Tafuta

Familia ya Kanisa la Mungu Barani Afrika na Madagascar, limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Familia ya Kanisa la Mungu Barani Afrika na Madagascar, limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI.  

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI Alilipenda Kanisa la Afrika na Watu Wake

SECAM katika salam zake za rambirambi kutokana na kifo cha Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI aliyefariki dunia tarehe 31 Desemba 2022 na anatarajiwa kuzikwa tarehe 5 Januari 2023, linasema, Familia ya Kanisa la Mungu Barani Afrika na Madagascar, limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kwani alilipenda Kanisa la Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM katika salam zake za rambirambi kutokana na kifo cha Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI aliyefariki dunia tarehe 31 Desemba 2022 na anatarajiwa kuzikwa tarehe 5 Januari 2023, linasema, Familia ya Kanisa la Mungu Barani Afrika na Madagascar, limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Mtumishi wa Mungu anarejea nyumbani kwa Baba, mwingi wa huruma na mapendo, wakati huu wa Oktava ya Kipindi cha Noeli. Ni kiongozi ambaye alikazia huduma ya upendo katika ukweli, “Caritas in veritate” ni shuhuda mkuu wa mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya kibinadamu mwili na roho. Ni kiongozi aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Kanisa la Kristo Yesu bila ubinafsi. Akasimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani, maridhiano na majadiliano kati ya tamaduni. Katika uongozi wake, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alikuwa na upendeleo wa pekee kwa Kanisa Barani Afrika, akaridhia maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Afrika ili kutoa msukumo mpya unaofumbatwa katika Injili ya upendo. Alitoa wito kwa watu wa Mungu Barani Afrika kujiamini ili kusimama kwa heshima. Aliona ndani yake “pafu la kiroho kwa binadamu ambalo linaonekana kuwa katika mgogoro wa imani na matumaini” (Africae munus, 13).

Papa Mstaafu Benedikto XVI alilipenda Kanisa la Afrika na watu wake
Papa Mstaafu Benedikto XVI alilipenda Kanisa la Afrika na watu wake

Kanisa la Afrika na Madagascar, linaiunua sala zake za dhati kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kumkaribisha mtumishi wake Mwaminifu, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, Mtumishi mwaminifu wa Injili katika Ufalme wake wa amani. SECAM kwa niaba ya familia ya Mungu Barani Afrika na Madagascar inapenda kutoa heshima zake za mwisho kwa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI aliyelibeba Kanisa la Bara la Afrika kwa ari na moyo mkuu; kwa imani na ukarimu. Ujumbe wa SECAM umetiwa mkwaju na Kardinali Fridolin Ambongo, Askofu mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Kinshasa, nchini DRC. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI aliwahi kusema, vishawishi vikuu vinavyowandama wanadamu katika ulimwengu mamboleo ni: Uchu wa fedha na mali; madaraka na elimu! Haya ni mambo ambayo yameendelea kusababisha kinzani na mipasuko mbali mbali katika maisha ya mwanadamu! Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, amekuwa ni kiongozi mwenye busara, hekima na nguvu ya ndani, aliyethubutu kuleta mageuzi makubwa katika maisha na utume wa Kanisa! Lakini kama ilivyo kwa baadhi ya watu, walitaka kumnyong’onyeza kwa sababu zao binafsi! Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alianzisha mchakato wa mageuzi makubwa kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican, lakini alikumbana na “vizingiti vikubwa” katika maisha na utume wake.

Papa Mstaafu Benedikto XVI Mfano wa unyenyekevu
Papa Mstaafu Benedikto XVI Mfano wa unyenyekevu

Ni wakati wa uongozi wa Baba Mtakatifu Benedikto XVI, viongozi kutoka Barani Afrika wakaanza kupata nafasi za uongozi wa juu kama wakuu wa Mabaraza ya Kipapa na wengine, kutumwa sehemu mbali mbali za dunia kama Mabalozi wa Vatican. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alikazia zaidi: Imani, Matumaini na Mapendo mambo msingi ambayo yangewawezesha waamini kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano yao na Kristo Yesu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI ameandika Nyaraka za Kitume zifuatazo: “Deus Caritas Est” yaani “Mungu ni upendo”, “Spe salvi” yaani “Matumaini yanayookoa”; Caritas in veritate yaani “Ukweli katika upendo” na Wosia wa kitume, ambao haukuumaliza kuuandika kama hitimisho la maadhimisho ya Mwaka wa Imani ni “Lumen fidei” yaani “Mwanga wa Imani. Baada ya maadhimisho ya Sinodi mbali mbali, Baba Mtakatifu Mstaafu aliandika Wosia zifuatazo”: Verbum Domini” yaani “Neno la Mungu”; “Ecclesia in Medio Oriente yaani “Kanisa Mashariki ya Kati”; “Sacramentum Caritatis” yaani “Sakramenti ya upendo”; Africae munus” yaani “Dhamana ya Afrika.” Katekisimu ya Kanisa Katoliki: muhtasari wa: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na maisha ya Sala na hatimaye, maadhimisho ya Mwaka wa imani, ilikuwa ni fursa ya kufanya rejea tena katika mafundisho makuu ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Vatican, ili kuendelea kuyapyaisha na kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha na utume wa Kanisa.

Papa Benedikto XVI alilipenda sana Kanisa la Afrika na watu wake
Papa Benedikto XVI alilipenda sana Kanisa la Afrika na watu wake

Familia ya Mungu Barani Afrika inamkumbuka kwa namna ya pekee Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kwa kuridhia maamuzi ya Mtakatifu Yohane Paulo II ya kuadhimisha Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu Katoliki Barani Afrika, iliyofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 4-25 Oktoba 2009. Mtakatifu Yohane Paulo II alikwisha tangaza nia hii hapo tarehe 13 Novemba 2004, lakini akafariki dunia kabla ya kutekeleza ndoto hii ambayo imekuwa na mafao makubwa kwa Kanisa la Mungu Barani Afrika. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI wakati wa hija yake ya kitume Barani Afrika kuanzia tarehe 17-23 Machi 2009 alizindua rasmi hati ya kutendea kazi yaani “Instrumentum Laboris” huko Cameroon na Angola. Tarehe 9 Novemba 2011 Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akawasilisha Wosia wa Kitume “Africae munus” yaani “Dhamana ya Afrika” huko Benin kwa heshima ya Kardinali Bernardin Gantin aliyeishi na kufanya naye kazi kwa miaka mingi mjini Roma. Alionesha ujasiri wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kanisa la Mungu Barani Afrika. Sekretarieti kuu ya Sinodi ya Maaskofu ikasema, Kanisa ni Jumuiya ya waamini wanaopaswa kujipatanisha na Mungu na jirani zao, ili kuendelea kutangaza na kushuhudia Injili ya haki, amani na upatanisho. Bara la Afrika limekuwa likikabiliwa na vita, migogoro na kinzani za aina mbali mbali; unyonyaji sanjari na ukosefu wa haki msingi za binadamu.

Kanisa Barani Afrika: Haki, Amani na Upatanisho
Kanisa Barani Afrika: Haki, Amani na Upatanisho

Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya huruma na mapendo, kumbe, jitihada zote za haki, amani na upatanisho zinapaswa kupata chimbuko na hatima yake kwenye Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kanisa kama familia ya Mungu inayowajibika Barani Afrika haina budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa muhtasari tu, Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI “Africae munus” yaani “Dhamana ya Afrika” unaongozwa na kauli mbiu “Ninyi ni chumvi ya dunia ... Ninyi ni nuru ya ulimwengu” Mt. 513:14. Kanisa Barani Afrika kama chombo cha haki, amani na maridhiano.” Wosia huu umegawanyika katika sehemu kuu mbili: Sehemu ya kwanza: Tazama, nayafanya yote kuwa mapya: Kanisa katika huduma ya upatanisho, haki na amani. Familia ya Mungu Barani Afrika inahimizwa kuwa ni shuhuda katika huduma ya upatanisho, haki na amani kama chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu. Kristo katika moyo wa maisha ya Kiafrika ni chemchemi ya upatanisho, haki na amani. Hii ni changamoto kwa familia ya Mungu kupatanishwa kwanza na Mwenyezi Mungu na hatimaye, kuanza mchakato wa kujipatanisha na jirani zao kwani upatanisho hushinda matatizo, hurudisha heshima ya watu binafsi na hufungua njia ya maendeleo na amani ya kudumu kati ya watu na katika ngazi mbali mbali. Hii ni changamoto ya kujikita katika haki na kuhakikisha kwamba, jamii inajenga na kudumisha mifumo inayosimamia na kutekeleza haki. Mwaliko kwa waamini ni kuishi kadiri ya haki ya Kristo inayofumbatwa katika toba, wongofu wa ndani na upendo wa dhati kabisa! Baba Mtakatifu Mstaafu anasema, upendo katika ukweli ni chemchemi ya amani inayokita mizizi yake katika huduma halisi ya kidugu na kwamba, Kanisa ni chombo cha haki, amani na upatanisho.

Papa Benedikto XVI: Dhamana ya Afrika
Papa Benedikto XVI: Dhamana ya Afrika

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Wosia wake wa Kitume, “Dhamana ya Afrika”, anabainisha mahali pa kufanyia kazi kwa ajili ya upatanisho, haki na amani: toba, wongofu wa ndani, kwa kujali utu na heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni changamoto kwa waamini kukimbilia katika kiti cha huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, ili kukuza na kudumisha umoja na mshikamano katika maisha ya kiroho. Mchakato huu hauna budi kwenda sanjari na utamadunisho wa Injili na uinjilishaji wa tamaduni mbali mbali Barani Afrika, maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu na Neno la Mungu yakipewa msukumo wa pekee katika maisha ya waamini. Haki, amani na upatanisho vipate chimbuko lake ndani ya familia, kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; kwa kuwajali na kuwathamini wazee; kwa wanaume na wanawake kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na nyajibu zao katika familia na jamii kwa ujumla. Kanisa linapaswa kuwajali na kuwathamini vijana wa kizazi kipya, kwa kuwashirikisha katika maisha na utume wa Kanisa.

Papa Benedikto XVI Africae munus- Angola
Papa Benedikto XVI Africae munus- Angola

Ikumbukwe kwamba, watoto ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu, walindwe, waheshimiwe na kuthaminiwa; ukweli na unyenyekevu ni msaada mkubwa kutoka kwa watoto. Familia ya Mungu Barani Afrika, haina budi kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kwa kuheshimu na kutunza mazingira nyumba ya wote. Kanisa Barani Afrika lisaidie juhudi za utawala bora; kwa kuheshimu utawala wa sheria, demokrasia shirikishi; uhuru na haki msingi za binadamu. Hii ni changamoto na mwaliko wa kuonesha mshikamano wa hali na mali kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Utu, heshima na haki zao msingi ni mambo ya kuzingatiwa na wote. Kanisa Barani Afrika linahamasishwa kujenga na kudumisha utandawazi wa upendo na mshikamano. Juhudi hizi zikite mizizi yake katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, ili kujenga umoja na udugu wa familia ya Mungu inayowajibika. Ni katika kutekeleza yote haya, Kanisa Barani Afrika litaweza kuwa kweli ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu. Baba Mtakatifu Mstaafu katika Wosia wake wa Kitume, "Africae munus" yaani “Dhamana ya Afrika”: Sehemu ya Pili anakazia umuhimu wa kushirikishana karama. Maaskofu wanahimizwa kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano na familia ya Mungu, ili kuendelea kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Watu wa Mungu Barani Afrika Wanakukumbuka
Watu wa Mungu Barani Afrika Wanakukumbuka

Maaskofu wawe ni wachungaji wema na watakatifu; waaminifu na wakweli katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Mapadre wahakikishe kwamba, wanaendelea kujipyaisha katika maisha na utume wa Kanisa hasa katika Maandiko Matakatifu na Mafundisho Jamii ya Kanisa ili kukabiliana na changamoto mamboleo. Mapadre wanapaswa kujikana na kubeba vyema Misalaba yao, tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Ni wakati wa kuendelea kuiga mifano bora ya wamisionari na watakatifu kutoka Barani Afrika. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anathamini sana mchango wa watawa na makatekista Barani Afrika pamoja na kuwahimiza waamini walei kujifunga kibwebwe ili kuweza kuyatakatifuza malimwengu, kwa njia ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Kanisa Barani Afrika liendelee kuwekeza katika sekta ya elimu, huduma ya afya na katika teknolojia na ulimwengu wa mawasiliano ya jamii. Kanisa liendelee kuwafundisha waamini umuhimu wa Neno la Mungu na ushiriki makini katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa hususan: Ekaristi Takatifu chanzo na utimilifu wa maisha na utume wa Kanisa. Sakramenti ya Upatanisho ni muhimu katika maondoleo ya dhambi, ili hatimaye, kuishi: kwa upendo, huruma, umoja na udugu wa kibinadamu. Juhudi zote hizi ziende sanjari na uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ni mwanga wa ulimwengu. Huu ni wakati hata kwa watoto wa Mungu Barani Afrika kushiriki kikamilifu kwa ari na mwamko mpya wa shughuli za kimisionari ndani na nje ya Bara la Afrika. Uinjilishaji mpya Barani Afrika unafumbatwa katika huduma ya upatanisho, haki na amani. Mwishoni mwa wosia wake, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anawataka watu wa Mungu Barani Afrika kujipa moyo, kuinuka na kuanza safari ya haki, amani na upatanisho, kwani wao ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu.

BXVI Fadhila za Kimungu
03 January 2023, 15:53