Tafuta

Tarehe 16 Oktoba ilichaguliwa kwa kuwa ni tarehe ambayo mwaka 1945 lilianzishwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO, lenye Makao yake Makuu mjini Roma, nchini Italia. Tarehe 16 Oktoba ilichaguliwa kwa kuwa ni tarehe ambayo mwaka 1945 lilianzishwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO, lenye Makao yake Makuu mjini Roma, nchini Italia.  

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Siku ya Chakula Duniani Oktoba 2022: Mshikamano wa Udugu

Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani anasema, mwaka 2022 FAO inaadhimisha kumbukizi ya Miaka 77 tangu kuanzishwa kwake, kwa lengo la kupambana na baa la njaa duniani, kutokana na madhara ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Hata leo hii, Jumuiya ya Kimataifa bado inashuhudia “Vita kuu ya Tatu ya Dunia” inayopiganwa vipande vipande., hatari sana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya Chakula Duniani ilianza kuadhimishwa kunako mwaka 1981 kufuatia azimio namba A/RES/35/70 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililopitishwa tarehe 5 mwezi Desemba mwaka 1980. Na ilichaguliwa tarehe 16 Oktoba kwa kuwa ni tarehe ambayo mwaka 1945 lilianzishwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO, lenye Makao yake Makuu mjini Roma, nchini Italia. Maadhimisho ya Siku 42 ya Chakula Duniani kwa Mwaka 2022 yananogeshwa na kauli mbiu “Hakuna wa kuachwa nyuma: kupitia uzalishaji bora, lishe bora, mazingira bora na maisha bora.” Kila mtu anapaswa kuwa ni sehemu ya kuchochea mabadiliko chanya ili dunia iweze kuwa na uhakika na usalama wa chakula kwa watu wote. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Dr. QU Dongyu, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO, anasema, mwaka 2022 FAO inaadhimisha kumbukizi ya Miaka 77 tangu kuanzishwa kwake, kwa lengo la kupambana na baa la njaa duniani, kutokana na madhara ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Kwa bahati mbaya sana, hata leo hii, Jumuiya ya Kimataifa bado inashuhudia “Vita kuu ya Tatu ya Dunia” inayopiganwa vipande vipande. Jumuiya ya Kimataifa itaweza kupambana na hatimaye, kutokomeza baa la njaa duniani, ikiwa kama watu watatambuana kwa vitendo kwamba, wote ni ndugu wamoja wanaounda familia kubwa ya binadamu, kumbe, wanategemeana na kukamilishana katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza katika maisha ya mwanadamu.

Vita sehemu mbalimbali za dunia vinakwamisha shughuli za kilimo
Vita sehemu mbalimbali za dunia vinakwamisha shughuli za kilimo

Baba Mtakatifu anaipongeza FAO kwa kuzindua Mpango Mkakati wa Mwaka 2022-2031. Lengo ni kufuta baa la njaa duniani ifikapo mwaka 2030 kama iliyokubaliwa kwenye Malengo ya Maendeleo Endelevu Ifikapo mwaka 2030. Umoja wa Mataifa unasema pili, ni kumaliza baa la njaa, kufikia usalama wa chakula na lishe bora na kueneza kilimo endelevu, huku familia zikipewa kipaumbele cha kwanza kama mahali ambapo kilimo kinaweza kuendelezwa na hivyo kuwa na matokeo chanya si tu kwa ajili ya sekta ya kilimo, bali kwa ajili ya binadamu wote pamoja na utunzaji bora wa mazingira. Katika mkutadha huu, familia inaweza kuwa ni nyenzo inayounganisha binadamu, kazi ya uumbaji na kilimo! Baa la umaskini duniani linachangiwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula na lishe bora. Kumbe, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na hivyo kusimikwa katika upendo kama kigezo muhimu sana cha ushirikiano wa Kimataifa.

Huu ni upendo unaokita mizizi yake katika mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa kukazia wongofu wa kiikolojia unaowahamasisha watu kuwa na shauku ya kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Laudato si, 216. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kumhakikishia Dr. QU Dongyu, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO, ushirikiano kutoka Vatican na kwa Kanisa Katoliki katika ujumla wake, katika mapambano dhidi ya baa la njaa na umaskini duniani, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza katika mchakato wa ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya kizazi hiki na kile kijacho, ili kuwalisha wenye njaa na kuwanywesha wenye kiu, sehemu mbalimbali za dunia.

Baa la njaa linasigina utu, heshima na haki msingi za binadamu
Baa la njaa linasigina utu, heshima na haki msingi za binadamu

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema maadhimisho ya mwaka 2022 yanafanyika wakati dunia inakabiliwa na janga kubwa la uhakika wa kupata chakula kutokana na ukweli kwamba, idadi ya watu wanaosiginwa na baa la njaa duniani imeongezeka maradufu kuanzia mwaka 2019. Zaidi ya watu milioni moja wanaishi katika mazingira ya kukumbwa na baa la njaa duniani. Watu bilioni 3 hawana uwezo wa kupata lishe bora na hivyo wako katika mazingira hatarishi ya kukumbwa na utapiamlo wa kutisha au unene wa kupindukia. Ukosefu wa uhakika na usalama wa chakula duniani ni matokeo ya maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; madhara ya mabadiliko ya tabianchi; ukosefu wa usawa na kwamba, vita kati ya Urussi na Ukraine vimepelekea ongezeko kubwa la bei ya chakula na pembejeo za kilimo pamoja na nishati.

Papa Francisko asema mshikamano wa udugu wa kibinadamu ni muhimu.
Papa Francisko asema mshikamano wa udugu wa kibinadamu ni muhimu.

Bado kuna matumizi mabaya ya chakula, kwani kuna watu wanakula hadi kufuru wakati kuna mwingine, wanalala huku wakisiginwa na baa la njaa. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anasema, hali hii inaweza kubadilishwa kwa kujenga na kudumisha ushirikiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Mbinu Mkakati na Ushauri wa FAO: Kupunguza upotevu na utupaji wa chakula ni muhimu katika dunia ambayo mamilioni ya watu wanalala njaa kila siku, limesema Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO.  Shirika hili linasisitiza kwamba “Tunapopunguza utupaji chakula, tunaheshimu kuwa chakula hakipatikani kirahisi kwa mamilioni ya watu ambao wanalala njaa kila uchao. Ni juu yetu kubadili tabia zetu ili kufanya upotevu wa chakula kutokuwa ndio mfumo wa maisha maisha.” FAO imeainisha hatua rahisi ambazo kila mmoja anaweza kuchukua ili kukithamini na kukienzi chakula: Tumia lishe bora na endelevu maisha yanaenda kwa kasi na kuandaa chakula chenye lishe inaweza kuwa changamoto, lakini milo yenye afya si lazima itumie muda mrefu kuandaliwa.

Siku ya Chakula Duniani 2022
16 October 2022, 15:54