Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 20 Oktoba 2022 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Mariannhill Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 20 Oktoba 2022 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Mariannhill  (Vatican Media)

Wamisionari Muwe Waaminifu Kwa Karama ya Shirika & Jengeni Mshikamano wa Upendo

Papa Francisko amekazia umuhimu wa kuwa waaminifu katika karama ya Shirika; kwa kuendelea kumwilisha kauli mbiu “Mshikamano: Mnaitwa katika nia moja na shauri moja” katika maisha na utume wao; kwa kumtegemea Roho Mtakatifu ili waweze kukua na kukomaa katika utakatifu na uaminifu wa huduma ya Injili., karama na mashauri ya Kiinjili yaani: Useja, Utii na Ufukara.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Wamisionari wa Mariannhill (Congregatio Missionariorum de Mariannhill, C.M.M.) na Mtumishi wa Mungu Abate Franz Pfanner kunako mwaka 1909 huko Mariannhill, KwaZulu Natal, nchini Afrika ya Kusini. Kwa sasa linatekeleza dhamana na utume wake nchini Afrika ya Kusini, Austria, Ujerumani, Hispania, Uswis, Uingereza, Marekani, Canada, Zambia, Zimbabwe na Colombia. Lengo la kuanzishwa kwa Shirika hili lilikuwa ni kusaidia mchakato wa ujenzi wa Kanisa mahalia kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mungu nchini Afrika ya Kusini. Shirika la Wamisionari wa Mariannhill kuanzia tarehe 3 hadi 24 Oktoba 2022 wanaadhimisha Mkutano Mkuu wa 17 wa Shirika ambao unanogeshwa na kauli mbiu inayochota amana na utajiri wake kutoka katika Waraka wa kwanza wa Mtakatifu Paulo kwa Wakorintho: “Mshikamano: Mnaitwa katika nia moja na shauri moja.” 1Kor 1:10 Hii ni tema ambayo wanahamasishwa kuimwilisha katika medani mbalimbali za maisha na utume wao hususan katika: malezi na majiundo ya awali na endelevu; matumizi bora zaidi ya mali, amana na utajiri wa Shirika waliokabidhiwa na uongozi Madhubuti katika miundombinu ya Shirika. Huu ni mwaliko wa kuendelea kumwilisha mshikamano katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kimwili na kiroho; mshikamano na watu wa Mungu katika ujumla wao, lakini zaidi mshikamano kati yao wenyewe kama wanashirika. Kiini cha mchakato wote huu wa uinjilishaji ni kuwasaidia watu kukutana na Kristo Yesu, anayewamegea huruma na upendo wake wa daima.

Muhimu kuzingatia uaminifu kwa karama na mashauri ya Kiinjili.
Muhimu kuzingatia uaminifu kwa karama na mashauri ya Kiinjili.

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 17 wa Shirika la Wamisionari wa Mariannhill (Congregatio Missionariorum de Mariannhill, C.M.M.), Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 20 Oktoba 2022 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu. Katika hotuba yake amekazia umuhimu wa kujikita kwa uaminifu katika karama ya Shirika; kwa kuendelea kumwilisha kauli mbiu “Mshikamano: Mnaitwa katika nia moja na shauri moja” katika maisha na utume wao kwa kumtegemea Roho Mtakatifu ili waweze kukua na kukomaa katika utakatifu na uaminifu wa huduma ya Injili. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Wamisionari hawa wataendelea kujikita zaidi katika mizizi ya karama ya mwanzilishi wa Shirika lao; kwa kuwa waaminifu kwa mashauri ya Kiinjili, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia; tayari kujenga ufalme wa Kristo Yesu unaosimikwa katika: Utakatifu, haki na amani. Kauli mbiu “Mshikamano: Mnaitwa katika nia moja na shauri moja” inakwenda hatua kwa hatua na maadhimisho ya Sinodi ya Kumi na Sita ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Lengo kuu la Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake.

Sinodi iwawezeshe watu wa Mungu kujenga utamaduni wa kusikiliza na kushiriki
Sinodi iwawezeshe watu wa Mungu kujenga utamaduni wa kusikiliza na kushiriki

Baba Mtakatifu Francisko anasema, hii ni safari ya Kanisa inayopania kuimarisha umoja, ushiriki na majitoleo ya kimisionari kwa wabatizwa wote, kwa njia ya mchakato wa mang’amuzi ya maisha ya kiroho, kwa watu wa Mungu kukutana, kusikiliza na kutafakari Neno la Mungu sanjari na kuendelea kujiweka wazi zaidi kwa maongozi ya Roho Mtakatifu. Jambo la msingi katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni ushiriki na uwajibikaji mkamilifu wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa kwa sasa na kwa siku za usoni. Tangu mwanzo kabisa mwa Shirika hili, kumekuwepo na lengo maalum la kuhamasisha na kukuza miito kutoka kwa watu wa Kanisa mahalia; kwa kujikita kikamilifu katika mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu kwa watu mahalia, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na ustawi wa wengi. Baba Mtakatifu anawataka wanashirika kuendelea kujikita katika: umoja na mshikamano kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kwa kujielekeza zaidi katika toba na wongofu wa shughuli za kichungaji hali inayopaswa kujionesha katika maisha na utume wao; malezi na majiundo ya awali na endelevu kwa makleri na waamini walei; kupanga na kutekeleza sera na mikakati ya maendeleo endelevu.

Wongofu wa kichungaji ni muhimu katika kumwilisha maazimio makuu ya Shirika
Wongofu wa kichungaji ni muhimu katika kumwilisha maazimio makuu ya Shirika

Kwa hakika mchakato wa maadhimisho ya Sinodi unalengo la kuwasaidia watu wa Mungu kutembea kwa pamoja, kusikilizana, lakini zaidi wanapaswa kumsikiliza Roho Mtakatifu, na hiki ndicho kinachopaswa kuwa ni kipaumbele cha maisha na utume wao. Wanahitaji maji ya Roho Mtakatifu, ili kulainisha nyoyo za waamini ambazo kwa hakika zimegeuka na kuwa sugu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 17 yatazaa matunda ya utakatifu wa maisha na uaminifu katika huduma ya Injili.

Mariannhill 2022
20 October 2022, 14:56