Tafuta

CEI, kuanzia tarehe 24-27 Novemba 2022 limekuwa likiendesha huko Verona, Kongamano la 12 la Mafundisho Jamii ya Kanisa. Kauli mbiu “Ni katika "Kujenga uaminifu. Shauku ya kukutana." CEI, kuanzia tarehe 24-27 Novemba 2022 limekuwa likiendesha huko Verona, Kongamano la 12 la Mafundisho Jamii ya Kanisa. Kauli mbiu “Ni katika "Kujenga uaminifu. Shauku ya kukutana."  

Mafundisho Jamii ya Kanisa Ni Amana na Utajiri wa Maisha Adili

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia: Kongamano la 12 la Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Ni katika "Kujenga uaminifu. Shauku ya kukutana." Licha ya changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo, lakini Kanisa halina budi kuendelea kujikita katika kukuza na kudumisha matumaini, utu, heshima na haki msingi za binadamu

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapata chimbuko lake mintarafu kanuni na muundo wa elimu fahamu, taalimungu, hususan taalimungu maadili ambayo ni dira na mwongozo wa maisha ya watu. Yanachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa na imani thabiti ambayo inamwilisha Neno la Mungu katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Mambo msingi katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu: Amani katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Hizi ni tunu ambazo ni urithi mkubwa kwa binadamu wote kwani zinabubujika kutoka katika asili ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu hivyo zinapaswa kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa na wote; kwa kuzingatia kwamba, haki inakwenda sanjari na wajibu; hakuna haki pasi na wajibu. Hii ni haki ya kuishi, kupata huduma bora ya makazi, afya, elimu, kuabudu, uhuru wa dhamiri, uhuru wa kuchagua mfumo wa maisha; haki za kiuchumi na kisiasa pamoja na uhuru wa kwenda unakotaka kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo. Kanisa Katoliki lina amana na utajiri mkubwa wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayopata chimbuko lake katika Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Leo XIII; Mambo Mapya; Rerum Novarum.

Kiini cha Mafundisho Jamii ya Kanisa: Utu, heshima na haki msingi
Kiini cha Mafundisho Jamii ya Kanisa: Utu, heshima na haki msingi

Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, katika Waraka wake kuhusu Masuala ya Kijamii Centesimus Annus, alifafanua kwa kina kuhusu asili ya haki msingi za binadamu; umuhimu wa kukuza na kudumisha upendo na mshikamano miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa, kama inavyojidhihirisha katika Waraka wake wa “Sollicitudo Rei Socialis” cheche ya uanzishaji wa vyama vya kitume kijamii vilivyokuwa vinapania kulinda na kutetea uhuru, utu na haki msingi za binadamu. Itakumbukwa kwamba, uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu ni muhtasari wa haki zote za binadamu. Dini zisaidie kujenga amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu na kamwe zisiwe ni chanzo cha vurugu, kinzani na vita. Kanuni maadili na utu wema ni sehemu muhimu sana katika maisha ya mwanadamu zinazopaswa kulindwa ili amani na utulivu viweze kushika kasi, bila kusahau nafasi na dhamana ya uwepo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Waamini wanapaswa kufahamu vyema kweli za imani yao ili wasiyumbishwe, bali wasimame kidete kuilinda na kuitetea kwa ajili ya ustawi, mafao ya maendeleo ya wengi.

Mafundisho Jamii ya Kanisa: Umoja na Mshikamano wa Kimataifa
Mafundisho Jamii ya Kanisa: Umoja na Mshikamano wa Kimataifa

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, kuanzia tarehe 24-27 Novemba 2022 limekuwa likiendesha huko Verona, Kongamano la 12 la Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Ni katika "Kujenga uaminifu. Shauku ya kukutana." Licha ya changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo, lakini Kanisa halina budi kuendelea kujikita katika kukuza na kudumisha matumaini, utu, heshima na haki msingi za binadamu dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika vita, uchoyo na ubinafsi uliokithiri. Waamini wajiaminishe kwa Mwenyezi Mungu kwa kujikita mchakato wa ujenzi wa matumaini. Mada zilizochambuliwa na wataalamu mbalimbali ni pamoja na: Mustakabali wa demokrasia; Uhuru na Mfumo Mpya wa Mahusiano Kimataifa. Vijana: Mahusiano, mapenzi, urafiki na ujenzi wa jumuiya. Ufunguo wa majadiliano haya ni majadiliano kama njia ya maisha ya uaminifu wa mwanadamu iliyo wazi katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana sanjari na uwajibikaji wa kijamii. Wamegusia kuhusu ruzuku, mafunzo ya watalaam; uzoefu mpya katika ushirikiano wa Kimataifa; Mustakabali kati ya watu na Mazingira; Fedha na Uchumi fungamani; tuzo kwa wafanyakazi bora; Changamoto ya uzazi nchini Italia; Uzuri wa kutoa zawadi. Kongamano hili limefungwa rasmi kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Mario Grech, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu.

Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unasimikwa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu.
Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unasimikwa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa Kongamano la 12 la Mafundisho Jamii ya Kanisa, amewataka watu wa Mungu nchini Italia kuwa ni wasanii wa jamii inayoaminiana na wajenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika msingi wa amani, usalama na utulivu dhidi ya utamaduni wa kifo unaoendelea kuwatumbukiza watu katika umaskini; kuwapoka watoto nafasi ya kusoma na kupata matibabu bora. Hii ni dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa ujasiri mkubwa kwa kuaminiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja. Huu ni mwaliko wa kumtumainia na kumtegemea Mwenyezi Mungu pamoja na jirani. Nabii Yeremia anasema, “Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA, Ambaye BWANA ni tumaini lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda.” Yer 17: 7-8. Matumaini ni chachu muhimu katika maisha inayokamilika kwa kushirikiana, kuthaminiana na kutegemezana kwa kupendana na wengine, ili kuimarishana na kukua kwa pamoja; kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadanu. Hii ni njia inayoiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kuondokana na dhana ya vita duniani na tabia ya kudhaniana kuwa maadui, chanzo cha Vita duniani.

Ushiriki wa Watu wa Mungu katika maisha na utume wa Kanisa
Ushiriki wa Watu wa Mungu katika maisha na utume wa Kanisa

Kardinali Mario Grech, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu katika mahubiri yake, Dominika ya kwanza ya Kipindi cha Majilio Mwaka A wa Kanisa amekazia kuhusu: Umuhimu wa kukesha kwa sababu Mkombozi anakuja; Safari ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Mwanga wa ujio wa Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu utafunua ukweli wa maisha ya kila mwamini, ndiyo maana mwaliko wa jumla ni “kesheni basi, kwa maana hamjui siku ipi atakayokuja Bwana wenu, kufunga Agano Jipya na la milele, kwa njia ya Fumbo la Msalaba, kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Lengo ni kuwawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni wasanii wa jamii inayoaminiana na wajenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika msingi wa amani, usalama na utulivu dhidi ya utamaduni wa kifo, kama ambavyo Baba Mtakatifu Francisko amekazia katika ujumbe wake kwa washiriki. Katika kipindi hiki cha Majilio, waamini wanaalikwa kukesha na kuhakikisha kwamba, kila mmoja wao anatekeleza dhamana na majukumu yake kadiri ya sheria, taratibu na kanuni, daima wakijitahidi kusimama kidete kulinda na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Waamini wasimezwe na malimwengu na hivyo wakajikuta wanatopea katika mazoea na hivyo kushindwa kusoma alama za nyakati.

Mafundisho Jamii ya Kanisa ni muhimu katika uwanja wa kisiasa
Mafundisho Jamii ya Kanisa ni muhimu katika uwanja wa kisiasa

Ujumbe mahususi hapa ni “Kesheni” kumbe, ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unasimikwa katika mchakato wa kusoma alama za nyakati mintarafu maongozi ya Roho Mtakatifu, ili hatimaye, Injili iweze kupenya na kuitajirisha jamii; kwa kukazia uhuru unaofumbatwa katika wokovu unaopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu na hivyo kuenea katika maisha ya kijamii katika masuala ya kisiasa; kiuchumi, kazi, sheria na tamaduni, ili kujenga na kuimarisha ushirika wa watu wa Mungu, haki na amani, mintarafu hekima ya Kimungu. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapania pamoja na mambo mengine: kumjengea mwanadamu uhuru kamili, kama sehemu msingi ya maisha na utume wake. Huruma, upendo na wokovu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Waamini wawe makini kusoma alama za nyakati katika hija ya maisha yao hapa duniani, daima wakiwa wameungana na kushikamana na Kristo Yesu Mkombozi wa ulimwengu pamoja na Kanisa lake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Monsinyo Adriano Vincenzi aliyezaliwa tarehe 4 Novemba 1952, Muasisi wa Makongamano ya Mafundisho Jamii ya Kanisa ni mfano bora wa kuigwa katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana na kuaminiana. Tarehe 25 Juni 1977 alipewa Daraja Takatifu ya Upadre, akajikita zaidi katika malezi, majiundo na makuzi ya kijamii na kisiasa. Baada ya mapambano na ugonjwa wa muda mrefu, tarehe 13 Februari 2020 akafariki dunia na kulala katika usingizi wa amani.

Mafundisho Jamii
27 November 2022, 15:42