Tafuta

Papa Francisko tarehe 25 Januari 2023 ameongoza Masifu ya Jioni kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo nje ya kuta za Roma, kama kielelezo cha kufunga Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo. Papa Francisko tarehe 25 Januari 2023 ameongoza Masifu ya Jioni kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo nje ya kuta za Roma, kama kielelezo cha kufunga Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo.   (Vatican Media)

Kilele cha Maadhimisho Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo: Haki, Amani na Ushuhuda

Papa amewaonya waamini kuachana na vita na wasimame kidete kupinga vitendo vyote vinavyokwenda kinyume cha haki na badala yake, wajielekeze kutenda mema, kama kielelezo cha wongofu wa ndani, ili kuambata neema, tayari kuunda taifa jipya la Mungu, linalowawezesha kushirikiana katika Roho Mtakatifu, ili wakue kwa pamoja katika sala, huduma na katika majadiliano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa anakiri kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye alimtenga tangu tumboni mwa mama yake, akamwita kwa neema yake, Rej. Gal 1:15, akakutana uso kwa uso na Kristo Yesu Mfufuka wakati akiwa njiani kuelekea Dameski, akienda kuwadhulumu Wakristo. Kitabu cha Matendo ya Mitume kinaelezea kwa kina wito wa Sauli, jinsi alivyoitwa na Kristo Yesu, akamwongokea Mungu, toka katika upofu mwili, akabahatika kuuona Mwanga wa kweli, Kristo Yesu Mfufuka, akawa kweli ni chombo kiteule cha Mungu, ili kutangaza na kushuhudia Jina la Mungu kwa watu wa Mataifa. Rej. Mdo 9:15. Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Januari sanjari na kilele cha Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo. Baba Mtakatifu Francisko anasema, mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo unafumbatwa katika: Uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo inayotangazwa, kushuhudiwa na hatimaye, kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu wa Mungu.

Waamini wote wasimame kidete kupinga vita na matumizi ya nguvu
Waamini wote wasimame kidete kupinga vita na matumizi ya nguvu

Juma la 56 la Kuombea Umoja wa Wakristo kuanzia tarehe 18-25 Januari 2023 linaongozwa na kauli mbiu: “Jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki” Isa 1:17. Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 25 Januari 2023 majira ya jioni ameongoza Masifu ya Jioni kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo nje ya kuta za Roma, kama kielelezo cha kufunga Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, amewaonya waamini kuachana na vita na matumizi ya nguvu; wasimame kidete kupinga vitendo vyote vinavyokwenda kinyume cha haki na badala yake, wajielekeze kutenda mema, kama kielelezo cha wongofu wa ndani, ili kuambata neema, tayari kuunda taifa jipya la Mungu, linalowawezesha waamini kushirikiana katika Roho Mtakatifu, ili wakue kwa pamoja katika sala na huduma; katika majadiliano, ili kwa pamoja waendelee kujikita katika majadiliano yatakayowawezesha kufikia umoja kamili, kadiri ya mapenzi ya Kristo Yesu. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia kuhusu umuhimu wa sala katika maisha ya Kikristo, kwa kutubu na kumwongokea Mungu; kwa kujitakasa na kuondokana na uovu, tayari kujifunza kutenda mema; kwa kutaka hukumu na haki.

Waamini wajifunze kutenda mema kwa ajili ya ustawi wa wengi
Waamini wajifunze kutenda mema kwa ajili ya ustawi wa wengi

Huu ni mwaliko kwa Wakristo kujikita katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili wakitambua kwamba Siku ya Mwisho, kila mtu atahukumiwa kadiri ya matendo yake. Vita imekuwa na madhara makubwa katika maisha ya binadamu, kwa wale wote wanaoungama na kujitambulisha kuwa ni Wakristo, wanapaswa kuachana na vita na mambo yote yale yanayopelekea ukosefu wa haki katika jamii. Waamini wajibidiishe kupyaisha tasaufi ya maisha ya kiekumene pamoja na taalimungu yake. Katika muktadha huu, kuna watu ambao wamemezwa na utaifa wenye misimamo mikali kwa kisingizio cha udini, unaopelekea hata wakajikuta wakiwa wametumbia katika kinzani na mipasuko ya kijamii; chuki na uhasama dhidi ya wageni “Xenophobia.”. Wakristo wajitahidi kuiga mfano bora wa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa anayesema “Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami.” 1Kor 15:10. Neema ya Mungu iwasaidie kuepukama na mifumo mbalimbali ya ubaguzi, vita, vurugu na ukosefu wa haki.

Waamini wajifunze kuepuka mifumo ya ubaguzi
Waamini wajifunze kuepuka mifumo ya ubaguzi

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Juma la 56 la Kuombea Umoja wa Wakristo kuanzia tarehe 18-25 Januari 2023 limeongozwa na kauli mbiu: “Jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki” Isa 1:17. Huu ni mwaliko wa kuachana na ubaya na kuanza kujifunza kutenda mema; kwa kutaka hukumu na haki; kwa kuwasaidia wale walioonewa, kutetea wanyonge ndani ya jamii sanjari na kutoa haki. Ni wakati wa kujitaka, kufanya toba na wongofu wa ndani mintarafu maelekeo ya kijumuiya na kikanisa, ili kwa neema na baraka kutoka kwa Kristo Yesu, Wakristo wote wawe na umoja kati yao na jirani zao chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuyashukuru Makanisa pamoja na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo kwa moyo wa upendo na mshikamano unaolisindikiza Kanisa Katokiki katika maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu ambayo kwa sasa imeingia katika maadhimisho katika ngazi ya Mabara. Lengo ni kuwawesha Wakristo kujitambulisha kuwa wao ni wajenzi wa ushirika chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu. Wongofu wa ndani unawawezesha waamini kujenga utamaduni wa kukutana na wengine na kujiaminisha kwa Kristo Yesu, tayari kujenga na kudumisha Ufalme wa Mungu na kuendelea kukoleza matumaini kwa Kristo Yesu.

Waamini wajenge madaraja ya kuwakutanisha watu
Waamini wajenge madaraja ya kuwakutanisha watu

Huu ni mwaliko wa kuendeleza juhudi zinazofanywa na Kanisa kurejesha umoja kamili mintarafu harakati za majadiliano ya kiekumene, ili pole pole kwa kuviondoa vikwazo vinavyozuia ushirika kamili wa Kikanisa, Wakristo wote wakusanyike kwa adhimisho la pamoja la Ekaristi katika umoja wa Kanisa lililo moja na pekee, umoja ambao Kristo Yesu alilijalia Kanisa lake tangu mwanzo. Rej. Unitatis redintegratio, 4. Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wakuu wa Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo walioshiriki katika Ibada ya kufunga Maadhimisho ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo. Kwa upande wake, Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo katika hotuba ya kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuongoza Ibada ya Masifu ya jioni, ili kufunga Maadhimisho ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo amesema, amani ya kweli ni matunda ya haki na kwamba, kwa Wakristo kushirikishana zawadi, amana na utajiri wao ni ushuhuda wa upendo na umoja wa kiekumene.

Umoja wa Wakristo 2023
27 January 2023, 14:50