Papa Francisko Maisha na Utume wa Watawa Uwe wa Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume ni kipindi maalum cha watawa kukutana katika: Sala, tafakari na mang’amuzi ya kina mintarafu amana na utajiri wa mashirika na wanashirika wenyewe. Ni wakati muafaka kwa wanashirika kufanya upembuzi yakinifu kuhusu maisha na utume wa mashirika yao kwa kuangalia changamoto, matatizo na fursa zilizopo kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni wakati muafaka wa kusoma alama za nyakati na kuangalia wapi ambapo Roho Mtakatifu anawataka kwenda baada ya mikutano yao mikuu. Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba, watawa wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili kwa kujikita katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu kama chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Mama Kanisa anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa watu wa Mungu wanaoteseka kutokana na vita sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, Kanisa linatambua na kuthamini ushuhuda wa maisha na utume wao sehemu mbalimbali za dunia. Kumbe, maadhimisho ya Mkutano mkuu wa Shirika ni wakati muafaka wa kupyaisha utume wa Shirika mintarafu karama ya Shirika kwa kusoma alama za nyakati, kwa kuboresha maisha ya kiroho ya mtawa mmoja mmoja na Shirika katika ujumla wake. Shirika la Watawa wa Mtakatifu Brigida, lilianzishwa kunako Karne ya 18 kwa juhudi za Mwenyeheri Mama Elisabetta Hesselblad. Lengo kuu ni kufufua umoja wa Wakristo wote kwa kuzingatia Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ili wote wawe wamoja.
Kwa upande mwingine kuna Shirika la Masista wa Wamisionari wa Comboni, S.M.C., lilianzishwa tarehe Mosi Januari 1872 na Mtakatifu Daniele Comboni. Kama sehemu ya kumbukizi la Miaka 150 tangu kuanzishwa kwao, Mwezi Oktoba 2022 wameadhimisha Mkutano mkuu wa 21, kielelezo cha neema ya Mungu inayotenda kazi ndani mwao, ili kuwaletea mabadiliko yanayowasukuma kwenda pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, kama Mitume wamisionari. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 22 Oktoba 2022 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa mikutano mikuu ya Mashirika haya mawili. Katika hotuba yake, amewataka watawa hawa kutoa kipaumbele cha uwepo wa Mungu katika maisha na utume wao. Wajenge na kudumisha umoja, ushiriki na utume kama sehemu ya utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Ni wakati wa kusikilizana kwa kina, kujifunza na kuthamini karama za wanashirika wao. Ni mwaliko kwa kusaidiana na hatimaye, kufanya maamuzi kwa pamoja kama kielelezo cha ushuhuda wa Sinodi inayomwilishwa katika vitendo kama sehemu ya utendaji wa Kanisa na Watu wa Mungu katika ujumla wao. Huu ni mwaliko wa kuondoa vikwazo vinavyowekwa katika Ukuhani wa jumla wa waamini na juu ya ufahamu wa imani ya watu wa Mungu “Sensus fidei” hususan kuhusu utambulisho wao kama wahudumu wa Habari Njema ya Wokovu.
Ni furaha na shangwe kubwa kupata ndugu wanaoshiriki katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Watawa washiriki kikamilifu katika mchakato wa utekelezaji wa maadhimisho ya Sinodi katika ngazi mbalimbali. Watawa wajenge na kudumisha moyo wa Sala na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kwa sababu Sinodi inasimikwa pia katika Sala na Tafakari ya Kina ambayo baadaye inamwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Watawa wawe na nidhamu katika kutumia ndimi zao, kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu na wala si kwa ajili ya kupika majungu pamoja na kuwachafulia wengine sifa zao njema. Wawe na ujasiri wa kumkiliza Roho Mtakatifu katika maisha na utume wao, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kupambana na umaskini, kwa kuwapatia maskini kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wao. Unyenyekevu iwe ni fadhila na utambulisho wao katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa, kwa kuondokana na uchoyo na ubinafsi. Sala ipewe msukumo wa pekee katika maisha na utume wao, kielelezo makini cha uwepo na ukaribu wa Mungu kati yao. Waangalie ukweli wa mambo kwa jicho la huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.