Tafuta

, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 28 Januari 2023 alikutana na kuzungumza na viongozi wa Kanisa wanaojihusisha na utume wa vijana Jimbo kuu la Barcellona, Hispania. , Baba Mtakatifu Francisko tarehe 28 Januari 2023 alikutana na kuzungumza na viongozi wa Kanisa wanaojihusisha na utume wa vijana Jimbo kuu la Barcellona, Hispania.  (Vatican Media)

Papa Francisko: Utume wa Mama Kanisa Kwa Vijana wa Kizazi Kipya: Ushuhuda Amini

Papa Francisko anasema: Lengo ni kutembea kwa pamoja na vijana katika umoja, kwa kusikiliza kabla ya kuzungumza, tayari kuchukua nafasi ambayo si lazima wawe ni walengwa wa matukio kama haya. Kristo Yesu anawaita na kuwaalika, kwanza kabisa kwa kujikita katika umaskini, unyonge na udhaifu wao wa kibinadamu, changamoto ya kujielekeza katika toba na wongofu wa ndani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake elekezi wakati wa kufungua maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana Oktoba 2018 yaliyonogeshwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito” aliwataka Mababa wa Sinodi kuhakikisha kwamba, wanajenga sanaa na utamaduni wa kusikiliza vijana kwa makini na kuzungumza nao kwa ujasiri unaofumbatwa katika ukweli na uwazi. Lengo ni kusaidia mchakato wa wongofu wa kimisionari unaojikita katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kusoma alama za nyakati, tayari kujibu kilio na matamanio halali ya vijana wa kizazi kipya sanjari na kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa vijana wanaoonekana kuvunjika na kupondeka moyo! Mama Kanisa katika mbinu mkakati wake wa shughuli za kichungaji anataka kuwajengea vijana matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi inayosimikwa katika: haki, amani; ustawi, maendeleo, utu na heshima ya binadamu. Katika maadhimisho ya sehemu ya kwanza, Mababa wa Sinodi ya vijana walikazia umoja na mshikamano wa Kanisa, wajibu na umuhimu wa kuwasikiliza, kuwasindikiza na kuwasaidia vijana katika kufanya maamuzi magumu katika maisha yao, kwa kuambatana na Kristo Yesu, chemchemi ya furaha ya Injili na matumaini! Mababa wa Sinodi walisema, kuna haja ya kuwasikiliza kwa makini vijana ili waweze kujitambua; kushirikiana nao kwa karibu kwa kutambua lugha wanazotumia, ili kuweza kuwafikishia Habari Njema ya matumaini.

Viongozi wa Kanisa wajenge utamaduni wa kuwasikiliza vijana
Viongozi wa Kanisa wajenge utamaduni wa kuwasikiliza vijana

Viongozi wa Kanisa wajenge sanaa na utamaduni wa majadiliano na vijana katika ukweli na uwazi, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko! Mababa wa Sinodi walikazia umuhimu wa vijana katika maisha na utume wa Kanisa na kwamba, viongozi wa Kanisa hawana budi kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Yesu ambaye ni njia, ukweli na uzima. Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, ili kuwa karibu na binadamu mdhambi na hatimaye, akampatia nafasi ya kutubu na kumwongokea Mungu. Kanisa halina budi kujikita katika toba, wongofu wa ndani, unyenyekevu, ari na moyo mkuu; mambo msingi yanayopaswa kumwilishwa katika ushuhuda unaoakisi Fumbo la Utakatifu wa maisha na Sakramenti ya maisha hai. Vijana wasikilizwe kwa moyo wa huruma na mapendo. Kanisa linawapokea na kuwasaidia kadiri ya matamanio yao halali, changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga katika hatua mbalimbali za maisha, malezi na makuzi ya vijana: kwenye familia, shule na taasisi za elimu bila kusahau umuhimu wa maisha na utume wa vijana kwenye Parokia. Kuna kundi kubwa la vijana ambalo limejeruhiwa na kwamba, linahitaji kusikia Injili ya matumaini inayomwilishwa katika Katekesi makini na endelevu; katika huduma kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; malezi ya awali na endelevu kwa kuzingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Vijana wafundwe kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo
Vijana wafundwe kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo

Vijana wafundwe kuthamini na kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Wasindikizwe kwa imani, matumaini na mapendo, ili waweze kung’amua wito katika maisha yao na hatimaye, kufanya maamuzi magumu na endelevu! Vijana ni amana na utajiri wa maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Changamoto za maisha ya kifamilia, kiuchumi, kijamii na kitamaduni; mambo yanayoibuka kwa kasi katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia yanapaswa kushughulikiwa kikamilifu kwa kuwajengea vijana uwezo wa kupambana na hali zao, bila kutafuta njia za mkato katika maisha! Madhara ya vita, njaa, magonjwa, rushwa na ufisadi ni kati ya mambo yanayochangia hali ngumu ya maisha ya vijana, kiasi cha kuwakatisha tamaa. Kuna haja ya kuimarisha utandawazi wa mshikamano utakaotoa fursa ya ajira, elimu, ustawi na maendeleo endelevu ya vijana kwa kuondokana na utamaduni usiojali wala kuthamini utu, maisha na haki msingi za binadamu. Vijana wajikite katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kuondokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani, mambo yanayohatarisha umoja, upendo, mshikamano na mafungamano ya kijamii. Taasisi za elimu na vyuo vikuu viwe ni jukwaa la kurithisha imani, maadili na utu wema; kwa kuwafunda vijana kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano; tayari kujisadaka katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kanisa lina dhamana na wajibu wa kuwafunda vijana katika malezi
Kanisa lina dhamana na wajibu wa kuwafunda vijana katika malezi

Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linajitahidi kuwafahamu vijana, kuwapokea, kuwasikiliza na kuwasindikiza katika hatua mbalimbali za safari ya maisha yao, daima Kanisa likikuza na kudumisha “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa” changamoto inayovaliwa njuga kwa sasa na Baba Mtakatifu Francisko. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 28 Januari 2023 alikutana na kuzungumza na viongozi wa Kanisa wanaojihusisha na utume wa vijana Jimbo kuu la Barcellona, nchini Hispania nafasi ya wahudumu wa Injili ya matumaini kumzunguka Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili kujenga na kuimarisha ushirika, tayari kupyaisha tena roho yake ya Kitume inayosimikwa katika mang’amuzi ya mtu binafsi na maisha ya kijumuiya. Lengo ni kutembea kwa pamoja katika umoja, kwa kusikiliza kabla ya kuzungumza, tayari kuchukua nafasi ambayo si lazima wawe ni walengwa wa matukio kama haya. Kristo Yesu anawaita na kuwaalika, kwanza kabisa kwa kujikita katika umaskini, unyonge na udhaifu wao wa kibinadamu, changamoto ya kujielekeza katika toba na wongofu wa ndani. Baba Mtakatifu anawataka wadau katika utume wa vijana, kuwa ni mashuhuda amini kwa vijana kwa kuondokana na maisha unafiki, maisha ya undumila kuwili; kwa kujikuta wakimezwa na malimwengu. Kimsingi wanapaswa kuukumbatia na kuuambata Msalaba wa Kristo Yesu pamoja na tafakari za kina zinazotolewa na Mama Kanisa.

Mama Kanisa anataka kutangaza na kushuhudia Huruma ya Mungu
Mama Kanisa anataka kutangaza na kushuhudia Huruma ya Mungu

Mchakato huu uboreshwe kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, maisha ya sala, toba na wongofu wa ndani. Watambue kwamba, wao wamekuwa ni watu wa kwanza kugusa na kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, changamoto ni kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili zinazowaunganisha na kuwafungamanisha kwa dhati na Mwenyezi Mungu. Wawe ni wajenzi wa udugu wa kibinadamu katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Wajifunze kuwakaribisha na kufanya kazi na watu wote; huku wakijitahidi kutafuta suluhu za matatizo yanayowakumba vijana wa kizazi kipya. Wajitahidi kuwajibika barabara, huku wakiwa huru na makini katika maisha na utume wao.  

Utume wa Kanisa Kwa Vijana

 

30 January 2023, 15:29