Tafuta

Wafranciskani 300 wameteuliwa kuratibu Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Francisko wa Assisi. Wafranciskani 300 wameteuliwa kuratibu Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Francisko wa Assisi.  (Vatican Media)

Jubilei ya Miaka 800 Tangu Mtakatifu Francisko wa Assisi Afariki Dunia 2023-2026: Ushuhuda

Mtakatifu Francisko anatambulikana sana kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: Maskini, Amani na Mazingira nyumba ya wote; chimbuko la yote haya ni upendo kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kiasi cha kumzawadia Madonda Matakatifu, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha: unyenyekevu, huruma na upendo wa Mungu. Jubilei ya Miaka 800 tangu afariki dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wafranciskani 300 wameteuliwa kuratibu Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Francisko wa Assisi, Mlinzi na Mwombezi wa Italia, 2023-2026. Mtakatifu Francisko wa Assisi aliishi kati ya Mwaka 1181 hadi tarehe 3 Oktoba 1226. Maadhimisho ya Jubilei hii yalizinduliwa rasmi tarehe 29 Novemba 2021 na kilele chake ni tarehe 3 Oktoba 2026, kwa kuwashirikisha kikamilifu waamini walei na watawa kuweza kutembea kwa pamoja. Mtakatifu Francisko anatambulikana sana kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: Maskini, Amani na Mazingira nyumba ya wote; chimbuko la yote haya ni upendo kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kiasi cha kumzawadia Madonda Matakatifu, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha: unyenyekevu, huruma na upendo wa Mungu. Huu ni mwaliko wa kumfuasa Kristo Yesu, kwa kusoma, kutafakari hatimaye, kumwilisha Habari Njema ya Wokovu katika uhalisia wa maisha ya waamini kwa kushuhudia upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa njia ya ufukara wa Kiinjili, Wafranciskani, wanahimizwa kupyaisha sura ya Mama Kanisa katika maisha na huduma zao. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko, kwa Waratibu wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Francisko wa Assisi.

Maandalizi ya Jubilei ya Miaka 800 tangu Mt. Francisko wa Assisi afariki dunia
Maandalizi ya Jubilei ya Miaka 800 tangu Mt. Francisko wa Assisi afariki dunia

Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amebainisha hatua kuu tatu za maisha na utume wa Mtakatifu Francisko wa Assisi: Hatua ya kwanza 1223 ni Fumbo la Umwilisho, Njia ya Mungu na matokeo yake ni katika maisha ya Mtakatifu Francisko. Pili ni mwaka 1224 Madonda Matakatifu, Tafakari ya Fumbo la Pasaka katika maisha na utume wa Mtakatifu Francisko. Tatu ni mwaka 2026: Matumaini ya maisha na uzima wa milele. Huu ni mwaliko kwa Wafranciskani: Kusikiliza, Kutembea na Kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Jubilei ya Miaka 800 tangu Mtakatifu Francisko alipofariki dunia, iwe ni fursa ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, tayari kupyaisha uso wa Kanisa. Huu ni mwaliko wa kugundua tena ndani mwao, umuhimu wa Fumbo la Umwilisho kama kielelezo cha Njia ya Kristo Yesu na Njia ya Mwenyezi Mungu. Kristo Yesu Adamu Mpya anafafanua Fumbo la Upendo wa Mungu linalojidhihirisha kikamilifu kwa binadamu na jinsi alivyo na hatimaye, kumjulisha wito wake mkuu. Ukuu na utakatifu wa binadamu unashuhudiwa kwa namna ya pekee kabisa katika Fumbo la Umwilisho. Rej. Gaudium et spes, 22.

Ushirikiano na mshikamano wa watu wa Mungu: Ushuhuda
Ushirikiano na mshikamano wa watu wa Mungu: Ushuhuda

Pili ni mwaka 1224 Madonda Matakatifu, Tafakari ya Fumbo la Pasaka katika maisha na utume wa Mtakatifu Francisko. Fumbo la Pasaka, lilisaidia kumtakasa na kumwiimarisha Mtakatifu Francisko wa Assisi, kiasi cha kuthubutu kuzika udhaifu na mapungufu yake ya kibinadamu, na hatimaye, kufunuliwa Ufufuko wa miili na uzima wa milele ijayo, kielelezo cha utakatifu na utukufu wa Mungu. Huu ni mwaliko wa kusikiliza kwa makini, kutembea na hatimaye, kutangaza Habari Njema ya Wokovu pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, tayari kupyaisha uso wa Kanisa, kwa kutumia nguvu na ukarimu wake. Hii ni changamoto kwa Wafranciskani kuendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa; kwa kulipenda na kulitumikia kwa sababu ni kielelezo cha uso wa Kristo. Wafranciskani wanahimizwa kutembea, ili kuweza kukutana na watu na hivyo kujenga madaraja na hatimaye, kupunguza umbali kati ya Kanisa na watu wateule wa Mungu. Ni wakati wa kusimama na kutafakari; kwa kuendelea kuzama zaidi katika sala, tayari kuwatangazia na kuwashuhudia watu wa Mungu huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.

Jubilei ya Miaka 800: 2023-2026: Sala inayomwilishwa katika matendo
Jubilei ya Miaka 800: 2023-2026: Sala inayomwilishwa katika matendo

Wafranciskani kwa kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema, wanahimizwa kujizatiti kikamilifu katika kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa zilizopo, kwa ajili ya kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kwa kuzingatia mambo haya msingi, walimwengu wanaweza kusimamia mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu bila kukata tamaa. Maadhimisho ya kumbukizi ya Miaka 60 tangu kuzinduliwa kwa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican chini ya uongozi wa Mtakatifu Yohane wa XXIII, imekuwa ni fursa ya maandalizi ya Mwaka wa kwanza wa Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025. Hiki ni kipindi cha Kanisa kujikita zaidi katika Nyaraka Kuu 4 za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican yaani: “Dei verbum” yaani “Ufunuo wa Kimungu”, “Sacrosanctum concilium” yaani “Juu ya Liturujia”; “Lumen gentium” yaani “Fumbo la Kanisa” pamoja na “Gaudium et spes” yaani “Kanisa katika ulimwengu mamboleo.” Mtakatifu Francisko wa Assisi anapenda kulihamasisha Kanisa katika ulimwengu mamboleo kujikita katika uaminifu kwa Kristo Yesu na hivyo kuendeleza utume wake wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa ari, bidii na moyo mkuu kwa watu wa nyakati hizi.

Jubilei ya Miaka 800
02 November 2022, 14:00