Hija za Kitume Mjini Vatican Zinalenga Kuimarisha Urika wa Maaskofu na Papa: Umoja!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, katika Kanisa hili la Kristo Yesu, Kuhani Mkuu wa Roma, aliye mwandamizi wa Mtakatifu Petro, ambaye Kristo Yesu alimkabidhi kondoo na wanakondoo wake ili awachunge, kwa agizo la kimungu amepokea mamlaka ya juu kabisa, kamili na yanayojitegemea na ya jumla kwa ajili ya huduma ya roho za watu “Curam animalum.” Hivyo basi, kwa kuwa amewekwa kuwa mchungaji wa waamini wote, ili kukuza manufaa ya wote na ya Kanisa zima na pia ya Makanisa mahalia, anashika mamlaka ya juu ya kawaida juu ya Makanisa yote. Kwa upande mwingine na Maaskofu wamewekwa na Roho Mtakatifu kuwa waandamizi wa Mitume kama wachungaji wa watu, na pamoja na Baba Mtakatifu na chini ya Mamlaka yake, wanao utume wa kudumisha kazi ya Kristo Mchungaji wa milele, kwa sababu Kristo Yesu aliwapa Mitume na waandamizi wao agizo na mamlaka ya kuwafundisha mataifa yote, ya kuwatakatifuza watu katika ukweli na kuwachunga. Rej. Christus Dominum, n. 2-3. Papa Sixtus wa V kunako mwaka 1585 alianzisha hija za kitume zinazotekelezwa na Maaskofu Jimbo mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano, yaani “Ad Limina Apostolorum Visitatio” na kwa kifupi, “Ad Limina.”
Kwa busara yake ya kichungaji akaamuru Maaskofu wote Katoliki kutembelea mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano. Hii ni nafasi ya kutembelea na kusali kwenye Makaburi ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani. Kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu pamoja na kutoa taarifa ya Maandishi kwa Baraza la Kipapa la Maaskofu kuhusu mwenendo mzima wa maisha na utume wa Kanisa katika Jimbo husika. Ni fursa pia ya kujadiliana na wakuu wa Mabaraza ya Kipapa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo Yesu. Hija hizi ni za manufaa sana kwa ajili ya kukoleza kazi ya Kristo Yesu kwa ajili ya Kanisa lake sanjari na huduma kwa roho za waamini “Curam animarum.” Kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika hija za kitume zinazotekelezwa na Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbalimbali za dunia katika muktadha wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, Baba Mtakatifu Francisko anakazia zaidi utamaduni wa kusikiliza na kujifunza kutoka katika Makanisa mahalia.
Mtakatifu Paulo VI, Muasisi wa maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu mara baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican anasema, Sinodi ni chombo cha kimisionari na uinjilishaji mpya unaolisaidia Kanisa baada ya kutembea pamoja katika sala, tafakari, mang’amuzi na hatimaye, utekelezaji wake unaofanywa na watu wote wa Mungu kadiri ya wito na nafasi zao katika maisha na utume wa Kanisa. Sinodi ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Ni katika muktadha huu, hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar wakati wa Hija ya Kitume mjini Roma “Ad limina Apostolorum.” Baba Mtakatifu pia amekutana na kuzungumza na Maaskofu Katoliki kutoka Kanda ya Kusini mwa Brazil. Kati ya mambo ambayo Baba Mtakatifu amekazia ni: haki, amani na utulivu. Bwana Luiz Lula Da Silva kutoka kambi ya mrengo wa kushoto, ambaye aliwahi pia kuiongoza Brazil kutoka mwaka 2003 hadi 2010 ameibuka kidedea katika uchaguzi wa marudio uliofanyika tarehe 30 Oktoba 2022 kwa kupata kura 60,345,999 sawa na asilimia 50.9% ya kura zote halali zilizopigwa siku hiyo. Kumekuwepo na mpasuko mkubwa pamoja na vurugu za kisiasa nchini Brazil kutokana na uchaguzi wa marudio.
Baba Mtakatifu Francisko aliwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Aparecida, Mlinzi na Mwombezi wa Brazil, ili aweze kuwalinda na kuwaponya; awaweke huru kutokana na chuki, vurugu na hali ya kutokuvumiliana. Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu Katoliki nchini Brazila kusimama kidete katika sheria, kanuni na Mafundisho ya Kanisa, ili kuweza kukabiliana na changamoto za maisha na kamwe wasiogope changamoto kwani ni fursa katika mchakato wa maboresho ya maisha, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu. Maaskofu Katoliki Brazil wanakiri kwamba, katika mazungumzo yao: ukweli, uwazi, upendo na mshikamano wa shughuli za kichungaji ni kati ya mambo makubwa yaliyojadiliwa kati ya Baba Mtakatifu na Maaskofu Katoliki kutoka Brazil. Baba Mtakatifu ameonesha sadaka na majitoleo, licha ya changamoto za kiafya, lakini ameweza kukaa pamoja na Maaskofu wenzake ili kusikilizana. Baba Mtakatifu ameonesha kuwa ni mtu mwenye furaha kubwa, akitoa mwaliko wa kujadiliana masuala ya maisha na utume wa Kanisa katika ukweli na uwazi kwa ajili ya: ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo. Baba Mtakatifu kwa hakika wanasema Maaskofu Katoliki Brazil kwamba, ameonesha upole, ubaba na ukaribu. Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kujenga na kudumisha ari na mwamko wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalosimikwa katika umoja, ushiriki na utume wa Kanisa.