Tafuta

Baba Mtakatifu, Ijumaa tarehe 3 Februari 2023 amehitimisha hija yake kwa kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, CENCO Baba Mtakatifu, Ijumaa tarehe 3 Februari 2023 amehitimisha hija yake kwa kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, CENCO  (Vatican Media)

Hija ya Kitume ya Papa Francisko DRC: Hotuba kwa Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, CENCO

Baba Mtakatifu Francisko ameonesha moyo wa shukrani, Sura ya Kanisa linaloteseka kwa ajili ya watu wa Mungu, Msalaba wa Kristo katika maisha ya watu wa Mungu nchini DRC. Maaskofu wanahimizwa kuwa ni mashuhuda wa ukaribu wa Mungu na Unabii kwa ajili ya watu wa Mungu kwa kuunda dhamiri hai, kwa kukataa uovu na kuwatangazia watu Injili ya matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya 40 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini DRC kuanzia tarehe 31 Januari 2023 hadi tarehe 3 Februari 2023 inanogeshwa na kauli mbiu “Wote wapatanishwe katika Yesu Kristo.” Baba Mtakatifu, Ijumaa tarehe 3 Februari 2023 amehitimisha hija yake kwa kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, “Conférence Episcopale Nationale du Congo” (CENCO). Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu ameonesha moyo wa shukrani, Sura ya Kanisa linaloteseka kwa ajili ya watu wa Mungu, Msalaba wa Kristo katika maisha ya watu wa Mungu nchini DRC. Maaskofu wanahimizwa kuwa ni mashuhuda wa ukaribu wa Mungu na Unabii kwa ajili ya watu wa Mungu kwa kuunda dhamiri hai, kwa kukataa uovu na kuwatangazia watu Injili ya matumaini. Baba Mtakatifu ametoa shukrani kwa viongozi wa Kanisa waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu nchini DRC na kwamba, hawana sababu ya kuogopa, bali wasimame kidete kuwa ni watangazaji na mashuhuda wa furaha ya Injili, Mitume wa haki na Wasamaria wema wa mshikamano, huruma na upatanisho. Shukrani kwa wale wote waliojisadaka kwa ajili ya kufanikisha hija hii ya kitume nchini DRC. Baba Mtakatifu Francisko analishukuru na kulipongeza Baraza la Maaskofu Katoliki DRC kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa ujasiri; kwa faraja, mshikamano na matumaini na watu wa Mungu wanaokabiliana na changamoto mbalimbali katika maisha.

Papa anawashukuru watu wa Mungu DRC kwa ukarimu na upendo wao.
Papa anawashukuru watu wa Mungu DRC kwa ukarimu na upendo wao.

Baba Mtakatifu anashukuru kwa kupata fursa ya kukaa katika mazingira yanayozungukwa na misitu, amana na utajiri mkubwa wa kiikolojia, unaopaswa kulindwa na kuendelezwa dhidi ya tabia ya ubinafsi na uchoyo wa watu wachache ndani ya jamii, pamoja na kulinda imani katika nyoyo za vijana ili isichafuliwe, hivi ndivyo inavyopaswa kuwa pia kwa Kanisa Barani Afrika. Kanisa nchini DRC linajikita katika ari na mwamko wa kimisionari kwa kutangaza upendo wa Mungu na kwamba, Kristo Yesu ni Bwana na Mkombozi wa ulimwengu. Kanisa halina budi kuwa ni mdau wa Injili ya upendo, jumuiya ambayo inaweza kuwashirikisha wengine ari na mwamko wake. Kanisa nchini DRC lina uso wa ujana ambao ni angavu na wa kupendeza, lakini umeharibiwa na mateso, hofu na kukatishwa tamaa. Hili ni Kanisa linaloteseka kwa ajili ya watu wa Mungu katika shida na mahangaiko yao. Kanisa hili ni alama hai ya ya Kristo Yesu ambaye hata leo hii bado anaendelea kukataliwa, na kudhihakiwa, kuteswa na kuhukumiwa afe kama inavyoshuhudiwa sehemu mbalimbali za dunia. Kristo Yesu anaendelea kuteseka katika historia ya watu wa Mungu nchini DRC, anahukumiwa kifo, anadhihakiwa na kuteswa hali inayoonesha mateso ya watu wa Mungu wasiokuwa na hatia, wanaopekenywa na rushwa, ukosefu wa haki na umaskini mkubwa.

Maaskofu wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili
Maaskofu wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili

Licha ya mambo yote haya, viongozi wa Kanisa bado wana matumaini, ingawa amani inaonekana kuzongwa na unyonyaji, uchoyo na ubinafsi; kwa kupindisha ukweli. Viongozi wa Kanisa kwa kufuata mfano wa Nabii Yeremia wanaitwa kuwa ni mashuhuda wa ukaribu wa Mungu, kwa kuendelea kuishi unabii wa matumaini kwani wao kimsingi ni Wachungaji wa watu wa Mungu wanaosimikwa katika nguzo ya sala, huku wakiwa wameungana na Kristo Yesu. Kamwe wasikubali kumezwa na malimwengu, bali waishi na kutenda kadiri ya vigezo vya utumishi vinavyotolewa na Kristo Yesu mchungaji mwema, kwa kujikita katika unyenyekevu unaomwilishwa katika sala ya kila siku. Ukaribu wa Mungu uwawezeshe viongozi wa Kanisa kuwasaidia watu wa Mungu kutambua utu, heshima na haki zao msingi kama watoto wa Mungu. Wakiwa wameimarishwa kwa nguvu ya Mungu wawe ni mashuhuda na vyombo vya faraja na upatanisho, ili kuganga na kuponya madonda ya wale wanaoteseka katika mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo, wawe na uwezo wa kupanda Neno la Mungu linalookoa historia ya watu waliojeruhiwa katika nchi yao wenyewe.

Viongozi wa Kanisa wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili
Viongozi wa Kanisa wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili

Viongozi wa Kanisa wanaitwa kuwa mashuhuda katika muktadha wa vita, ghasia, rushwa na ufisadi, ili mwanga wa Neno la Mungu uweze kuwaangazia wale wanaotembea katika giza na uvuli wa mauti, ili kwa kushirikiana na neema ya Mungu waweze kujenga na kudumisha misingi ya amani, kwa kung’oa sumu ya chuki, uhasama na vita; na kuanza ujenzi wa msingi wa haki, ukweli na amani na kupandikiza mbegu ya maisha mapya, ili DRC ya kesho iweze kuwa na furaha pasi na vita au umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia. Neno la Mungu lisaidie kuasha dhamiri nyofu ili watu waweze kupambana na ubaya na hivyo kuwajengea matumaini. Ukaribu wa Mungu unasimikwa katika ushuhuda wa mapadre wanaoshirikiana na kushikamana, huku wakitembea pamoja kama unavyoonesha mchakato wa maadhimisho ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Wajenge na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiutu na kimaadili, watekeleze shughuli zao katika ukweli na uwazi; wawe ni watu wa msamaha, watumishi wa watu wa Mungu na wala si wafanyabiashara. Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kujenga na kudumisha majadiliano na Mwenyezi Mungu, kwa kupaaza sauti kwa ajili ya kutetea wanyonge kama alivyofanya Askofu mkuu Christophe Munzihirwa Mwene Ngabo, SJ., (1926 – 29 Oktoba 1996) aliyesimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu wakati wa vita ya kwanza nchini DRC. Huu ni wakati wa kusimama imara katika imani, matumaini na mapendo.

Wasimame kidete kutangaza na kushuhidia Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo
Wasimame kidete kutangaza na kushuhidia Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo

Ni muda wa kusimama kidete kutetea Injili ya uhai kwa kuwakumbuka wote waliosadaka maisha yao kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Injili, bila kumsahau Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya. Maaskofu wasiogope kuwa manabii wa matumaini, faraja, mashuhuda wa furaha ya Injili, Mitume wa amani, Wasamaria wa mshikamano, huruma na upatanisho. Daima watambue kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa, amefufuka kwa wafu na ameushinda ulimwengu. Rej. Yn 16:33. Baba Mtakatifu anawashukuru kwa ari na mwamko wao wa kitume na ushuhuda. Mwishoni mwa hotuba yake, amelishukuru Baraza la Maaskofu Katoliki DRC kwa kufanya mara mbili maandalizi ya hija yake ya kitume nchini DRC. Mwezi Juni 2023, Kanisa nchini DRC linaadhimisha Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa huko Lubumbashi, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Kristo Yesu Yu hai katika maumbo ya Mkate na Divai; anawakirimia amani, anawaganga na kuwatibu; anawafariji, kuwaunganisha na kuwaangazia na hatimaye, anawaletea mageuzi katika maisha. Kristo Yesu mpole, mnyenyekevu wa moyo, mshindi wa dhambi na mauti awe daima chemchemi ya furaha na matumaini yao.

Papa Francisko amekuwa ni Msamaria mwema
Papa Francisko amekuwa ni Msamaria mwema

Wakati huo huo Askofu mkuu Marcel Utembi Tapa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, “Conférence Episcopale Nationale du Congo” (CENCO) katika hotuba ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, amemwelezea jinsi ambavyo watu wa Mungu nchini DRC wanavyorutubishwa na wenyeheri kutoka DRC na kuomba neema ya Mungu ili waweze kutangazwa kuwa ni watakatifu. Wanamshukuru Baba Mtakatifu kwa kuridhia Makubaliano ya Mwezi Mei 2016 kati ya Vatican na Serikali ya DRC na kwamba, Baraza la Maaskofu linapania kuona kwamba, makubaliano haya yanatekelezwa. Hija ya Kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II nchini DRC mwezi Agosti 1985, iligusa medani mbalimbali za maisha ya watu wa Mungu nchini DRC na kwa sasa wanakabiliana na mlipuko wa magonjwa ya kuambukiza, majanga asilia, vita na machafuko ya kisiasa yanayowanyima lepe la usingizi na furaha ya maisha. Wanamtambua Baba Mtakatifu Francisko kama Msamaria mwema, wanamshukuru kwa kuendelea kuliweka Kanisa katika huduma ya upendo na mshikamano. Ushirikiano wa Vatican na DRC ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao yao: kiroho, kimwili, kijamii na kitamaduni. Wanayo matatizo, changamoto na fursa mbalimbali lakini wanatambua kwamba, Mwenyezi Mungu hawezi kamwe kuwatelekeza kwani anawapenda katika umoja na tofauti zao na Kanisa linataka kuwa ni chombo na shuhuda wa matumaini nchini DRC. Wanamshukuru Baba Mtakatifu kwa kuwaimarisha katika imani na kuwapatia baraka na kuendelea kuimarisha ushirika na Kanisa zima. Wameiweka DRC, Ukraine na Urusi chini ya ulinzi na tunza ya Moyo Safi wa Bikira Maria.

Maaskofu Cenco

 

03 February 2023, 16:27