Tafuta

Papa Francisko: Utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu Barani Afrika ni mchakato unaofumbata uinjilishaji na utamadunisho. Papa Francisko: Utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu Barani Afrika ni mchakato unaofumbata uinjilishaji na utamadunisho.  (Vatican Media)

Papa Francisko Kanisa Barani Afrika: Uinjilishaji na Utamadunisho: Utu!

Waamini wawe tayari kujisadaka kwa ajili ya uinjilishaji unaopania kuleta upyaisho katika maisha ya watu na kama njia ya kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ni mchakato ulioliwezesha Kanisa kupyaisha maisha na utume wake; ni wakati wa kujizatiti katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mchakato wa Uinjilishaji Barani Afrika unapania pamoja na mambo mengine kumletea mwanadamu ukombozi halisi kutoka katika umaskini, magonjwa na ujinga. Waamini watambue kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, watu ambao wanapaswa kuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya uinjilishaji unaopania kuleta upyaisho katika maisha ya watu na kama njia ya kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ni mchakato ambao umeliwezesha Kanisa kupyaisha maisha na utume wake, changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu nyakati hizi, kujizatiti kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalosimikwa katika: Umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa kwa kukazia utamaduni wa kusikiliza, ushiriki mkamilifu wa watu wateule wa Mungu kwa kumsikiliza kikamilifu Roho Mtakatifu, ili kusoma alama za nyakati. Hija ya Kitume ya Papa Francisko nchini DRC na Sudan ya Kusini ni kuwatia shime watu wa Mungu kuthamini utu, heshima na haki msingi za binadamu. Amana, utajiri na rasilimali za Bara la Afrika zinapaswa kutumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika. Huu ni muhtasari wa masuala mazito yaliyozungumzwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahojiano maalum na “Mundo Negro”: Jarida la Shirika la Wamisionari wa Comboni wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, M.C.C.J linalochapishwa kwa lugha ya Kireno hivi karibuni. Anasema tangu mwanzo alipojiunga na Wayesuit alikuwa na nia ya kutekeleza utume wake wa kimisionari nchini Japan, lengo likuwa ni kutoa kipaumbele cha kwanza kwa watu wa Mungu walioko pembezoni mwa vipaumbele vya jamii katika ujumla wake.

Papa Francisko tangu ujana wake alikuwa ametinia nia ya kwenda Japan kwa utume.
Papa Francisko tangu ujana wake alikuwa ametinia nia ya kwenda Japan kwa utume.

Utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu Barani Afrika ni mchakato unaofumbata uinjilishaji na utamadunisho. Huu ni mchakato unaogusa maisha na mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili na wala Kanisa halina sababu ya kufanya wongofu wa shuruti. Kanisa Katoliki halina utamaduni unaoweza kujitambulisha nao. Waamini watambue kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, watu ambao wanapaswa kuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya uinjilishaji unaopania kuleta upyaisho katika maisha ya watu na kama njia ya kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili na kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mhimili mkuu wa mchakato wa Uinjilishaji. Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya Kitume nchini Canada anasema, aligusia mifumo mbalimbali ya ukoloni, lakini hasa ukoloni wa kiitikadi na madhara yake katika maisha ya watu. Baba Mtakatifu aliwahimiza watu wa Mungu nchini Canada kujenga na kuimarisha tunu msingi za maisha ya kifamilia na jamii katika ujumla wake. Katika hotuba yake, aliwaomba tena msamaha watu wa Mungu nchini Canada kwa makosa na udhaifu ulioneshwa na wamisionari wa Kanisa Katoliki katika mchakato wa uinjilishaji na utamadunisho. Sasa ni wakati wa kujizatiti katika mchakato wa uponyaji na upatanisho wa Kitaifa, na kuendelea kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira, ndugu na historia yao katika ujumla wake. Waendelee kutembea kifua mbele katika mwanga wa maisha unaowawezesha kuwa huru, kwa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya.

Uinjilishaji na Utamadunisho ni chanda na pete katika utume wa Kanisa
Uinjilishaji na Utamadunisho ni chanda na pete katika utume wa Kanisa

Mama Kanisa anataka kujikita katika mchakato wa kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Juhudi zote hizi hazina budi kwenda sanjari na majadiliano ya kidini na kiekumene kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji. Idadi ya waamini wa Kanisa Katoliki si hoja ya msingi, bali ubora: Imani, Matumaini na mapendo, kwa kuendelea kumtumainia Mwenyezi Mungu. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ulipaniwa na Mtakatifu Yohane XXIII na kuhakikisha kwamba, unaadhimishwa, kama tukio la kihistoria katika maisha na utume wa Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Huu ni Mtaguso endelevu ambao bado haujafahamika na wengi; kiasi cha kumwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa, changamoto kwa Mama Kanisa ni kusimama kidete, ili kuhakikisha kwamba, maamuzi ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican yanatekelezwa kikamilifu. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ni mchakato ambao umeliwezesha Kanisa kupyaisha maisha na utume wake, changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu nyakati hizi, kujizatiti kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalosimikwa katika: Umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa kwa kukazia utamaduni wa kusikiliza, ushiriki mkamilifu wa watu wateule wa Mungu kwa kumsikiliza kikamilifu Roho Mtakatifu, ili kusoma alama za nyakati.

Uinjilishaji, Utamadunisho na Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi
Uinjilishaji, Utamadunisho na Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi

Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na mambo mengine umekazia kuhusu: Taifa jipya la Mungu, Watu wa Mungu; Ukuhani wa watu wote; Hisia ya imani na karama katika taifa la Mungu “Sensus fidei.” Wachunguzi wa mambo wanasema, bado kunahitaji muda wa kutosha kuweza kukamilisha na kumwilisha maamuzi makuu ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Hadi sasa kuna mabadiliko makubwa ambayo yamejitokeza na kushuhudiwa na Mama Kanisa ni katika liturujia. Kuna kundi la Waamini wanaopinga mafanikio ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Dhana ya umisionari unaosimikwa katika ushuhuda inaendelea kupyaishwa. Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameambatana na Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani na Mheshimiwa Dr Iain Greenshields Mkuu wa Kanisa la “Presbyterian la Scotland kama kielelezo cha ushuhuda wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika huduma, maisha ya kiroho, damu na sala watatembelea Sudan ya Kusini kuanzia tarehe 3 Februari hadi tarehe 5 Februari 2023. Lengo ni kupaaza sauti zao kulilia amani katika nchi hizi mbili sanjari na kusaidia mchakato wa upatanisho wa Kitaifa katika nchi hizi mbili. Viongozi wa Makanisa haya wanaendelea kushirikiana ili kukamilisha hija hii ya Kitume. Vita ni kati ya changamoto zinazoendelea kugumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi katika nchi hizi mbili.

Hija ya Kitume nchini DRC: Injili ya Upatanisho na Matumaini
Hija ya Kitume nchini DRC: Injili ya Upatanisho na Matumaini

Viongozi hawa wa Makanisa wanataka kushuhudia kwa macho yao wenyewe athari za vita katika ustawi, maendeleo na maisha ya watu, ili kuwasaidia kuondokana na hali kama hii. Utu, heshima na haki msingi za watu wa Mungu zinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Amana, utajiri na rasilimali za Bara la Afrika hazina budi kutumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Afrika. Nchi nyingi za Kiafrika zimepata uhuru wa bendera lakini upande wa uchumi bado ni tegemezi na zinaendelea kunyonywa sana na Nchi zilizoendelea duniani. Bara la Afrika limebahatika kuwa na utajiri mkubwa sana wa watu wenye akili, Bara la Afrika linahifadhi makuu ya Mungu, bila kusahau sanaa na utamaduni wa watu wa Afrika. Uzuri na utajiri wote huu hauonekani kutokana na unyonyaji wa kupindukia, vita, chuki na mipasuko ya kijamii sehemu mbalimbali za Bara la Afrika zinazochochewa na watu wenye uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka kutokana na biashara haramu ya silaha duniani, ambayo imegeuka kuwa ni kiwanda cha kufyatulia vifo. Kama biashara ya silaha duniani ingesitishwa kwa muda wa mwaka mmoja, kungekuwepo na uwezekano mkubwa wa kufyekelea mbali baa la njaa na umaskini unaosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kumekuwepo pia na dhuluma na nyanyaso kubwa kwa wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi.

Utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji zizingatiwe
Utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji zizingatiwe

Kwa bahati mbaya, wakimbizi na wahamiaji hawa wamekuwa wakiwekwa vizuizini, hali inayodhalilisha utu na heshima yao. Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, bado kuna ukosefu mkubwa wa haki jamii Barani Ulaya. Nchi za Ugiriki, Cyprus, Italia, Hispania na Malta ni kati ya nchi ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika kuwapokea wakimbizi na wahamiaji. Serikali ya Italia pamoja na sera zake kuwa ngumu lakini bado imeendelea kujizatiti kuokoa maisha ya wakimbizi na wahamiaji. Kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, EU kuwa na sera zinazojielekeza katika kulinda na kuokoa maisha ya watu.

Papa Mahojiano
17 January 2023, 16:39