Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 26 Septemba 2022 amekutana na kuzungumza na Masista Watersiari Wakapuchini wa Familia Takatifu. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 26 Septemba 2022 amekutana na kuzungumza na Masista Watersiari Wakapuchini wa Familia Takatifu. 

Papa Watawa Jengeni Utamaduni wa Usikivu Unaosimikwa Katika Ukimya, Sala na Huduma

Mkutano mku unanogeshwa na kauli mbiu: Usikivu wa unyenyekevu na Sinodi. Baba Mtakatifu amekazia ujenzi wa usikivu unaosimikwa katika ukimya wa ndani, kielelezo cha sala makini, inayowawezesha kujitenga na malimwengu kwa kutoa kipaumbele kwa mambo mazito katika maisha. Watawa wawe ni manabii wa utamaduni wa kusikiliza, ili kukutana na Mungu katika undani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Masista Watersiari Wakapuchini wa Familia Takatifu ni watawa Wafranciskani wanaounda Shirika la Kipapa lililoanzisha na Luis Amigo (1854-1934) Ufupisho wake ni H.T.C.F.S., kwa Kihispania ni: Hermanas Terciarias Capuchinas de la Sagrada Familia). Masista walianza kuishi kijumuia mwaka 1878 kwenye mahali patakatifu pa “Nuestra Señora de Montiel” huko Benaguacil, Hispania Mashariki. Walitambuliwa kisheria katika ngazi ya Jimbo tarehe 11 Mei 1885 kwa kupata kibali kutoka kwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Valencia, nchini Hispania na wawata wa kwanza wakaweka nadhiri zao za kwanza kabisa ndani ya Shirika. Padre Luis Amigo aliwaandikia Kanuni za maisha ya kitawa na hususan Utawa wa Tatu wa Mtakatifu Francisko pamoja na Katiba ya Shirika, mwongozo mama wa maisha na utume wa watawa hawa. Ni watawa waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa na hasa wagonjwa wa Kipindupindu na hivyo kupelekea watawa wanne kuambukizwa na hatimaye kufariki dunia. Tarehe 6 Machi 1902 Papa Leo XIII aliridhia kuanzishwa kwa Shirika hili na hivyo kuhusianishwa na lile la Mwanzilishi wa Shirika la Ndugu Wadogo Wakapuchini hapo tarehe 15 Septemba 1905. Hili ni Shirika ambalo limeenea katika nchi thelathini na tatu duniani kote.

Mkutano mkuu wa 23: Usikivu, Unyenyekevu na Sinodi
Mkutano mkuu wa 23: Usikivu, Unyenyekevu na Sinodi

Kwa upande wa Bara la Afrika, watawa hawa wanafanya utume wao nchini Benin, DRC, Guinea ya Ikweta, Tanzania na hasa katika Jimbo kuu la Dar es Salaam na Jimbo Katoliki la Morogoro, kule Msolwa, Wilayani Kilosa kwa msisitizo. Ni watawa wanaojisadaka katika huduma ya elimu bora na makini: kiroho na kimwili; Malezi na makuzi ya watoto na vijana wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Wanatoa pia huduma katika sekta ya afya, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa wazee na walemavu. Wamebobea katika Katekesi, Uinjilishaji pamoja na Utume wa familia, ili kuwajengea uwezo wa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume ni kipindi maalum cha watawa kukutana katika: Sala, tafakari na mang’amuzi ya kina mintarafu amana na utajiri wa mashirika na wanashirika wenyewe. Ni wakati muafaka kwa wanashirika kufanya upembuzi yakinifu kuhusu maisha na utume wa mashirika yao kwa kuangalia changamoto, matatizo na fursa zilizopo kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Watawa wajifunze kutemba kwa mshikamano wa upendo
Watawa wajifunze kutemba kwa mshikamano wa upendo

Huu ni wakati muafaka wa kusoma alama za nyakati na kuangalia wapi ambapo Roho Mtakatifu anawataka kwenda baada ya mikutano yao mikuu. Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba, watawa wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili kwa kujikita katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu kama chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 26 Septemba 2022 amekutana na kuzungumza na Masista Watersiari Wakapuchini wa Familia Takatifu, kama sehemu ya maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 23 tangu Shirika hili lilipoanzishwa. Mkutano huu unanogeshwa na kauli mbiu: Usikivu wa unyenyekevu na Sinodi. Baba Mtakatifu amekazia ujenzi wa usikivu unaosimikwa katika ukimya wa ndani, kielelezo cha sala makini, inayowawezesha kujitenga walau kidogo na malimwengu kwa kutoa kipaumbele kwa mambo makuu na mazito katika maisha. Watawa wawe ni manabii wa utamaduni wa kusikiliza, ili kukutana na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yao; tayari kutembea kwa pamoja katika umoja, ushiriki na maisha ya Kitume na kuendelea kutegemea maongozi ya Roho Mtakatifu.

Roho Mtakatifu awasaidie kujenga umoja na mshikamano
Roho Mtakatifu awasaidie kujenga umoja na mshikamano

Ukimya wa ndani uwe ni msingi wa malezi na majiundo makini katika maisha na utume wa kitawa. Baba Mtakatifu anawataka watawa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza kwa makini, kwa kujijengea ukimya wa ndani unaobubujika na kujikita katika maisha ya sala. Watawa wawe na moyo mkuu wa kuweza kusikiliza kilio chao cha ndani kinachokita mizizi yake katika kimya kikuu, tayari kutoa majibu muafaka pale yanapohitajika kutolewa. Watawa wajijengee uwezo wa kuratibu vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii, ili kujiundia kimya kikuu. Watawa wawe ni Manabii wa Ukimya, ili kuondokana na uwezekano wa kumezwa na malimwengu. Waswahili husema "Miruzi mingi humpoteza mbwa". Amani na utulivu wa ndani ni fadhila na wala si mambo ya kulazimishana. Watawa wajiepushe na “kishawishi cha kupiga majungu” kwani majungu si mtaji, ungekuwa mtaji, hapana shaka kwamba, wengi wangekuwa wametajirika. Unabii wa Ukimya unaofumbatwa katika unyenyekevu ambao ni silaha madhubuti dhidi ya kiburi, ambacho kimsingi ni kaburi la utu na heshima ya binadamu.

Watawa wajitahidi kutembea pamoja kama wanasinodi
Watawa wajitahidi kutembea pamoja kama wanasinodi

Unabii wa ukimya uwasaidie kusikiliza sauti ya Mungu inayozungumza nao kutoka katika undani wa maisha yao, yaani dhamiri nyofu, tayari kuwapokea watu wenye mawazo tofauti. Kimya kikuu ni jukwaa la watawa kuweza kukutana na kuzungumza na Mwenyezi Mungu, tayari kutembea kwa pamoja kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Huu ni mchakato wa kufanya Njia ya Msalaba, kutembea katika ufukara na kujikita zaidi katika huduma kwa Mungu na jirani. Iwe ni fursa ya kutafakari mateso ya Kristo Yesu kama alivyokuwa anafanya Muasisi wa Shirika, Luis Amigo aliyejinyenyekeza, kiasi cha kuwa ni mdogo, ili kupata amani na utulivu wa ndani; ustawi na maendeleo ya jumuiya yake. Roho Mtakatifu ni chanzo cha amani na utulivu wa kijumuiya. Kimya kikuu, kiwawezeshe watawa kugundua ukweli, ili kupyaisha maisha na utume wao; tayari kufuata na kuiga mifano bora. Hii ni fursa ya kuweza kujikita zaidi katika malezi na majiundo ya ndani; katika masomo na tafakari ya maisha inayosimikwa katika sala. Kwa njia hii, watawa wanaweza kuendelea kujifunza kutoka katika shule ya Injili ambayo kimsingi ni safari ya wokovu.

Papa Watersiari
27 September 2022, 16:07