Pasaka Kwa Wakristo Wote 2025; Jubilei ya Nicea: Kanuni ya Imani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Uinjilishaji unaotekelezwa na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo unajikita katika mchakato wa ushuhuda wa majadiliano ya kiekumene na kidini ili kujenga na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Baba Mtakatifu Francisko anakazia uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala, huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii pamoja na uekumene wa shughuli za kichungaji kwa watu wa Mungu, hususan maisha ya Kisakramenti. Mtaguso Mkuu wa Efeso: Ilikuwa ni tarehe 26 Juni 431 katika maadhimisho ya Mtaguso wa Efeso, Mababa wa Kanisa walipotamka kwamba, yule ambaye Bikira Maria amemchukua mimba kama mtu na ambaye amekuwa ni Mwana wake kadiri ya mwili, ndiye Mwana wa Baba milele, Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kanisa linaungama kwamba, kweli Bikira Maria ni “Mama wa Mungu” “Theotokos, Θεοτόκος”. Hiki ndicho kiini cha Taalimungu na Ibada kwa Bikira kwa sababu mhusika mkuu ni Mwenyezi Mungu. Katika Agano Jipya, Bikira Maria anatambulikana kuwa ni Mama wa Yesu. Tangu mwanzo, Kanisa lilimtambua Bikira Maria kuwa ni Mama wa Mungu lakini kiri hii ya imani ikaendelezwa na kufikia kilele chake kwenye Mtaguso wa Efeso ili kukukabiliana na changamoto zilizoibuliwa na wazushi wa nyakati zile, waliokuwa wanapinga Umungu wa Kristo.
Mtaguso wa Efeso ukaweka mafundisho haya kuwa ni sehemu ya Kanuni ya Imani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kanisa. Kristo Yesu alitungwa mimba tumboni mwa Bikira Maria kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Kumbe, Kristo Yesu ni Mungu kweli na Mtu kweli. Katika karne ya tatu kulizuka mgogoro kuhusu Umungu wa Kristo na Ubinadamu wake. Mtaguso wa Efeso ulifafanua kwa kina na mapana kuhusu imani ya Kanisa na kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Mungu. Waamini wa Efeso wakashangilia sana na huo ukawa ni mwanzo wa kukua na kuendelea kuimarika kwa Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu tangu wakati huo hadi sasa. Katika hali na mazingira kama haya, Wakristo wajitambulishe na wale wanaomtafuta Mungu, katika unyenyekevu, uvumilivu na mshikamano wa kidugu. Wakristo wote wasaidiane katika shida na kama wanahitaji kusimama kidogo wasimame ili kujichotoea nguvu sanjari na kupambanua malengo waliyojiwekea. Kuna matukio makubwa mawili ambayo yako mbele ya Wakristo wote. Mosi, Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo yanajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Nicea ulipoadhimishwa kunako mwaka 325 na kilele cha maadhimisho haya ni mwaka 2025, tukio la pekee na muhimu sana. Mwaka huo Wakristo wote wataadhimisha Pasaka ya Bwana siku moja, matendo makuu ya Mungu kwa waja wake.
Kanuni ya Imani ya Nicea-Constantinopoli ni formula rasmi ambayo ilipitishwa na Mababa wa Mtaguso wa Kwanza wa Nicea (325) ikakamilishwa na Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli (381) ili kubainisha imani sahihi ya Kanisa Katoliki dhidi ya uzushi, hasa wa Ario na wafuasi wake. Katika mazingira hayo, lengo kuu lilikuwa kwanza kabisa ni kumkiri Kristo Yesu “Mungu kweli kwa Mungu kweli” yaani Mungu kweli sawa na Baba, halafu kwamba Roho Mtakatifu anastahili kuabudiwa pamoja na Baba na Mwana (Utatu Mtakatifu). Wakristo wanataka kutembea pamoja na Kristo ambaye ni njia, ukweli na uzima. Watu wanamtafuta Kristo Yesu hata bila ya kutambua. Katika Tamko la Pamoja Kuhusu Ufahamu wa Kristo la Mwaka 1994, Kanisa Katoliki na Kanisa la Ashuru la Mashariki “The Assyrian Church of the East” walitamka kwamba, wanaungama imani moja katika Mwana wa Mungu aliyefanyika mwili, ili wanadamu wapate kuwa watoto wa Mungu kwa neema yake. Huu ni urithi wa pamoja wa imani iliopokelewa, ukadumishwa, kufundishwa, kuthibitishwa na kufafanuliwa na Roho Mtakatifu katika Mapokeo ya Makanisa haya mawili, hususan kwa njia ya urithi wao wa Kisakramenti na Kiliturujia. Sakramenti zikiwa ni Sakramenti za imani, Kanisa Katoliki na Kanisa la Ashuru la Mashariki sasa wanaweza kutamka kwamba wameungana pia katika kuadhimisha imani ileile katika “Mwana aliyefanyika mwili, ili wanadamu wapate kuwa ni watoto wa Mungu kwa neema yake” na katika kutangaza na kushuhudia Fumbo lilelile la wokovu, kupitia Mapokeo yao ya Kisakramenti na Kiliturujia.
Kwa utimilifu na ukamilifu wa ushirika kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Ashuru la Mashariki sio tu kwamba, unatazamia umoja kuhusu maudhui ya imani na adhimisho la Sakramenti, lakini pia kuhusu Katiba ya Kanisa, kama ilivyoandikwa katika Tamko la Pamoja Kuhusu Kristo la Mwaka 1994. Kwa hiyo, Azimio la Pamoja Kuhusu Ufahamu wa Kristo la 1994 na Tamko la Pamoja la sasa juu ya Maisha ya Kisakramenti yanaweka msingi wa awamu ya tatu katika majadiliano ya kitaalimungu yaani, Katiba ya Kanisa. Ikifikisha hatima yake katika muafaka awamu ya tatu itakuwa imekamilisha makubaliano kuhusu: Imani, Maisha ya Kisakramenti na Katiba ya Kanisa, na njia itakuwa wazi kwa Kanisa Katoliki na Kanisa la Ashuru la Mashariki kuadhimisha pamoja Fumbo la Ekaristi Takatifu ambalo ni ishara ya ushirika wa Kikanisa ambao umepyaisha tena. Taalimungu ya Maisha ya Kisakramenti inapembua kuhusu: Daraja Takatifu, Ishara ya Msalaba, Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara, Ekaristi Takatifu na Mikate isiyotiwa chachu; Kutabaruku Altare, Ndoa ya Kikristo pamoja na Maisha ya Kitawa. Maisha ya Kisakramenti yanagusia pia Sakramenti ya Upatanisho, Mpako wa Wagonjwa na Mazishi ya Kikristo.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 19 Novemba 2022 amekutana na kuzungumza na Patriaki Mar Awa wa III wa Kanisa la Ashuru la Mashariki. Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso wa NICEA, Pasaka ya Bwana Kwa Wakristo wote 2025, Mchakato wa majadiliano ya kiekumene katika huduma za kichungaji: Uekumene wa Kichungaji!Katika mazungumzo yao, wamegusia kuhusu: Tamko la Pamoja Kuhusu Ufahamu wa Kristo “Common Christological Declaration” la Mwaka 1985, lililotiwa saini kati ya Mtakatifu Yohane Paulo II na Patriaki Mar Dinkha na hivyo kusitisha malumbano ya Kitaalimungu yaliyokuwa yamedumu kwa takaribani miaka 1, 500 mintarafu Mtaguso wa Efeso wa Mwaka 431. Imekuwa ni fursa kwa Baba Mtakatifu kukumbushiana hija ambayo wameifanya kwa pamoja tangu mwaka 2018, maadhimisho ya Fumbo la Ekarisri Takatifu kwa pamoja kufuatia majadiliano ya kiekumene yaliyofikiwa kunako mwaka 2001, kielelezo makini cha Uekumene wa shughuli za kichungaji miongoni mwa waamini wa Makanisa haya mawili, njia muafaka itakayowawezesha Wakristro kufikia umoja unaoonekana wa Kanisa.
Patriaki Mar Awa wa III wa Kanisa la Ashuru la Mashariki kwa sasa amejielekeza zaidi katika kuandika Waraka kuhusu Taswira ya Kanisa la Ashuru na Mapokeo ya Baba wa Kanisa la Kilatini, waliotumia lugha ya picha inayochota maudhui yake kutoka katika Maandiko Mtakatifu kama vile: Mwezi, vazi lisilo na mshono, karamu, chumba cha bibi arusi, meli, bustani, mzabibu… Lugha hii ni rahisi na ya kawaida, inayofikika kwa wote, iko karibu na ile iliyotumiwa na Kristo Yesu na kwa hiyo ni lugha hai zaidi inayochota maana na utajiri wake kutoka kwa Mafundisho ya Mababa wa Kanisa, mwaliko wa ushuhuda wa maisha na utume wa Kanisa kwa maneno, Fumbo la Maisha ya Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake. Makanisa haya mawili yanasimikwa katika utajiri na urithi mkubwa wa historia ya imani na utume; watakatifu, mashuhuda wa imani na wahungama dini; mateso, dhuluma na nyanyaso za Wakristo Ukanda wa Mashariki ya Kati ambako bado kuna changamoto ya ukosefu wa uhuru a kubudu, kidini na kidhamiri na kwamba, kuna baadhi ya wananchi wanaonekana kuwa ni “watu wa kuja” katika mahangaiko yao. Katika hali na mazingira kama haya, watoto wa Mama Kanisa hawana budi kuwa ni vyombo na mashududa wa umoja na ushirika wa Kanisa.
Baba Mtakatifu Franciko katika hotuba yake, amekazia uhuru wa kidini, uhuru wa kuabudu na raia wote kuheshimiwa na kuthaminiwa katika nchi yao wenyewe pasi na ubaguzi. Changamoto kubwa kwa sasa ni kuona na kushuhudia waamini wa Makanisa haya mawili wakiadhimisha kwa pamoja Fumbo la Ekaristi Takatifu kielelezo cha umoja kamili na unaoonekana wa Kanisa la Kristo unaosimikwa katika udugu wa kibinadamu katika ukweli na upendo. Patriaki Mar Awa wa III wa Kanisa la Ashuru la Mashariki amepangiwa pia kutoa mada kuhusu “Mang’amuzi ya Safari za Kisinodi kwa Makanisa Kiorthodox na Makanisa ya Mashariki katika ujumla wake katika Kongamano lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Kipapa cha Angelicum. Kanisa Katoliki katika miaka ya hivi karibuni limeendelea kujikita katika Hija ya Kisinodi inayosimikwa katika utamaduni wa watu kukutana, kufahamiana na kushirikishana matumaini na mahangaiko yao; kusali pamoja na kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo yanajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Nicea ulipoadhimishwa mwaka 325 na kilele cha maadhimisho haya ni mwaka 2025, tukio la pekee na muhimu sana.
Mwaka huo wa 2025 Wakristo wote wataadhimisha Pasaka ya Bwana siku moja, matendo makuu ya Mungu kwa waja wake, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kanisa Katoliki kama alivyowahi kusema Mtakatifu Paulo VI liko tayari, kuadhimisha Pasaka ya Bwana, ikiwa kama Makanisa na Madhehebu ya Kikristo yataamua tarehe ya pamoja ili kujenga na kuimarisha umoja na ushirika wa Kanisa. Baba Mtakatifu amemzawadia Patriaki Mar Awa wa III wa Kanisa la Ashuru la Mashariki masalia ya Mtakatifu Thoma aliyekiri Umungu wa Kristo Yesu baada ya kugusa Madonda yake Matakatifu, chemchemi ya upendo na huruma ya Mungu Rej. Yn 20:28.