na kusima kidete kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.