Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 18 Novemba 2022 amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 18 Novemba 2022 amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani   (ANSA)

Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani Lakutana na Papa Francisko Mjini Vatican...!

Maaskofu wanawajibika kukuza na kuhifadhi umoja wa imani na nidhamu iliyo moja kwa Kanisa lote; tena kuwafundisha waamini wawe na upendo kwa Kanisa hasa kwa viungo vilivyo maskini, vyenye kuteswa na kuudhiwa kwa ajili ya haki. Maaskofu wanawajibika kuendeleza utendaji wote unaohusu Kanisa lote, ili imani ipate kukua na mwanga wa ukweli kamili uwazukie watu wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maaskofu wamewekwa na Roho Mtakatifu kuwa Waandamizi wa Mitume kama wachungaji wa watu, na pamoja na Baba Mtakatifu na chini ya Mamlaka yake, wanao utume wa kudumisha kazi ya Kristo Mchungaji wa milele, kwa sababu Kristo Yesu aliwapa Mitume na Waandamizi wao agizo na mamlaka ya kuwafundisha mataifa yote, ya kuwatakatifuza watu katika ukweli na kuwachunga. Rej. Christus Dominum, n. 2-3. Papa Sixtus wa V kunako mwaka 1585 alianzisha hija za kitume zinazotekelezwa na Maaskofu Jimbo mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano, yaani “Ad Limina Apostolorum Visitatio” na kwa kifupi, “Ad Limina.” Kwa busara yake ya kichungaji akaamuru Maaskofu wote Katoliki kutembelea mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano. Hii ni nafasi ya kutembelea na kusali kwenye Makaburi ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani. Ni fursa ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu pamoja na kutoa taarifa ya Maandishi kwa Baraza la Kipapa la Maaskofu kuhusu mwenendo mzima wa maisha na utume wa Kanisa katika Jimbo husika. Ni wakati muafaka wa kujadiliana na wakuu wa Mabaraza ya Kipapa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo Yesu. Hija hizi ni za manufaa sana kwa ajili ya kukoleza kazi ya Kristo Yesu kwa ajili ya Kanisa lake sanjari na huduma kwa roho za waamini “Curam animarum.” Kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika hija za kitume zinazotekelezwa na Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbalimbali za dunia katika muktadha wa mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, Baba Mtakatifu Francisko anakazia zaidi utamaduni wa kusikilizana, kujadiliana na kujifunza kutoka katika Makanisa mahalia.

Baraza la Maaskofu Katoliki Canada, ad limina visit 2022
Baraza la Maaskofu Katoliki Canada, ad limina visit 2022

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 18 Novemba 2022 amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani “The German Bishops' Conference (Deutsche Bischofskonferenz). Katika mkutano huu, kulikuwepo jumla ya Maaskofu 62 ambao baadaye wamekutana na kufanya mkutano na Wakuu wa Mabaraza ya Kipapa kwenye Ukumbi wa “Taasisi ya Augustianum” iliyoko mjini Roma. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican ndiye aliyeratibu mkutano huu. Kati ya mada zilizojadiliwa ni pamoja na Sinodi ya Kanisa Katoliki Nchini Ujerumani, inayopembua juu ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa nchini Ujerumani. Kardinali Pietro Parolin amekazia umuhimu wa Maaskofu kuwajibika kukuza na kuhifadhi umoja wa imani na nidhamu iliyo moja kwa Kanisa lote; tena huwafundisha waamini wawe na upendo kwa Mwili wote wa fumbo wa Kristo, hasa kwa viungo vilivyo maskini, vyenye kuteswa na kuudhiwa kwa ajili ya haki. Maaskofu wanawajibika kuendeleza utendaji wote unaohusu Kanisa lote, hasa kusudi imani ipate kukua na mwanga wa ukweli kamili uwazukie watu wote. Rej. Lumen gentium, 23.

Urika wa Maaskofu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro ni muhimu
Urika wa Maaskofu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro ni muhimu

Kardinali Parolin amesikika akisema kwamba, hii ilikuwa ni fursa ya neema na mazungumzano; ili kukuza na kudumisha umoja na utofauti katika maisha na huduma ya Kanisa. Ameonesha hatari inayoweza kujitokeza ndani ya Kanisa kutokana na msimamo wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Ujerumani kuitisha na kuadhimisha Sinodi inayoweza kutafsiriwa kuwa ni mageuzi ya Kanisa na wala si mchakato wa mageuzi ndani ya Kanisa lenyewe, jambo ambalo linapewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko. Kwa upande wake, Baraza la Maaskofu Katoliki Ujeruman “The German Bishops' Conference (Deutsche Bischofskonferenz) limepembua kwa kina na mapana, mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Kanisa Katoliki nchini Ujerumani; ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza watu wa Mungu nchini Ujerumani; madhara ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Wamegusia kuhusu madaraka na mgawanyo wa madaraka ndani ya Kanisa; Ushiriki wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa; sera na mikakati ya kimisionari; Maisha na utume wa Wakleri katika ulimwengu wa utandawazi; Wanawake wakatoliki na madaraka katika Kanisa; maisha na mafungamano yenye afya kwa utume wa Kanisa; upendo na maisha ya ndoa na familia.

Umoja wa Kanisa upewe kipaumbele cha kwanza
Umoja wa Kanisa upewe kipaumbele cha kwanza

Maaskofu Katoliki wa Ujerumani wamempongeza na kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuitisha Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ambayo kwa sasa yamegawanywa katika awamu kuu mbili. Awamu ya kwanza ni kuanzia tarehe 1-29 Oktoba 2023 na Awamu ya Pili ni Mwezi Oktoba 2024 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Lengo kuu la Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake. Pili ni kuendelea kufanya mang’amuzi ya kina kuhusu dhana ya Sinodi kama chombo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa Mataifa. Kardinali Luis Francisco Ladaria Ferrer, S.J., Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na Kardinali Marc Armand Ouellet, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu wamedadavua masuala tete mintarafu mwanga wa kitaalimungu kuhusu hofu iliyojitokeza katika mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Kanisa nchini Ujerumani kuhusu: Njia zilizotumika, Maudhui pamoja na mchakato mzima wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi; Umuhimu wa ujenzi wa umoja na ushiriki wa Kanisa; dhamana na utume wake wa Uinjilishaji wa mtu mzima kama sehemu ya Maadhimisho ya Sinodi kwa Kanisa zima.

Sinodi ya Kanisa Katoliki Nchini Ujerumani
Sinodi ya Kanisa Katoliki Nchini Ujerumani

Baadaye yalifuatia majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi mintarafu madonda yanayojitokeza katika mfumo wa uongozi wa Kanisa, Utume na maisha ya Kipadre pamoja na uelewa wa binadamu kadiri ya Mafundisho ya Mama Kanisa. Wajumbe katika umoja wao, wamekiri kuhusu umuhimu wa kushikamana na kufungamana na watu wa Mungu katika maisha na utume wa Kanisa na pale inapowezekana washirikishwe pia madaraka. Mchakato wote huu ni kuhakikisha kwamba, Mama Kanisa anaendelea kujielekeza zaidi katika utume na dhamana ya uinjilishaji. Imeonekana haja ya kushughulikia Sinodi ya Kanisa Katoliki nchini Ujerumani, kwa kujadiliana na kusikilizana katika ukweli na uwazi, ili kuondokana na hofu pamoja na wasiwasi uliojitokeza kiasi kwamba, Sinodi hii inaonekana kutokuwa na muafaka na Kanisa la Kiulimwengu. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, mwishoni mwa mkutano huu, amewashukuru na kuwapongeza wajumbe wote jinsi walivyoshiriki katika majadiliano haya hata kama hayakuwa rasmi, lakini yameonesha umuhimu wa kuzingatia na kuufanyia kazi mchango uliotolewa na wajumbe wa mkutano huo. Kuanzia sasa wajumbe wamekazia kwa namna ya pekee, ujenzi wa utamaduni wa kusikilizana, unaowawezesha watoto wa Kanisa kutajirishana katika maadhimisho ya Sinodi zote mbili yaani Sinodi ya Kanisa Nchini Ujerumani sanjari na Sinodi ya kumi na sita ya Maaskofu Ulimwenguni kote.

Ad Limina
19 November 2022, 15:31