Tafuta

Picha nzuri za ziara ya Papa Francisko huko Bahrain!

Ziara 39 ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko huko Bahrain imefikia tamati.Na katika video fupi inawezekana kufanya uzoefu wa kuona vipindi muhimu sana vya ziara hiyo na mikutano iliyoanza tarehe 3 hadi 6 Novemba 2022.

Na Angella Rwezaula, – Vatican.

Katika ziara ya kitume ya Papa Francisko iliyoanza tarehe 3 Novemba, hatimaye imehitimishwa tarehe 6 Novemba 2022.  Katika Video fupi inawezekana kufurahia picha nzuri za vipindi muhimu sana katika hija hiyo ya kitume nchini Bahrain. Kabla ya kuondoka, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 2 Novemba, yake ya kitume nchini Bahrain kwa Bikira Maria, Afya ya Waroma ili kushiriki maadhimisho ya Kongamano la Bahrain la Majadiliano: Mashariki na Magharibi Kwa Ajili ya Kuishi Pamoja Kwa Binadamu.

Ziara ya Papa Francisko huko Bahrain 3 hadi 6 Novemba
Ziara ya Papa Francisko huko Bahrain 3 hadi 6 Novemba

Baada ya kufika huko na kupokelewa rasmi Baba Mtakatifu alitoa hotuba yake kwa Viongozi wa Kisiasa, Kidiplomasia na Kiraia ambapo alikazia umuhimu wa familia kama inavyofafanuliwa kwenye Katiba ya nchi hiyo Bahrain kuwa kama mti wa maji ya uhai yanayojenga na kuimarisha udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika misingi ya kuheshimiana, maridhiano na uhuru wa kidini. Wahamiaji na wakimbizi wamekuwa na mchango mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu kwenye Ufalme wa Bahrain.

Papa akizungumza na wazee wa Baraza la Kiislam
Papa akizungumza na wazee wa Baraza la Kiislam

Baba Mtakatifu Francisko vile vile alitoa Hotuba yake katika Baraza Kuu la Wazee Wa Dini ya Kiislam ambapo alisema Mwenyezi Mungu ndiye chanzo cha amani; ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana, kuheshimiana na kuthaminiana ili kudumisha uhai wa binadamu dhidi ya utamaduni wa kifo. Kwa njia hiyo aliwaomba wajenge mahusiano na ufungamanishwaji wao katika sala na udugu wa kibinadamu ili kwa pamoja waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali za taifa na Kimataifa hasa katika kuhamasisha zaidi amani ambayo inatishiwa kwa wakati huu.

Mkutano wa Sala huko Bahrain
Mkutano wa Sala huko Bahrain

Baba Mtakatifu Francisko akishiriki katika mkutano wa kiekumene pia aliweza kusisitizia juu ya dhamana ya Roho Mtakatifu katika mchakato wa ujenzi wa umoja wa Kanisa hasa kwa kuzingatia utofauti pamoja na ushuhuda wa maisha kama ilivyojitokeza siku ya Pentekoste. Papa alithibtisha kwamba Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe [Mdo 2: 9-11]. 

Mkutano wa sala ya kiekumene kwa ajili ya  Amani
Mkutano wa sala ya kiekumene kwa ajili ya Amani

Na katika  Misa ya Papa Francisko, aliyoadhimishwa Jumamosi tarehe 5 Novemba 2022 , katika Uwanja wa Taifa wa Bahrain, mahubiri yake yalijikita na mada kuhusu amani na haki na kwamba nguvu ya Yesu ni upendo kwa wote hata maadui. kwa sababu hiyo Yeye anavunja minyororo ya ubaya na kujenga ulimwengu wa udugu. Kwa kukazia zaidi aliomba uhusiano wa jumuiya, jamii na kidugu ukuzwe kila mahali.  Kadhalika alisisitiza juu ya kutolipiza kisasi kwa sababu Yesu anadiriki kupendekeza jambo jingine jipya, ambalo ni tofauti na lisilofikiriwa, na mantiki ya mwanadamu kwamba, msibishane na mtu mbaya bali mtu akikupiga shavu la kulia umwelekezee pia jingine [Mt 5,39].

Misa  katika Uwanja wa Taifa huko Bahrain
Misa katika Uwanja wa Taifa huko Bahrain

Papa Francisko  katika ziara hiyo akikutana na vijana katika shule ya Moyo Mtakatifu huko Awali nchini Bahrain , Jumamosi jioni  tarehe 5 Novemba  2022 kwenye  hotuba yake aliwapatia mialiko mitatu: Kukumbatia utamaduni wa kutunza katika kuendeleza tabia ya ndani kwa mtazamo wa kidugu, kupanda mbegu ya udugu na lazima kuwa mabingwa kwa hilo na sio katika uwanja wa mchezo tu. Na hatimaye mwaliko wa tatu ni changamoto ya chaguzi ya maisha binafasi ambapo aliwaomba watafuta wasindikizaji kwa msaada wa Mungu, walimu, wazazi wao na zaidi babu na bibi, lakini wasitembee peke yao.

Misa  katika Uwanja wa Taifa huko Bahrain
Misa katika Uwanja wa Taifa huko Bahrain

Siku ya mwisho ya Papa Francisko huko Bahrain, Dominika tarehe 6 Novemba 2022 ilifunguliwa kwa mkutano wa sala na Sala ya Malaika wa Bwana kwa Maaskofu, mapadre, watawa na wahudumu wa kichungaji. Papa Francisko kwa maana hiyo amewaachia ushauri wa kuruhusu karama za Roho Mtakatifu zitiririke yaani chemchemi ya furaha, umoja na unabii. Na amewaomba kusali kwa ajili ya amani ya kudumu nchini Ethiopia na nshi za Mashariki ya Kati na zaidi nchini Ukraine wanaoteseka.

Mkutano wa vijana na Papa huko Bahrain
Mkutano wa vijana na Papa huko Bahrain
06 November 2022, 15:20