Tafuta

Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Baraza Kuu la Wazee wa Kiislam “Muslim Council of Elders”  kwenye Msikiti Mkuu wa Sakhir. Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Baraza Kuu la Wazee wa Kiislam “Muslim Council of Elders” kwenye Msikiti Mkuu wa Sakhir. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Bahrain: Hotuba Kwa Baraza Kuu la Wazee Wa Dini ya Kiislam

Baba Mtakatifu amesema kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye chanzo cha amani; ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana, kuheshimiana na kuthaminiana ili kudumisha uhai wa binadamu dhidi ya utamaduni wa kifo. Waamini wajenge mahusiano na mafungamano yao katika sala na udugu wa kibinadamu, ili kwa pamoja waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali za Kimataifa. Amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya 39 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa Ufalme wa Bahrain kuanzia Alhamisi tarehe 3 hadi Dominika tarehe 6 Novemba 2022, ni kumwezesha kushiriki katika maadhimisho ya Kongamano la Bahrain la Majadiliano: Mashariki na Magharibi Kwa Ajili ya Kuishi Pamoja Kwa Binadamu lililohitimishwa Ijumaa tarehe 4 Novemba 2022 kwa ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko. Hii pia ni fursa ya kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo sanjari na ujenzi wa udugu wa kibinadamu, kama sehemu ya mchakato wa kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Baraza Kuu la Wazee wa Kiislam “Muslim Council of Elders”  kwenye Msikiti Mkuu wa Sakhir. Baraza hili liliundwa tarehe 18 Julai 2021 ili kuragibisha amani katika Jumuiya za Waamini wa Dini ya Kiislam. Baraza linaundwa na wasomi wa dini ya Kiislam, waamini mashuhuri, wataalam na viongozi wa sheria. Lengo ni kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano miongoni mwa Jumuiya za waamini wa dini ya Kiislam, kwa kusimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za dini ya Kiislam, Kiutu na Kijamii, kwa kukazia maridhiano dhidi chuki na ghasia zinazotaka kuwagawa waamini katika madhehebu.

Maadili, utu wema na elimu ni muhimu kwa vijana wa kizazi kipya.
Maadili, utu wema na elimu ni muhimu kwa vijana wa kizazi kipya.

Mkutano huu umetajirishwa na sehemu ya Maandiko Matakatifu kutoka katika Quran Tukufu, Agano la Kale na baadaye viongozi mbalimbali wamepata fursa ya kutoa neno wakiwemo wawakilishi wa Baraza Kuu la Wazee wa Kiislam na ujumbe wa Vatican umeongozwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na salam za Vatican katika mkutano huu kutolewa na Kardinali Miguel Á. AYUSO GUIXOT, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, amewatakia heri na baraka katika mchakato wa kudumisha amani kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye chanzo cha amani; ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana, kuheshimiana na kuthaminiana ili kudumisha uhai wa binadamu dhidi ya utamaduni wa kifo. Waamini wajenge mahusiano na mafungamano yao katika sala na udugu wa kibinadamu, ili kwa pamoja waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali za Kimataifa. Baba Mtakatifu Francisko amewaombea wajumbe wa Baraza Kuu la Wazee wa Kiislam “Muslim Council of Elders”  kwenye Msikiti Mkuu wa Sakhir fadhila ya amani inayosimikwa katika utamaduni wa kuheshimiana, kuaminiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja. Amewapongeza kwa kujielekeza zaidi katika malezi na makuzi ya vijana wa kizazi kipya kwa kukazia maadili na utu wema sanjari na elimu makini ili kuondokana na chuki na tabia ya kutowavumilia wengine.

Ujenzi wa udugu wa kibinadamu ni muhimu katika kudumisha amani duniani
Ujenzi wa udugu wa kibinadamu ni muhimu katika kudumisha amani duniani

Mwenyezi Mungu ndiye chemchemi ya amani, anayewawezesha waamini kwa wakati wao kuwa ni mito ya amani, changamoto kwa waamini ni kuendelea kujikita katika utamaduni wa kukutana na kujadiliana katika msingi wa haki. Amani ni matunda ya udugu wa kibinadamu dhidi ya ukosefu wa haki msingi za binadamu na usawa na inakita mizizi yake katika uhalisia wa maisha ya watu, ili kung’oa mifumo yote ya ubaguzi na ukosefu wa usawa. Waamini wajitahidi kutangaza, lakini zaidi kumwilisha amani inayobubujika kutoka katika sakafu ya nyoyo zao, ili kuweza kukutana na kutembea pamoja katika umoja. Lengo ni kudumisha udugu wa kibinadamu kwa kufyekelea mbali maamuzi mbele, ili kujenga na kudukisha amani, uhuru, haki jamii na maadili na utu wema. Hii ni dhamana na wajibu nyeti wa viongozi wa kidini duniani, kwani wamepewa jukumu la kumhudumia mwanadamu kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kujenga na kudumisha utamaduni wa maisha kwa kusimama kidete dhidi ya utamaduni wa kifo pamoja na kuendelea kujielekeza zaidi katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Vijana warithishwe elimu bora,  maadili na utu wema
Vijana warithishwe elimu bora, maadili na utu wema

Kama waamini wanamwamini Mungu mmoja, mafungamano ya kijamii Kitamataifa na upendo wa kidugu unaopata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Huu ni wajibu wao wa kuendelea kujikita katika maisha ya sala na ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Watambue uwepo wa Mwenyezi Mungu katika maisha yao na kwamba, wanaitwa kusaidiana katika maisha. Usalama, amani na utulivu vinahatarishwa na wale wanaojiaminisha kwenye matumizi ya nguvu, vita na manunuzi makubwa ya silaha. Kuna mamilioni ya watu wanaolazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na vita, kinzani na migogoro ya kijamii na kisiasa kutokana na baadhi ya watu kutopea katika uchu wa: fedha, mali na madaraka. Ujenzi wa udugu wa kibinadamu ndiyo unaweza kuokoa mwelekeo huu ambao ni hatari katika maisha ya mwanadamu, kwa kuwekeza zaidi katika vitendo, kwani wote ni watoto wa Abrahamu katika imani. Ujenzi wa umoja miongoni mwa binadamu ni jambo la msingi sana. Leo hii anasema Baba Mtakatifu ulimwengu umegubikwa na mateso, maovu, vifo na ukosefu wa haki. Kuna mamilioni ya watu wanaosiginwa na baa la njaa na umaskini. Huu ni mwaliko wa kutangaza na kudumisha amani duniani; kwa kushirikiana na kushikamana kama ndugu wamoja, ili kutembea katika mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ili hatimaye, mwanga angavu wa amani, uweze kung’aa na kutawala katika akili na nyoyo za watu!

Baraza Kuu wazee
04 November 2022, 16:19