Tafuta

Kumbukizi la Miaka 60 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican sanjari na mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa. Kumbukizi la Miaka 60 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican sanjari na mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa. 

Miaka 60 ya Mtaguso Mkuu wa II wa Vatican na Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi: Ushiriki Wa Walei

Ni kiongozi aliyethubutu kuitisha Mtaguo Mkuu wa Pili wa Vatican ili kulipyaisha Kanisa la Kristo na kuendelea kusoma alama za nyakati. Mama Kanisa anamkumbuka kila mwaka ifikapo tarehe 11 Oktoba, siku ambapo Kanisa lilizindua rasmi Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Mwaka 2022 ni kumbukizi la Miaka 60 tangu kufunguliwa rasmi kwa maadhimisho ya Mtaguso.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Yohane wa XXIII Alibahatika kuliongoza Kanisa Katoliki kuanzia tarehe 28 Oktoba 1958 hadi kifo chake tarehe 3 Juni 1963 na hivyo kuwa ni Papa wa 261 kuliongoza Kanisa Katoliki. Alikuwa ni mtu mwema na mwenye mvuto na faraja kwa watu weng.i Alitangazwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Mwenyeheri tarehe 3 Septemba 2000 wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2000 ya Ukristo. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 27 Aprili 2014 akamtangaza kuwa ni Mtakatifu. Ni kiongozi aliyethubutu kuitisha Mtaguo Mkuu wa Pili wa Vatican kuanzia mwaka 1962 hadi mwaka 1965, ili kulipyaisha Kanisa la Kristo na kuendelea kusoma alama za nyakati. Mama Kanisa anamkumbuka kila mwaka ifikapo tarehe 11 Oktoba, siku ambapo Kanisa lilizindua rasmi Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Maadhimisho ya Mwaka 2022 yanabeba amana na uzito wa hali ya juu kwani Mama Kanisa anafanya kumbukizi la Miaka 60 tangu Mtakatifu Yohane XXIII alipofungua rasmi Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne tarehe 11 Oktoba 2022 majira ya saa 11: 00 Jioni kwa Saa za Ulaya anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Miaka 60 tangu kuadhimishwa kwa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi
Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi

Baba Mtakatifu Francisko katika dibaji alioandika kwenye Kitabu kilichotungwa na Ettore Malnati na Marco Roncalli: “Giovanni XXIII, Il Vatican II Concilio Per Mondo, Boliz Edition” anasema, Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ulipaniwa na Mtakatifu Yohane XXIII na kuhakikisha kwamba, unaadhimishwa, kama tukio la kihistoria kwa maisha na utume wa Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Huu ni Mtaguso endelevu ambao bado haujafahamika na wengi; kiasi cha kumwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa, changamoto kwa Mama Kanisa kusimama kidete, ili kuhakikisha kwamba, maamuzi ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican yanatekelezwa kikamilifu. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ni mchakato ambao umeliwezesha Kanisa kupyaisha maisha na utume wake, changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu nyakati hizi, kujizatiti kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalosimikwa katika: Umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa kwa kukazia utamaduni wa kusikiliza, ushiriki mkamilifu wa watu wateule wa Mungu kwa kumsikiliza kikamilifu Roho Mtakatifu, ili kusoma alama za nyakati. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na mambo mengine umekazia kuhusu: Taifa jipya la Mungu, Watu wa Mungu; Ukuhani wa watu wote; Hisia ya imani na karama katika taifa la Mungu “Sensus fidei.”

Walei wanahimizwa kuyatakatifuza malimwengu kwa ushuhuda
Walei wanahimizwa kuyatakatifuza malimwengu kwa ushuhuda

Kanisa si mali ya wateule wachache, yaani Makleri na Watawa, bali kila Mbatizwa, anayo dhamana na jukumu la kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili ndicho kiini cha Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Baba Mtakatifu anatambua na kukiri kwamba, wafuasi wa Kristo Yesu ni wadhambi, lakini wamepewa dhamana ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Katika huruma na upendo wake wa daima, Kristo Yesu anaendelea kuwaonjesha huruma na upendo wake, kwa kuwasamehe dhambi zao; changamoto na mwaliko wa kuendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni utambuzi wa uwepo endelevu na angavu wa Kristo Yesu kati pamoja na waja wake. Huu ni wito wa kushikamana na wale waliovunjika na kupondeka moyo, ili waweze kuonja tena ndani mwao: huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kwa njia ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Kanisa linahamasishwa kusoma alama za nyakati, ili kufikisha Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati hizi, jambo la msingi ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kiini cha Uinjilishaji mpya! Miaka 60 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican imekuwa na matatizo, changamoto na fursa zake. Mama Kanisa daima amepandikiza mbegu ya imani,

Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi
Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi

matumaini na mapendo kwa uvumilivu na udumifu mkubwa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni mwaliko wa kurejea tena na tena katika historia ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ili kuweza kuishi kikamilifu mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, likiwa na moyo wazi na huru, tayari kukutana na huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, ili kuonesha ukaribu kwa waja wake. Huu ni mwaliko wa kupiga moyo konde na kujenga ujasiri wa kiimani, bila kukata wala kukatishwa tamaa, kwa kutoa nafasi ya pekee kwa uwepo wa Mungu katika maisha ya watu. Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu inasema, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa kuhusu umuhimu wa kumwilisha matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kukazia watu wote wa Mungu kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Hiki ni kiini cha “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa.” Baba Mtakatifu anakazia ukuhani wa waamini wote; umuhimu wa waamini kushiriki kikamilifu Sakramenti za Kanisa; umuhimu wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni; ari na mwamko wa kimisionari pamoja na umuhimu wa waamini walei kuwa ni chachu ya uinjilishaji mpya na utakatifu kwa njia ya ushuhuda wa maisha, kama kielelezo makini cha imani tendaji!

Uinjilishaji unakijika katika ushuhuda wa maisha.
Uinjilishaji unakijika katika ushuhuda wa maisha.

Umoja, upendo na mshikamano wa dhati ni mambo msingi katika utangazaji na ushuhuda wa Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inazingatia mambo yafuatayo: Ufahamu wa kina wa Neno la Mungu; umuhimu wa toba na wongofu wa ndani; ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Haya ni mambo msingi katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya katika ulimwengu mamboleo. Dhana ya Sinodi ni wazo lililotolewa na Mtakatifu Paulo VI, linaloihusisha Familia ya Mungu katika ujumla wake. Sinodi za Maaskofu zimekuwa ni chombo madhubuti cha uinjilishaji na upyaishaji wa maisha na utume wa Kanisa; kwa kulisaidia Kanisa kuendelea kudumu katika uaminifu kwa Maandiko Matakatifu; kupyaisha mafundisho ya Kanisa pamoja na kudumisha mchakato wa kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili miongoni mwa watu wa Mataifa. Rej. Evangelii gaudium, n. 69. Baba Mtakatifu Francisko katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi anakazia mambo makuu matatu: Umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa. Haya ni maneno yanayopata chimbuko lake katika Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, kielelezo cha imani ya Kanisa katika Ubatizo na Fumbo la Utatu Mtakatifu. Huu ni umoja katika tofauti zake msingi zinazojionesha katika utume na karama kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu na kama kielelezo cha furaha ya ushuhuda wa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu.

Dibaji, Mtaguso mkuu
10 October 2022, 15:28