Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anasema: Mashuhuda wa ukarimu wa Mungu unaojionesha katika huduma ya upendo. Baba Mtakatifu Francisko anasema: Mashuhuda wa ukarimu wa Mungu unaojionesha katika huduma ya upendo.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Papa Francisko Akutana na Mashuhuda wa Injili ya Huduma ya Upendo Nchini DRC

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amekazia kuhusu umuhimu wa: Mashuhuda wa ukarimu wa Mungu unaojionesha katika huduma ya upendo; vyombo vya mawasiliano ya jamii vinahimizwa kuragibisha matatizo, changamoto na matumaini ya Bara la Afrika; kumbukizi ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Ubalozi wa Vatican nchini DRC; diplomasia ya huduma ya upendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, maendeleo fungamani ni mchakato wa utekelezaji wa sera na mikakati ya maendeleo inayomgusa na kumwambata binadamu mzima, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” wanapaswa kupewa upendeleo wa pekee, ili kuwaonjesha huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Katika muktadha huu, Kanisa linataka kujipambanua kuwa ni mdau mkuu wa maendeleo fungamani ya binadamu, dhana inayokwenda kinyume kabisa na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, ubaguzi mbaya kabisa dhidi ya maskini ni ukosefu wa huduma za maisha ya kiroho. Hii inatokana na ukweli kuwa, maskini mara nyingi ni wepesi sana kukumbatia zawadi ya imani na wanayo kiu ya kutaka kukutana na Mwenyezi Mungu katika safari ya maisha yao. Maskini waonjeshwe urafiki na Neno la Mungu; washirikishwe katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa sanjari na safari ya kukua na kukomaa katika imani. Upendeleo kwa maskini unapaswa kutafsiriwa hasa kama huduma ya kiroho iliyo bora zaidi na inayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee! Baba Mtakatifu anasema, umoja ni kiini na tafsiri ya Kanisa linalopata chimbuko lake kwa kukutana na Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, ambaye kwa njia ya kutangaza na kushuhudia Neno lake, linaweza kuwafikia watu wengi zaidi na hivyo kujenga umoja katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Papa Francisko amewashukuru na kuwapongeza mashuhuda wa Injili ya upendo
Papa Francisko amewashukuru na kuwapongeza mashuhuda wa Injili ya upendo

Umoja kati ya Kristo Yesu na Kanisa lake ni kiini na chachu inayosindikiza na kuenzi huduma ya Injili ya upendo ndani na nje ya Kanisa. Huduma ya upendo inayotolewa na Kanisa inakuwa ni Sakramenti ya umoja wa Kanisa. Hija ya 40 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini DRC kuanzia tarehe 31 Januari 2023 hadi tarehe 3 Februari 2023 inanogeshwa na kauli mbiu “Wote wapatanishwe katika Yesu Kristo.” Baba Mtakatifu baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Ndege wa “Ndolo” Jimbo kuu la Kinshasa, jioni alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na wahanga wa vita na machafuko ya kisiasa kutoka eneo la Mashariki wa DRC, ambako Baba Mtakatifu Francisko alitamani kwenda ili kujionea mwenyewe maafa yaliyoko huko, lakini kutokana na sababu ambazo ziko nje ya uwezo wake, amesikiliza shuhuda za wahanga hawa kwenye Ubalozi wa Vatican nchini DRC. Hawa ni wawakilishi kutoka Bunia, Beni-Butembo, Goma, Masisi, Rutshuru, Bukavu na Uvira, ambayo mara chache sana wanaweza kusikika kwenye vyombo vya mawasiliano Kimataifa. Hawa ni waathirika wa watu wenye nguvu wanaotumia silaha kali kupandikiza utamaduni wa kifo. DRC haitaweza kamwe kupata amani ya kudumu, hadi maeneo ya Mashariki wa DRC yamekuwa na amani. Baadaye jioni, Baba Mtakatifu alikutana na kuzungumza na wawakilishi wa mashirika ya misaada ya Kanisa Katoliki yanayotekeleza dhamana na wajibu wake nchini DRC., mkutano ambao umefanyika kwenye Ubalozi wa Vatican nchini DRC.

Ubalozi wa Vatican unapaswa kuwa ni kitovu cha Injili ya huduma
Ubalozi wa Vatican unapaswa kuwa ni kitovu cha Injili ya huduma

Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia kuhusu: Mashuhuda wa ukarimu wa Mungu unaojionesha katika huduma ya upendo; vyombo vya mawasiliano ya jamii vinahimizwa kuragibisha matatizo, changamoto na matumaini ya Bara la Afrika, kumbukizi ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Ubalozi wa Vatican nchini DRC. Kuna haja ya kuwa na kumbukumbu hai, ili kuirithisha kwa vijana wa kizazi kipya, changamoto na mwaliko wa kusimama kidete kulinda, kudumisha na kuendeleza utu, heshima na haki msingi za binadamu na kwamba, kwa Kanisa madaraka ni kielelezo cha huduma inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Huduma ya upendo, haina budi kuwa na mwelekeo mpana zaidi sanjari na uwezo wa kuwaunganisha watu, kadiri ya karama, vipaumbele na watu wote katika ujumla wao. Baba Mtakatifu ameyashukuru mashirika ya misaada ya Kanisa Katoliki yanayotekeleza dhamana na wajibu wake nchini DRC., kwa kuwahudumia maskini na wahitaji, kama vyombo na mashuhuda wa upendo wa Kristo Yesu na Kanisa lake na hatimaye wameweza kuunda udugu wa kibinadamu, kama njia ya kukumbatia na kuambata upendo wa Kristo kwa waja wake. Baba Mtakatifu anasema, anataka kuwa ni sauti ya wale wasiokuwa na sauti, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa watu wa Mungu nchini DRC na Afrika katika ujumla wake. Kuna haja kwa walimwengu kuwatambua na kuwaheshimu watu wa Mungu Barani Afrika, kuenzi na kuthamini tamaduni; mahangaiko na matumaini yao kwa leo na kesho iliyo bora Zaidi.

Maskini waonjeshwe utajiri wa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa
Maskini waonjeshwe utajiri wa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa

Ni fursa ya kugundua ndani mwao karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu sanjari na tunu msingi za maisha ya Kikristo zinazofumbatwa katika heshima kwa utu wa mwanadamu na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu anasema, Ubalozi wa Vatican ni mahali muafaka pa kuragibisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hapa ni kiini cha Injili ya upendo kwa watu wa Mungu, tayari kuendeleza diplomasia ya huruma inayomwilishwa katika mshikamano wa upendo na huduma kwa watu wa Mungu inayotekelezwa kwa njia ya mtandao wa mshikamano. Ubalozi wa Vatican ulianzishwa rasmi nchini DRC takribani miaka 90 iliyopita kama sehemu ya uwakilishi wa Kitume na mwezi Januari 1977 Vatican ikaanzisha rasmi Ubalozi na hivi karibuni, nchi hizi mbili zinaadhimisha kumbukizi ya Miaka 60 tangu kuanzishwa rasmi kwa Ubalozi wa Vatican nchini DRC. Baba Mtakatifu anayashukuru na kuyapongeza Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Upendo na matumaini kiasi hata cha kuhatarisha usalama wa maisha yao. Lengo kuu likiwa ni kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu hasa miongoni mwa maskini. Maendeleo ya kweli yanazingatia historia ya watu husika inayorithishwa kwa vijana wa kizazi kipya.

Waamini wote wanaitwa na kutumwa kutangaza Injili ya upendo
Waamini wote wanaitwa na kutumwa kutangaza Injili ya upendo

Baba Mtakatifu anawahimiza waamini kushiriki kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na mapendo kwa maskini na wale wanaohitaji zaidi huruma yao, kwani kwa njia hii mara nyingi Mwenyezi Mungu anawashangaza sana waja wake. Ni kwa njia hii pia wanaweza kugundua ufunuo wa Uso wa Kristo Yesu kwa wale wanaowahudumia kwa imani na upendo mkuu. Mwelekeo huu ni kinyume kabisa cha wafanyabiashara wanaotumia rasilimali fedha kwa ajili ya kuwekeza kwenye utengenezaji silaha. Ikumbukwe kwamba, huduma ya upendo kwa maskini, inawanyanyua watu wa Mungu na hivyo kutambua na kuthamini utu, heshima na haki zao msingi kwa moyo wa unyenyekevu! Huduma elimu, afya na ustawi wa jamii, kimsingi zinapaswa kutolewa na Serikali. Waamini wasijiingize katika huduma hizi wakiwa na uchu wa mali na madaraka; wakitaka kufahamika na kujijengea jina na kamwe wasitumie maskini kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao yao binafsi. Baba Mtakatifu anakaza kusema, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma kwa ajili ya kutekeleza mapenzi ya Kristo kwa ndugu zake, kwa kujikita katika upendo na unyenyekevu; uvumilivu na udumifu, ili Familia ya Mungu iweze kukua, kutembea, kujenga na kumshuhudia Kristo Mkombozi wa Ulimwengu. Viongozi wa Kanisa waoneshe dira na njia ya kufuata kwa mfano na ushuhuda wa maisha yao. Ni hatari ikiwa kama viongozi wa Kanisa watageuka kuwa ni mbwa mwitu na kuanza kumezwa na malimwengu kwa kutafuta madaraka, fedha na mali, kinachotakiwa ni ushuhuda unaotekelezwa kwa kuzingatia: ukweli, uwazi, ustawi na maendeleo ya wengi yote haya yakijikita katika tija na weledi, kama mfano bora wa kuigwa!

Watawa wamekuwa mstari wa mbele katika huduma kwa maskini
Watawa wamekuwa mstari wa mbele katika huduma kwa maskini

Baba Mtakatifu anayataka Mashirika ya misaada ya Kanisa Katoliki kuwa na maono ya muda mrefu, yatakayosaidia kurithisha ujuzi na maarifa, nyenzo msingi kwa maendeleo fungamani ya binadamu. Mashirika haya kwa miaka mingi yamekuwa ni chombo cha faraja na matumaini kwa watu wa Mungu; yameendelea kutoa huduma kwa watu wanaoteseka kwa njaa, umaskini, magonjwa na majanga asilia pamoja na kuwajengea watu uwezo wa kutumia teknolojia rafiki kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu ameyataka Mashirika haya kujenga mtandao wa mshikamano na mafungamano katika uhalisia wa maisha, daima wakiimarisha ushirika na Makanisa mahalia katika ngazi mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa. Mtandao wa mshikamano uwe ni fursa ya kushirikishana karama, vipaumbele na mahitaji; kwa kuzingatia pia uekumene wa huduma ya upendo na Makanisa pamoja na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo pamoja na ushirikiano na waamini wa dini mbalimbali, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu amebahatika kusikiliza shuhuda kutoka kwa mashuhuda wa Injili ya huduma ya upendo: Chama cha Kitume cha Wafokolari, wanaojihusisha zaidi katika sekta ya elimu kwa vipofu ili waweze kujikwamua na umaskini pamoja na kushirikishwa zaidi katika jamii licha ya changamoto zao za kila siku.

Mashuhuda wa Injili ya huruma na mapendo ni muhimu sana
Mashuhuda wa Injili ya huruma na mapendo ni muhimu sana

Kuna Mashirika yanayoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Watoto na vijana wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, ili waweze walau kupata mahitaji yao msingi, matibabu na elimu. Mashirika haya yameonesha umuhimu wa uinjilishaji wa kina unaowahusisha kwa namna ya pekee watu wa familia na vijana wa kizazi kipya, ili watoto na vijana wa DRC waweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya hudumana mapendo inayokita mizizi yake katika imani na matumaini. Kuna Jumuiya ya Mtakatifu Egidio inayojihusisha na mapambano dhidi ya Ugonjwa wa UKIMWI, kama sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa “DREAM”, ili kuwasaidia wanawake wajawazito kupunguza maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kutoka kwa Mama mjamzito kwenda kwa mtoto mchanga. Katika orodhsa hii kimo pia Kikundi cha “Telema Ongenge na Mwinda wa Kristu” yaani “Simama, Chukua Msalaba wa Kristo.” Hiki ni kikundi kinachowahudumia walemavu, ili kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za walemavu nchini DRC. Kuna kundi linalowahudumia wagonjwa wa UKOMA, ambao wametelekezwa mitaani. Mwishoni, kuna kundi la watawa wa Shirika la Watrappisti, wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya upendo kwa maskini na wahitaji zaidi.

Mashuhuda wa Upendo
02 February 2023, 15:42