Tafuta

Papa Francisko Mwezi Oktoba ni Mwezi wa Kuhamasisha Shughuli za Kimisionari na ni Mwezi wa Rozari Takatifu, muhtasari wa historia ya ukombozi. Papa Francisko Mwezi Oktoba ni Mwezi wa Kuhamasisha Shughuli za Kimisionari na ni Mwezi wa Rozari Takatifu, muhtasari wa historia ya ukombozi. 

Papa: Mwezi Oktoba Ni Mwezi Wa Kimisionari Na Rozari Takatifu!

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 96 ya Kimisionari Ulimwenguni, Jumapili tarehe 24 Oktoba 2022 unanogeshwa na kauli mbiu: “Mtakuwa mashahidi wangu” (Mdo 1:8). 1. Baba Mtakatifu anasema "Mtakuwa mashahidi wangu" ni wito na mwaliko wa kila mkristo kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 5 Oktoba 2022 amewakumbusha waamini kwamba, Mama Kanisa katika kipindi cha Mwezi wa Oktoba anapenda kuwahamasisha waamini kushiriki kikamilifu katika shughuli za kimisionari pamoja na kuchangia kwa hali na mali mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Waamini wasali zaidi, wajifunze kudumisha ukimya ndani mwao, ili kukutana na Kristo Yesu, anayewakirimia waja wake njia na mbinu za kuwa waaminifu katika wito wao kama mitume wamisionari. Huu ni mwamko na ushuhuda wa kimisionari kama kielelezo cha imani tendaji na mapendo kamili kwa Mungu na jirani zao. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 96 ya Kimisionari Ulimwenguni, Jumapili tarehe 23 Oktoba 2022 unanogeshwa na kauli mbiu: “Mtakuwa mashahidi wangu” (Mdo 1:8). 1. Baba Mtakatifu anasema "Mtakuwa mashahidi wangu" ni wito na mwaliko wa kila mkristo kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu. Hili ni wazo kuu, moyo wa mafundisho ya Yesu kwa wafuasi wake kwa kurejea katika utume wao. Wafuasi wanapaswa kuwa mashuhuda wa KristoYesu, kwa kutegemea neema ya Roho Mtakatifu watakayempokea. Baba Mtakatifu anasema "Mpaka miisho ya dunia" ni dhana inayoonesha umuhimu wa udumifu wa utume wa uinjilishaji wa ulimwengu wote. Anawahimiza wafuasi wawe mashahidi wake, Bwana Mfufuka anawajulisha pia mahali wanapotumwa: “… Katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.” (Mdo .1.8). Hapa tabia ya kiulimwengu ya utume wa wafuasi inajitokeza kwa uwazi sana.

Mwezi Oktoba: Ushuhuda wa kimisionari
Mwezi Oktoba: Ushuhuda wa kimisionari

Baba Mtakatifu anakaza kusema “Mtapokea nguvu kutoka kwa Roho Mtakatifu" huu ni mwaliko wa kujiruhusu kila wakati kuimarishwa na kuongozwa na Roho Mtakatifu. Kristo Mfufuka alipowaagiza wafuasi kuwa mashahidi, aliwaahidi pia neema zilizohitajika kwa ajili ya jukumu kubwa: “Mtapokea nguvu za Roho Mtakatifu nanyi mtakuwa mashahidi wangu” (Mdo 1:8). Kadiri ya simulizi la Matendo ya Mitume, ilikuwa kwa hakika baada ya kushuka Roho Mtakatifu juu ya wafuasi ndipo tendo la kwanza la kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufuka lilitokea. Utangazaji huo wa “Ki-kerygma”, Hotuba ya kimisionari ya Mtakatifu Petro kwa wakazi wa Yerusalemu – ilizindua zama mpya ambapo wafuasi wa Yesu waliinjilisha ulimwengu. Hali mwanzoni walikuwa hakika dhaifu, wenye hofu na kujitenga ndani yao, Roho Mtakatifu aliwapa nguvu, ujasiri na hekima ya kumshuhudia Kristo mbele ya watu wote. Waamini wanakumbushwa kwamba, utakatifu ni wito na mwaliko kwa watu wote wa Mungu kuchuchumilia na kuambata ukamilifu wa maisha kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu, kwa kujivika moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu, daima wakijitahidi kumwilisha Matunda ya Roho Mtakatifu katika uhalisia wa maisha yao.

Mwezi Oktoba: Maisha ya Kiroho na Kiutu
Mwezi Oktoba: Maisha ya Kiroho na Kiutu

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Rozari Takatifu ni muhtasari wa huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Ni njia muafaka kabisa ya kutafakari maisha na utume wa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai, ili kumfahamu, kumpenda, kumfuasa na kumtumikia kwa njia ya upendo kwa Mungu na jirani wenye shida na mahangaiko mbalimbali wanaokumbukwa katika Sala ya Rozari Takatifu. Waamini wanahamasishwa kuendelea kusali Rozari Takatifu, muhtasari wa historia nzima ya kazi ya ukombozi; maisha na utume wa Kristo Yesu. Bikira Maria alipowatokea Watoto watatu wa Fatima yaani Francis, Yacinta na Lucia aliwaagiza kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya toba, wongofu wa ndani na amani duniani. Mwezi Oktoba, umetengwa rasmi na Mama Kanisa kwa ajili ya Ibada ya Rozari Takatifu. Hivyo basi, anawaalika waamini kuendelea kuwa waaminifu katika Mapokeo haya kwa kujitahidi kusali Rozari Takatifu, kama mtu binafsi, jumuiya, lakini inapendeza zaidi, ikiwa kama wanafamilia watasali na kutafakari kwa pamoja historia ya kazi ya ukombozi iliyotekelezwa kwa njia ya Kristo Yesu. Kwa njia ya Rozari Takatifu, waamini wanamshirikisha Bikira Maria furaha, machungu, mwanga na matumaini yao.

Wakati huo huo, Askofu mkuu Giampietro Dal Toso, Katibu Mwambata, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Rais wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa anasema, ushuhuda unasindikizwa na kumbukumbu hai. Ni wakati muafaka wa kupyaisha ahadi za Ubatizo, tayari kujisadaka kwa ajili ya Injili ya Kristo. Hakuna mtu yeyote anayetengwa na huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake! Takwimu zinaonesha kwamba, kuna kurugenzi 118 za Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari zinazotekeleza dhamana na utume wake katika mataifa 140 na hivyo kuunda mtandao wa mashirika haya kimataifa. Huduma hii inaweza kuimarishwa na kuendelezwa zaidi kwa kuzingatia mambo makuu matatu: Sala, Ushuhuda na Upendo unaomwilishwa katika huduma. Changamoto na mwaliko kwa waamini kushirikishana imani yao kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa kuondokana na uchoyo pamoja na ubinafsi.

Mwezi Oktoba
05 October 2022, 15:00