Tafuta

Mwaliko wa Baba Mtakatifu kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema ni kumfungulia Kristo Yesu malango ya nyoyo zao ili aweze kuingia na kuwakirimia mwanga wake angavu. Mwaliko wa Baba Mtakatifu kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema ni kumfungulia Kristo Yesu malango ya nyoyo zao ili aweze kuingia na kuwakirimia mwanga wake angavu.  (Vatican Media)

Kipindi cha Majilio: Mfungulieni Kristo Yesu Malango ya Nyoyo Zenu Apate Kuingia!

Kipindi cha Majilio ni maandalizi ya maadhimisho ya Sherehe ya Noeli, kuzaliwa kwa Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu. Mwaliko wa Baba Mtakatifu kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema ni kumfungulia Kristo Yesu malango ya nyoyo zao ili aweze kuingia na kuwakirimia mwanga wake angavu na uwepo wake unaoganga na kuponya udhaifu na mapungufu ya kibinadamu.

Na Padre Benjamin Mwinuka, C.PP.S., - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 23 Novemba 2022 amewakumbusha waamini kwamba, Dominika tarehe 27 Novemba 2022 Mama Kanisa anaanza Kipindi cha Majilio, kama Maandalizi ya maadhimisho ya Sherehe ya Noeli yaani kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu. Mwaliko wa Baba Mtakatifu kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema ni kumfungulia Kristo Yesu malango ya nyoyo zao ili aweze kuingia na kuwakirimia mwanga wake angavu na uwepo wake unaoganga na kuponya udhaifu na mapungufu ya kibinadamu. Mama Kanisa huchukulia wajibu wake kuadhimisha kwa kumbukumbu takatifu ya ukombozi ya Bwanaarusi wake aliye Mungu katika siku zilizopangwa katika mwenendo wa mwaka mzima, anapolikunjua Fumbo la Kristo Yesu, tangu Fumbo la Umwilisho na Pasaka hadi kungojea kwa tumaini lenye heri kurudi kwake Bwana Yesu, kuwahukumu wazima na wafu. Na kwa njia hii, Mama Kanisa huwafungulia waamini utajiri wa uweza na mastahili ya Bwana wake na hivyo waamini huweza kuchota na kujazwa na neema ya wokovu. Mama Kanisa katika huruma na upendo wake wa daima anapenda kuwakomaza waamini kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili; Mafundisho, Sala pamoja na matendo ya toba na huruma. Rej. Sacrosanctum concilium, 102-111.

Majilio kiwasaidie waamini kumngoja kwa Kristo Yesu kwa matendo mema
Majilio kiwasaidie waamini kumngoja kwa Kristo Yesu kwa matendo mema

Kipindi cha Majilio: “Kwa kuadhimisha kila mwaka liturujia ya majilio, Kanisa linahuisha kule kumngojea Masiha, likijiweka katika ushirika wa maandalizi marefu ya ujio wa kwanza wa mwokozi, waamini wakiamsha upya tamaa ya ujio wake wa pili.” (KKK 524). Majilio ni kipindi cha upendo, matumaini, furaha na amani inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Leo ni Dominika ya kwanza ya Kipindi cha Majilio Mwaka “A” wa Kanisa. Kwa kawaida Dominika ya kwanza ya Majilio hutamatisha kipindi cha mwaka wa Kanisa na kuanza mwaka mwingine mpya wa Kanisa. Mwaka mpya wa kiliturujia unaanza ambapo Kanisa litatuongoza katika kuadhimisha fumbo zima la Kristo, Mwana wa Mungu, Mungu pamoja na Baba, aliyekuja kati ya wanadamu ili kuwaokomboa Mwaka mpya wa kiliturujia ni fursa ya kuzungumza na kuishi na Kristo, kupyaisha maisha yetu ya kiroho, kumtumaini na kumpenda Kristo na Mungu Baba yetu aliye mbinguni, upendo unaoelekezwa pia kwa jirani zetu, hasa maskini na wahitaji zaidi. Ni kipindi kinacho tupatia fursa ya kutafakari mafumbo ya Wokovu wetu na kuonja upya uwepo wa milele wa Bwana wetu Yesu Kristo katika maisha yetu ya kila siku. Hiki ni kipindi cha kumwadhimisha Kristo Yesu, Emanueli, aliyetumwa na Baba na kuwepo kati yetu na akakubali kuingia katika historia yetu na kutembea na sisi ili aiponye historia hiyo iliyo jeruhiwa na dhambi.

Majilio ni kipindi cha maandalizi katika imani, matumaini na mapendo
Majilio ni kipindi cha maandalizi katika imani, matumaini na mapendo

Hebu tutafakari kwa ufupi maana ya kipindi hiki cha majilio tukianza na neno lenyewe Majilio. Majilio ni neno linatokana na neno la Kilatini “adventus” lenye maana ya “kuja” au “kuwasili.  Katika lugha ya Ulimwengu wa Kale lilikuwa neno la kitaalamu lililotumika kuonesha kuwasili kwa ofisa au ziara ya mfalme katika jimbo. Lakini pia lilitumika kuonesha ujio wa “uungu”, ambao hutoka kwenye maficho yake ili kudhihirisha nguvu au kuwapo katika ibada. Wakristo walichukua neno “ujio” na kulitamadunisha ili kueleza uhusiano wao na Yesu Kristo: Yesu ndiye Mfalme, ambaye aliingia katika “jimbo” maskini linaloitwa dunia, ili kumtembelea kila mtu, anawaalika wamwaminio kushiriki katika Sherehe ya ujio wake, wale wanaoamini uwepo wake katika kusanyiko la maadhimisho ya kiliturujia. Lakini pia neno “Adventus” lilimaanisha: “Mungu yupo hapa”, hajajitenga wala kujificha na ulimwengu, hajatuacha peke yetu. Hata kama hatuwezi kumwona na kumgusa, yupo nasi daima, anakuja kututembelea kwa njia mbalimbali, lakini kwa namna ya pekee katika: Sala, Maandiko Matakatifu, Sakramenti za Kanisa, kwa njia ya jirani, na zaidi katika historia ya kila mwamini.

Waamini wamsubiri Kristo Yesu anayekuja kwa imani na matumaini.
Waamini wamsubiri Kristo Yesu anayekuja kwa imani na matumaini.

Maana zaidi ya neno “ujio” inajumuisha ile ya “Visitatio”, ambayo kwa urahisi na kwa usahihi inamaanisha “kutembelea” maana yake ni kutembelewa na Mwenyezi Mungu.  Mungu anaingia maishani mwangu na anataka kutembea na mimi kama vile ujumbe wetu wa sinodi, unavyoyuhamasisha katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi kwa kututaka tutembee pamoja, tushirikishane katika safari yetu ya maisha ya kiroho na maisha ya kawaida tukiteta na kutafuta suluhisho la changamoto zinazo tukumba.   Majilio ni kipindi cha kungoja na wakati huo huo ni kipindi cha “Matumani.” Majilio hutuhimiza kuelewa maana ya wakati na historia kama tukio linalofaa kwa wokovu wetu. Yesu alionesha ukweli huu wa ajabu katika mifano mingi: katika mifano ya watumishi walioalikwa kukesha na kungojea kurudi kwa bwana wao (Mt 24:46-51; katika mfano wa wanawali wanao mngoja bwana arusi (Mt 25:1-13). Kadiri ya kalenda ya kanisa katoliki, Kipindi cha majilio kimegwanyika katika sehemu kuu mbili, kipindi cha kwanza huanza dominika ya kwanza ya majilio mpaka tarehe 16 Desemba. Katika kipindi hiki tunatafakari ujio wa pili wa Bwana wetu Yesu Kristu: “toka huko atakuja kuwa hukumu wazima na wafu.” KKK 668). Ni kipindi ambacho tunakumbushwa kuwa Kristo Mtukufu, ajapo mwishoni mwa nyakati, kuwahukumu wazima na wafu, atafunua hali ya siri ya mioyo, na atamlipa kila mtu kadili ya matendo yake na kadiri ya kupokea kwake, au kukataa kwake neema.

Kipindi cha pili huanza tarehe 17 Desemba hadi tarehe 24 Decemba, ambapo katika kipindi hiki tunatafakari juu ya ujio wa kwanza wa Bwana wetu Yesu Kristo, tunatafakari juu ya fumbo kuu la Umwilisho, mwanzo wa utimilifu wa nyakati yaani utimilifu wa ahadi na matayarisho kama Mtume Paulo anavyo tuambia: “Lakini wakati ulipo wadia, Mungu alimtuma mwanae mwana wake aliye zaliwa na mwanamke, aliye zaliwa chini ya sheria (Gal 4:4).” Tunamtafakri Mungu anaye amua kuja kukaa kati yetu; “Tazama Bikira atachukua Mimba na kuzaa mwana, naye watamwita Emanueli, maana yake Mungu pamoja nasi. (Mt 1:23).” Katika kipindi hiki cha Majilio kuna alama muhimu za kiliturujia ambazo hutumika zikiwa zimebeba ujumbe mahususi wa kipindi hiki cha majilio ambazo ni taji la mduara lenye kijani kibichi, mishumaa minne na rangi ya mavazi na vitambaa ikiwa ni ya zambarau. Na hizi ndizo maana halisi za alama hizo: Taji la kijani kibichi lenye umbo la mduarua, lisilo kuwa na mwanzo wala mwisho, kwa kadili ya mapokeo ya kale ya kanisa humanisha umilele wa Mungu, ndio kusema Mungu hana mwanzo wala mwisho (Alpha na Omega) vile vile humaanisha mwendelezo wa uhai. Lakini pia rangi ya kijani kibichi katika taji hilo hutukumbusha kuwa “Mungu ndiye asili ya mema yote” na vilevile hukazia juu ya uwepo wa matumaini, matumaini ambayo manabii walitabiri na kuwatangazia watu bayana: “Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda (Isaya 11:1).”

Majilio Sehemu ya Pili ni Ujio wa Kristo Yesu Katika Fumbo la Umwilisho
Majilio Sehemu ya Pili ni Ujio wa Kristo Yesu Katika Fumbo la Umwilisho

Mishumaa minne inawakilisha Majuma manne ya Kipindi cha Majilio. Kwa kadiri ya Mapokeo ni kwamba kila juma linawakilisha miaka elfu moja, kumbe majuma manne ni sawa na miaka 4,000 kutoka kwa wazazi wetu wa kwanza Adamu na Eva hadi Kuzaliwa kwa Mwokozi. Mishumaa mitatu ni ya rangi ya zambarau na moja ni wa rangi ya waridi. Mishumaa ya zambarau hutukumbusha kuwa kipindi cha majilio ni kipindi cha sala, toba, na matendo ya huruma: kiroho na kimwili ili kujitayarisha vema kumpokea Mkombozi wetu katika hali zote mbili, ujio wa kwanza na wa pili. Mshumaa wa rangi ya waridi huwashwa Dominika ya tatu, Dominika ya furaha “Gaudete” kwa sababu waamini wamefika katikati ya Kipindi cha Majilio, utimilifu wa ahadi ya kuzaliwa mwokozi ukaribu zaidi. Mwanga wa mishumaa unaashiria matarajio na tumaini linalozunguka ujio wa kwanza wa Bwana wetu ulimwenguni na matarajio ya ujio wake wa pili kuwahukumu wazima na wafu. Masomo yetu ya Dominika ya kwanza ya majilio mwaka A, yanaendelea kusisitiza juu ya ujio wa pili wa Bwana wetu Yesu Kristu, kama ilivyo kawaida kwa kipindi cha kwanza cha majilio. Tunaalikwa tuwe macho na kuyaishi maisha ya sasa kwa mioyo iliyo jengwa kwenye ufalme wa mbinguni na kuelekezwa kwenye ujio wa pili wa Bwana Yesu Kristo Mtukufu. Somo la Kwanza Isa 2:1-5: “Atahukumu kati ya mataifa, na kuwawekea maagano mataifa mengi. Zab122: “Twendeni nyumbani kwa Bwana tukishangilia.” 

Ni wakati wa kumsubiri Kristo Yesu Jua la Haki achomoze katika nyoyo za watu.
Ni wakati wa kumsubiri Kristo Yesu Jua la Haki achomoze katika nyoyo za watu.

Somo la pili, Rum 13:11-14: “Kwa maana wokovu wetu u karibu sasa kuliko tulipoanza kuamini; usiku umeenda, mchana umekaribia.” Na Injili ni Mathayo 24:37-44: “Lakini siku yake na saa yake hakuna aijuaye, wala malaika wa mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake. Kwa ujio wa mwana wa mtu itakuwa kama siku za Nuhu. Kipindi hiki cha majilio tulicho kianza, kinatualiaka kuwa watulivu na wakimya ili kutafakari kwa kina, kuelewa na kuonja uwepo wa Mungu maishani mwetu. Ni mwito wa kuyatafakari maisha yetu yote na kuelewa kwamba matukio tunayo kutana nayo, changamoto, furaha au huzuni ni namna ambayo Mungu anatukumbusha uwepo wake na ukuu wake. Uhakika wa uwepo wake unapaswa kutusaidia kuona ulimwengu kwa macho tofauti yaani kwa macho ya: Imani, matumaini na mapendo. Kipindi cha majilio na hasa sehemu ya kwanza inatukumbusha Wakristo wote kujua kwamba uwepo wetu hapa duniani ni kama “ziara.” Tunapaswa daima kukesha na kuwa macho; “Kwa maana wokovu wetu u karibu sasa kuliko tulipoanza kuamini; usiku umeenda, mchana umekaribia (Rum, 13:11-14).” Tusiishi kana kwamba tumemaliza mwendo tukasahau kuwa tupo “ziarani” makao yetu ni mbinguni. Majilio kwa mkristo ni fursa ya kuamsha tena ndani yetu maana halisi ya kungoja, tukirejea kiini cha imani yetu ambapo ni fumbo la Kristo, Masihi aliyengojewa kwa karne nyingi na kuzaliwa katika umaskini huko Bethlehemu.

Waamini wajiandae ili Yesu azaliwe tena nyoyoni mwao.
Waamini wajiandae ili Yesu azaliwe tena nyoyoni mwao.

Kwa kuja kati yetu, ametuleta na anaendelea kutupa zawadi ya upendo wake na wokovu wake. Akiwa kati yetu, anazungumza nasi kwa njia nyingi: katika Maandiko Matakatifu, katika mwaka wa kiliturujia, katika watakatifu, katika matukio ya maisha ya kila siku na katika uumbaji wote. Tunaweza kuzungumza naye, kuwasilisha kwake mateso yanayotupata, kukosa subira na maswali yanayobubujika kutoka mioyoni mwetu. Kila tunapo anza Mwaka wa Liturujia ni lazima kusahihisa kasoro tulizo fanya mwaka uliopita na kuanza upya, tukiiga mfano mzuri wa maisha ya wahusika wakuu katika Kipindi hiki ambao ni: Nabii Isaya, Yohane Mbatizaji, Zakaria na mkewe Elizabeti Wengine wanaopamba kipindi hiki ni: Wachungaji wa kondeni, Mamajusi, watu wa kawaida lakini kwa namna ya pekee, Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu wawe ni mifano bora ya kuigwa katika kipindi hiki cha Majilio! Hawa ni watu walioguswa kwa namna ya pekee na maandalizi ya ujio wa Masiha. Bwana wetu Yesu Kristo ndiye nguzo kuu ya tafakari katika kipindi hiki. Jambo hili yafaa lifanyike na kila mmoja wetu tukijua kuwa sote ni watoto wa Kanisa moja, takatifu, katoliki na la Mitume chini ya mchungaji mwema Bwana wetu Yesu Kristo. Tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa hii mpya ya kutustahilisha tena kuingia katika mzunguko wa mwaka mpya wa Liturujia ya Kanisa, tuendelee kumwomba neema na baraka zake aendelee kutuongoza.

Papa Majilio
24 November 2022, 15:04