Tafuta

Siku ya Kutokomeza Silaha za Nyuklia Duniani tarehe 26 Septemba 2022 : Silaha za nyuklia ni tishio kwa usalama, amani, ustawi na maendeleo fungamani ya mwanadamu. Siku ya Kutokomeza Silaha za Nyuklia Duniani tarehe 26 Septemba 2022 : Silaha za nyuklia ni tishio kwa usalama, amani, ustawi na maendeleo fungamani ya mwanadamu. 

Vita kati ya Urussi na Ukraine ni Hatari Kwa Amani na Usalama wa Jumuiya ya Kimataifa

Kardinali Pietro Parolin anasema: Vita kati ya Urussi na Ukraine ni hatari sana kwa: usalama, amani, mshikamano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa. Hii inatokana na ukweli kwamba, Mataifa yanaendelea kutengeneza na kulimbikiza silaha za nyuklia. Kuna haja ya kuendelea kuaminiana, kuheshimiana, tayari kusimama kidete kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kutokomeza Silaha za Nyuklia Duniani tarehe 26 Septemba 2022 ametamka kwa mara nyingine tena kwamba, matumizi ya nguvu za atomic kwa ajili ya vita, kwa wakati huu, kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya mwanadamu ni kwenda kinyume cha utu na heshima ya binadamu na tishio kubwa kwa mustakabali wa mazingira nyumba ya wote. #Peace #NuclearDisarmament #TimeofCreation.” Maadhimisho ya Siku ya Kutokomeza Silaha za Nyuklia Duniani ni changamoto iliyovaliwa njuga na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1946 kwa kuanzisha Tume ya Nguvu ya Atomic, iliyofutwa kunako mwaka 1952 na hatimaye, kukaanzishwa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomic, IAEA.

Siku ya kutokomeza silaha za nyuklia duniani kwa mwaka 2022
Siku ya kutokomeza silaha za nyuklia duniani kwa mwaka 2022

Umoja wa Mataifa umeendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika mchakato wa kutokomeza silaha za nyuklia duniani. Hadi leo hii, kuna zaidi ya silaha 14,000 za nyuklia sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, majadiliano kuhusu kutokomeza silaha za nyuklia bado yanaendelea ingawa yanakabiliana na changamoto kubwa. Katika enzi ya "vitisho vya nyuklia" Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika hotuba yake kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Jumatatu tarehe 26 Septemba 2022 ameonesha kwamba, vita kati ya Urussi na Ukraine ni hatari sana kwa: usalama, amani, mshikamano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa. Hii inatokana na ukweli kwamba, Mataifa yanaendelea kutengeneza na kulimbikiza silaha za nyuklia. Kuna haja ya ulimwengu kuondokana na hofu ya silaha za nyuklia na kwamba, wamiliki wa silaha hizi za maangamizi, watakuwa mstari wa mbele kuchangia utekelezaji wake, kwa Mataifa kuendelea kuaminiana na kuheshimiana, tayari kusimama kidete kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Vita kati ya Urussi na Ukraine ni hatari kwa mustakabali wa Taifa
Vita kati ya Urussi na Ukraine ni hatari kwa mustakabali wa Taifa

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, Jumatatu tarehe 26 Septemba 2022, amezitaka Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuondokana na tishio la maafa ya kimataifa na hivyo kuwataka wajikite katika mchakato wa ujenzi wa amani duniani. Silaha za kinyuklia zina uwezo mkubwa wa kusababisha maangamizi makubwa duniani, na ni tishio la usalama na amani duniani. Kwa kuondolewa kwake, hii ingeweza kuwa ni zawadi kubwa kwa wakati huu na kwa vizazi vijavyo. Vita Baridi ilikuwa na madhara makubwa kwa wat una maisha yao. Hata baada ya kuvunjwa kwa Ukuta wa Berlin, bado mwana damu anaendelea kutishiwa kwa uwepo wa silaha za kinyuklia. Huu ni wakati wa kumaliza kabisa vitisho na uhasama, ili kujenga msingi wa haki, amani na utulivu. Hakuna mtu anayeweza kujidai kwamba, anaweza kushinda vita ya nyuklia na amani iwe ni agenda inayopewa kipaumbele cha kwanza na Jumuiya ya Kimataifa, kwa ajili ya mustabakali wa ustawi, maendeleo na mafao mapana zaidi ya Jumuiya ya Kimataifa.

Parolin Silaha za Nyuklia

 

 

27 September 2022, 15:32