Tafuta

maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Andrea, Mtume, Mlinzi, Mwombezi na Msimamizi wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, inayoadhimishwa na Makanisa yote kila mwaka ifikapo tarehe 30 Novemba. maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Andrea, Mtume, Mlinzi, Mwombezi na Msimamizi wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, inayoadhimishwa na Makanisa yote kila mwaka ifikapo tarehe 30 Novemba.  

Sikukuu ya Mtakatifu Andrea: Umoja wa Kanisa Katika Sala na Huduma ya Upendo Kwa Wote

Sababu za kihistoria na kitaalimungu na matendo ya dhambi yamechagia kusambaratika kwa Kanisa na hivyo kuwa ni kizuizi kwa Roho Mtakatifu katika ujenzi wa umoja unaosimikwa katika utofauti. Huu ni wakati wa kujenga umoja wa Kanisa unaosimikwa katika maisha ya sala na udugu ili siku moja, Makanisa haya yaweze kuadhimisha kwa pamoja Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki ambaye pia ni Makamu wa Dekano wa Baraza la Makardinali, anaongoza ujumbe wa Vatican kwenye maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Andrea, Mtume, Mlinzi, Mwombezi na Msimamizi wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, inayoadhimishwa na Makanisa yote kila mwaka ifikapo tarehe 30 Novemba. Ujumbe huu umeshiriki katika mkesha na hatimaye Liturujia Takatifu ambayo imeongozwa na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu George al Fanar. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 30 Novemba 2022 amemkumbuka na kumwombea Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol pamoja na waamini wote katika maadhimisho ya Sikukuu hii, akiwa na matumaini ya kuona umoja kamili sanjari na amani kwa Kanisa sehemu mbalimbali za dunia, lakini kwa namna ya pekee nchini Ukraine. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol, ameonesha nia ya Makanisa haya mawili kutekeleza kwa vitendo utashi wa Kristo Yesu wa kuwa ni wamoja, changamoto inayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee.

Umoja wa Kanisa katika haki na utofauti wake
Umoja wa Kanisa katika haki na utofauti wake

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema katika Kristo Yesu, Kanisa ni kama Sakramenti au ishara na chombo cha kuwaunganisha watu kiundani na Mwenyezi Mungu na hivyo kuleta umoja kati ya wanadamu wote. Kumbe, Kanisa linapaswa kung’aa mng’ao wake Kristo kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu duniani kote. Lumen gentium, 1. Sababu za kihistoria na kitaalimungu; pamoja na matendo ya dhambi yamechagia kusambaratika kwa Kanisa na hivyo kuwa ni kizuizi kwa Roho Mtakatifu katika ujenzi wa umoja unaosimikwa katika utofauti. Huu ni wakati wa kujenga umoja wa Kanisa unaosimikwa katika maisha ya sala na udugu wa upendo ili siku moja, Makanisa haya yaweze kuadhimisha kwa pamoja Fumbo la Ekaristi Takatifu. Hadi wakati huu, Makanisa haya mawili yamepiga hatua kubwa katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu katika ujumla wake hususan: Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; kwa kuendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na mchakato wa ukombozi wa mwanadamu kutoka katika mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Makanisa yameendelea kujielekeza katika mchakato wa waamini kukutana kama ilivyokuwa hivi karibuni nchini Bahrain, kwa kukazia amani dhidi ya vita na mipasuko mbalimbali ya kijamii

Kuna mafanikio yamekwisha kupatikana katika majadiliano ya kiekumene
Kuna mafanikio yamekwisha kupatikana katika majadiliano ya kiekumene

Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Andrea Mtume, kwanza kabisa alikuwa ni Mfuasi wa Yohane Mbatizaji aliyemtambulisha Kristo Yesu akisema “Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu!” Yn 1:29. Mtakatifu Andrea alipomgundua Kristo Yesu kuwa ndiye Masiha akamshirikisha nduguye Simoni Petro na wote wakaamua kumufuasa Kristo Yesu katika maisha yao. Yn 1:41-42 na Yesu akawaambia kwamba tangu sasa watakuwa ni wavuvi wa watu. Mt. 4: 18-19. Andrea ndiye Mtume aliyemtambulisha yule kijana aliyekuwa na mikate mitano ya shayiri na samaki wawili waliomwezesha Kristo Yesu kufanya muujiza wa kuulisha mkutano mkuu. Yn 6:8-9. Hata wale Wayunani waliotaka kumwona Kristo Yesu walipitia kwa Andrea na Filipo, Yn 12: 20-21. Mtakatifu Andrea Mtume anajulikana kama “Protokletos” “Ανδρεας Πρωτοκλητος” yaani Andrea alikuwa ni mwanafunzi wa kwanza kuitwa na Kristo. Baba Mtakatifu Francisko anasema, ushiriki wa Vatican katika maadhimisho haya ni sehemu ya utamaduni wa Makanisa haya mawili, kama kielelezo cha umoja na chachu ya kusonga mbele katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili kuvunjilia mbali uhasama, kinzani na ukimya uliotawala kati ya Makanisa haya mawili kwa miongo kadhaa iliyopita. Roho Mtakatifu chemchemi ya umoja, ndiye aliyewawezesha kuanza tena mchakato wa majadiliano ya kidugu, kielelezo cha ujasiri wa imani uliooneshwa na Mtakatifu Paulo VI pamoja na Patriaki Athenagoras, walioyawezesha Makanisa haya mawili kugundua tena kifungo cha umoja uliokuwepo tangu awali kati ya Wakristo!

Uekumene

 

 

30 November 2022, 15:40