Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 15 Desemba 2022 amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Mabalozi wa: Belize, Bahamas, Thailand, Norway, Mongolia, Niger, Uganda na Sudan. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 15 Desemba 2022 amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Mabalozi wa: Belize, Bahamas, Thailand, Norway, Mongolia, Niger, Uganda na Sudan.  (Vatican Media)

Hotuba ya Papa Francisko Kwa Mabalozi Wakati wa Kuwasilisha Hati za Utambulisho

Mkazo ni kuhusu: Mchakato wa ujenzi wa: Umoja, mshikamano na ushirikiano kati ya watu wa Mataifa, kwa ajili ya kujenga na kudumisha amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Amana na utajiri wa Jumuiya ya Kimataifa visaidie maboresho ya maisha ya mwanadamu, maskini na kwamba, Vatican inapenda kushirikiana na Mabalozi wapya, ili kufanikisha majukumu yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 15 Desemba 2022 amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Mabalozi wa: Belize, Bahamas, Thailand, Norway, Mongolia, Niger, Uganda na Sudan na kuwahakikishia watu wote wa Mungu wanaowakilishwa na Mabalozi hawa sala zake. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amekazia kuhusu mchakato wa ujenzi wa: Umoja, mshikamano na ushirikiano kati ya watu wa Mataifa, kwa ajili ya kujenga na kudumisha misingi ya amani ya kudumu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Amana na utajiri wa Jumuiya ya Kimataifa visaidie maboresho ya maisha ya mwanadamu, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii wakipewa kipaumbele cha kwanza na kwamba, Vatican inapenda kushirikiana na Mabalozi wapya, ili kuhakikisha kwamba, wanatekeleza vyema nyajibu zao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwamba, mabalozi wapya kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali wanahamasishwa kushirikiana na kushikamana na watu wote ili kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano, kwa kujikita katika haki msingi za binadamu, kwa kukazia haki, upatanisho na majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, amani ya kudumu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kama zawadi safi kwa kizazi cha sasa na kile kijacho.

Papa Francisko Akipokea hati za utambulisho kutoka kwa Mabalozi wapya
Papa Francisko Akipokea hati za utambulisho kutoka kwa Mabalozi wapya

Huu ni wakati wa kusimama kidete kutetea kwa nguvu zote haki za Jumuiya ya Kimataifa, dhidi ya mipasuko, kinzani na Vita Kuu ya Tatu ya Dunia inayopiganwa kwa sasa vipande vipande. Watu wa Mungu wanataka kuona amani ya kudumu inayowajengea hata maskini, matumaini ya leo na Kesho iliyo bora zaidi, kwa watu kujitahidi kuwa ni wajenzi na madaraja ya amani duniani. Ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inatumia amana na utajiri wake wa kihistoria, kiakili, kiteknolojia, kisanaa na kitamaduni, kwa ajili ya maboresho na huduma kwa familia kubwa ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Kwa kuchangia nguvu kazi, kanuni maadili na utu wema; amana na utajiri wa maisha ya kiroho; tunu zote hizi zinaweza kusaidia katika mchakato wa kutafuta suluhu ya changamoto na matatizo yanayomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, haki msingi za binadamu zinadumishwa. Hii ni haki ya kupata maji safi na salama, chakula na lishe bora; huduma bora za afya na elimu.

Ushirikiano na mmshikamano wa Kimataifa umepewa kipaumbele
Ushirikiano na mmshikamano wa Kimataifa umepewa kipaumbele

Ni vyema ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itajielekeza zaidi katika kutafuta suluhu ya ukosefu wa fursa za ajira, ili kuhakikisha kwamba, wagonjwa, walemavu na vijana lakini zaidi wasichana, wanapata fursa za ajira ili waweze kutekeleza ndoto zao katika maisha. Kuna hatari kubwa kwa watu wanaotoka kwenye familia maskini wakajikuta wakishindwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa jumuiya zao. Baba Mtakatifu Francisko anawataka Mabalozi wapya kuendeleza shughuli za kidiplomasia, kuendelea kuwa ni sauti ya watu wasiokuwa na sauti. Katika utekelezaji wa shughuli zao za kidiplomasia wasaidie kuragibisha mshikamano na udugu wa kijamii, hasa miongoni mwa maskini. Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa hotuba yake kwa Mabalozi wapya waliowasilisha hati zao za utambulisho, amewahakikishia kwamba, wataweza kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican, ili waweze kuwajibika barabara, daima wakilenga kwenye ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; ili hatimaye, kujenga na kudumisha urafiki na mahusiano mema, ili hatimaye, ushirikiano na mshikamano huu uweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, yaani ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Hati Mabalozi
15 December 2022, 17:06