Tafuta

Mwaka 2022 Uratibu wa Vyama vya Mawasiliano Italia, “Coordinamento delle Associazioni per la Comunicazione (COPERCOM)” unaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwake. Mwaka 2022 Uratibu wa Vyama vya Mawasiliano Italia, “Coordinamento delle Associazioni per la Comunicazione (COPERCOM)” unaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwake.   (Vatican Media)

Jubilei ya Miaka 25 ya COPERCOM: Umuhimu wa Mawasiliano: Kukutana, Kusikiliza na Neno

Papa amekazia: Umuhimu wa Taasisi hii ya Uratibu, Mabadiliko katika mchakato wa mawasiliano ya jamii; haja yawatu kukutana, kusikilizana na Neno na hatimaye, ni mchakato wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu ambayo yamegawanywa sasa katika: Awamu ya kwanza ni kuanzia tarehe 1-29 Oktoba 2023 na Awamu ya Pili ni Mwezi Oktoba 2024. Neno!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Uratibu wa Vyama vya Mawasiliano Italia, “Coordinamento delle Associazioni per la Comunicazione (COPERCOM)” uliasisiwa kunako mwaka 1998 ili kusimamia haki msingi za binadamu sanjari na tunu msingi za maisha ya kifamilia katika ulimwengu wa mawasiliano ya jamii. Uratibu huu, unavijumuisha vyama 29 vya mawasiliano ya jamii, vyenye jumla ya wanachama zaidi ya milioni mbili. Mwaka 2022 Uratibu wa Vyama vya Mawasiliano Italia, “Coordinamento delle Associazioni per la Comunicazione (COPERCOM)” unaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwake. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei hii, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 31 Oktoba 2022 amekutana na kuzungumza na wanachama wa COPERCOM, wanaosimamiwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia kuhusu: Umuhimu wa Taasisi hii ya Uratibu, Mabadiliko katika mchakato wa mawasiliano ya jamii; umuhimu wa watu kukutana, kusikilizana na Neno na hatimaye, ni mchakato wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu ambayo yamegawanywa sasa katika awamu kuu mbili. Awamu ya kwanza ni kuanzia tarehe 1-29 Oktoba 2023 na Awamu ya Pili ni Mwezi Oktoba 2024. Lengo ni kuendelea kufanya mang’amuzi ya kina kuhusu dhana ya Sinodi kama chombo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa Mataifa.

Mawasiliano: Kukutana Kusikiliza na Neno
Mawasiliano: Kukutana Kusikiliza na Neno

Baba Mtakatifu anawapongeza Waratibu wa mtandao wa mawasiliano ya jamii chini Italia nchini ya usimamizi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI. Ni wakati wa kufanya upembuzi yakinifu kuhusu mchakato wa mabadiliko katika mawasiliano ya jamii, ili hatimaye, kutengeneza sera, mikakati, dira ya malengo ya muda mfupi na mrefu. Taasisi hii iliyopewa dhamana ya kuratibu inapania pamoja na mambo mengine kuhakikisha kwamba inasaidia kuboresha mawasiliano ya jamii katika uhalisia wa maisha ya watu. Hili ni jukumu linalohitaji uvumilivvu, dira, nia ya pamoja pamoja na kuthamini vyama mbalimbali vinavyoratibiwa chini ya COPERCOM, ili karama na mapaji ya wanachama yaweze kuzaa matunda yanayokusudiwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, lakini zaidi kwa ajili ya huduma kwa Kanisa nchini Italia. Hii ni changamoto ya kuyaangalia ya mbeleni kwa matumaini, tayari kuweza kuthubutu kukumbatia njia mpya, kwa kutumia karama na uzoefu wao katika medani za mawasiliano ya jamii. Baba Mtakatifu anasema, mwanadamu anaishi katika kipindi chenye mabadiliko makubwa yanayohitaji kuwa na mwelekeo mpya wa jinsi ya kujenga na kudumisha mahusiano; kufafanua na kutoa mawazo pamoja na kujenga mahusiano na mafungamano kwa marika mbalimbali ndani ya jamii; kwa kuzingatia fursa, matatizo na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika tasnia ya mawasiliano ya jamii.

Mawasiliano ya jamii ni muhimu sana katika kukuza mahusiano na mshikamano
Mawasiliano ya jamii ni muhimu sana katika kukuza mahusiano na mshikamano

Kuna mabadiliko makubwa ya maendeleo ya sayansi na teknolojia; mambo yanayohitaji elimu makini pamoja na habari mahususi. Hii ni changamoto ya kufanya upembuzi yakinifu ili kuweza kubaini mahusiano na mafungamano wanayoweza kuanzisha na vijana wa kizazi kipya; kwa kufanya wongofu na kupokea mabadiliko kwa mshangao mkubwa, bila ya kutumbukia katika mazoea na tabia ya kujitafuta. Katika mawasiliano, Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa watu kukutana, kusikilizana na Neno. Nia ni kujiweka wazi kwa wengine, kwa kufungua akili na nyoyo zao. Lengo ni kufahamiana, kwa njia ya kusikilizana. Utamaduni wa kusikilizana unajikita tabia ya ukimya na hali ya kusikiliza kwa makini; kwa kuheshimiana kwa kutambua kwamba, kila mwanadamu ni fumbo, linalohitaji kufumbuliwa kwa njia ya mazungumzo. Kumbe, baada ya kusikiliza kwa makini, hapo Neno na ushuhuda unafuatia kama anavyo sema Mwinjili Yohane “Lile lililokuwako tangu mwanzo, tulilolisikia, tuliloliona kwa macho yetu, tulilolitazama, na mikono yetu ikalipapasa, kwa habari ya Neno la uzima; (na uzima huo ulidhihirika, nasi tumeona, tena twashuhudia, na kuwahubiri ninyi ule uzima wa milele, uliokuwa kwa Baba, ukadhihirika kwetu); hilo tuliloliona na kulisikia, twawahubiri na ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi: na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo. “1 Yn 1:1-3.

COPERCOM inaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya uwepo na utume wake
COPERCOM inaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya uwepo na utume wake

Neno linalobubujika kutoka katika kimya na utamaduni wa kusikiliza linaweza kugeuka na kuwa ni Habari Njema na huo unakuwa ni mwanzo wa mawasiliano yanayojenga ushirika. Kumbe, kuna haja ya kujenga utamaduni wa watu kukutana, kusikilizana na hatimaye kuzungumzana, binadamu na utu wake, akipewa kipaumbele cha kwanza na kama sehemu ya mbinu mkakati wa kupambana na dalili za kinzani na mipasuko ya kijamii inayoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo. Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu ambayo yamegawanywa sasa katika awamu kuu mbili. Awamu ya kwanza ni kuanzia tarehe 1-29 Oktoba 2023 na Awamu ya Pili ni Mwezi Oktoba 2024. Nia ni kuendelea kufanya mang’amuzi ya kina kuhusu dhana ya Sinodi kama chombo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa Mataifa. Lengo ni kudumisha ushirika wa Kanisa kadiri ya mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, uliozinduliwa miaka 60 iliyopita. Huu ni mwaliko kwa COPERCOM, kuhakikisha kwamba, wanachangia mawazo yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa nchini Italia. Kama Jumuiya ya waamini, wao pia ni chombo cha matumaini yanayosimikwa katika udugu wa kibinadamu. Kumbe, wanaitwa na kuhamasishwa kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa ushirika. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amewaweka chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Francisko wa Sale: Mlinzi na Mwombezi wa waandishi wa habari, watunzi na wanafasihi, magazeti ya Kikatoliki pamoja na Mwenyeheri Carlo Acutis, wanaoonesha umuhimu wa kujikita katika kipaji cha ubunifu, ujuzi na maarifa kama sehemu ya utekelezaji wa dhamana na utume katika ulimwengu wa kidigitali.

Papa Copercom
31 October 2022, 15:29