Sherehe ya Kung'ara Bwana Yesu Kristo: Muhtasari wa Mafumbo Makuu ya Imani ya Kanisa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Tarehe 6 Agosti 2022, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Kung’ara Bwana Yesu Kristo, yaani akiwa Mlimani Tabor aligeuka sura mbele ya Mitume wake Petro, Yakobo, na Yohane nduguye. Uso wake ukang’aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama nuru. Rej. Mt 17:2. Hili ni tukio ambalo Kristo Yesu alipenda kuwafunulia Mitume wake na kwa njia hii, watu wote utukufu wake. Akawaonesha kwamba, hatima ya maisha ya mwanadamu ni kuelekea mbinguni kwa Baba wa milele. Hii ni changamoto ya kuendelea kujizatiti kikamilifu katika kuuponya Ulimwengu kutokana na uharibifu na uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote na kuendelea kuujenga Ufalme wa Mungu. Huu ni ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Mama Kanisa anawakumbusha watoto wake kwamba, maisha ya kila kiumbe yanaelekea kwenye hatima yake, yaani ufunuo wa Kristo Yesu. Yeye ni Bwana wa historia na viumbe vyote na hatima ya yote haya ni ufalme wa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu Kristo Yesu ni Mwana Mpendwa wa Mungu, waamini wanaalikwa kumsikiliza kwa dhati kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ni kuanzia Mwezi Septemba 2022 hadi Machi 2023.
Kila mwamini ajitahidi kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa bila kuwekewa vizingiti, kukataliwa au kuhukumiwa. Ni wakati wa kusiliza Neno la Mungu na waamini kusikilizana wao kwa wao! Ni muda wa kumsikiliza Roho Mtakatifu ili aweze kuwafunulia njia na lugha mpya, ili kuzama katika ukweli wa mambo. Roho Mtakatifu anawataka waamini kusikiliza maswali ya watu waliokata tamaa, matumaini ya watu na Makanisa mahalia! Mkazo ni sanaa ya kusikiliza kwa kwa makini. Baba Mtakatifu Francisko anakazia kung’amua baada ya kukutana na kusikilizana kwa makini kitendo kinachofuatia ni mang’amuzi. Sherehe ya Kung’ara Bwana anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko, ni mwaliko wa kuendelea kumtafakari Kristo Yesu, aliyeng’ara Mlimani Tabor. Kristo Yesu ni mwanga unaoyaangazia matukio mbalimbali ya kila siku katika maisha ya mwanadamu. Sherehe ya Kung’ara Bwana ni mwendelezo wa Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, Ukuu wa Fumbo la Msalaba na Mwanga unaong’ara katika maisha na utume wa Kanisa. Huu ni mwanga utakaojionesha kwa namna ya pekee, Siku ile Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho! “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Msikieni yeye.” Mt 17: 5 Kusikiliza ni sanaa inayohitaji majiundo makini, endelevu na fungamani, mwaliko kwa waamini kumwomba Roho Mtakatifu, ili awasaidie kuwa wasikivu wema na wazuri, tayari kumwilisha kile wanachokisikia kutoka katika dhamiri zao nyofu!
Kristo Yesu kama ilivyokuwa kwa Mitume wake wa karibu aliowateuwa kuwa mashuhuda kwa matukio muhimu ya maisha yake yaani: Petro, Yakobo na Yohane, Wakristo pia wanahamasishwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu imefunuliwa kwa njia ya Maandiko Matakatifu katika Sheria na Unabii na kupata utimilifu wake katika Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipotwaa mwili kwa njia ya Roho Mtakatifu, na kuzaliwa kwake Bikira Maria katika mambo yote alikuwa sawa na binadamu, isipokuwa hakutenda dhambi! Wakristo wanaitwa na wanatumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko kwa kutambua kwamba, daima Mwenyezi Mungu anaandama nao katika hija ya maisha yao. Sherehe ya kung’ara kwa Bwana ni chachu ya mabadiliko katika maisha, kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata upendo na huruma ya Mungu katika maisha, mambo msingi yanayowaelekeza waamini katika ukamilifu na utakatifu wa maisha.
Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, akifanya tafakari kuhusu Sherehe hii anasema kwamba, ni muhtasari wa Mafumbo ya Imani ya Kanisa, yaani: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, ili aweze kuwaimarisha wafuasi wake katika hija ya mwanga wa imani. Ni kielelezo cha mshikamano wa dhati kati ya Kristo Yesu na kazi ya uumbaji ambayo ameikomboa kwa njia ya Fumbo la Msalaba. Mama Kanisa katika maadhimisho haya, anaungama kwa dhati kabisa kuhusu: Ubinadamu na Umungu wa Kristo; Kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu na Mkombozi wa dunia sanjari na kuzaliwa kwa Kanisa Sakramenti ya wokovu kwa binadamu! Sherehe hii inagusa kwa namna ya pekee, umuhimu wa Kanisa kusimama kidete kulinda na kutunza kazi ya uumbaji kama anavyokaza kusema Mtakatifu Damascene. Kristo Yesu anaufunua Umungu wake kwa njia ya mwili uliotukuka, ndiyo maana Kanisa linamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa, shukrani na utukufu kwani ukuu una Yeye milele hata na milele! Hii ni changamoto kwa kila mwamini kuhakikisha kwamba, anatoa nafasi kwa mwanga wa imani, ili uweze kumletea mabadiliko ya dhati katika maisha, kwa kuifia dhambi na nafasi zake, ili kutoa fursa ya kuishi katika utu mpya unaofikia hatima yake katika Fumbo la Msalaba wa Kristo.
Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto anakaza kusema, huu ni mchakato wa toba na wongofu wa ndani, unaopania kumsafisha na kumtakasa mwamini katika hija ya maisha yake ya kiroho, ili siku moja aweze kuufikia utukufu wa maisha na uzima wa milele. Ni ufunuo wa mwanga utakaozima giza la Kashfa ya Fumbo la Msalaba, tayari kutoa nafasi kwa binadamu kumwabudu, kumsifu, kumtukuza na kumwomba Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kabisa, kuisikiliza sauti ya Mungu na kutekeleza mapenzi yake katika uhalisia wa maisha yao, kwani Neno la Mungu ni dira na mwongozo wa maisha. Neno la Mungu ni Ufunuo wa utambulisho wa Mwana wa Mungu kama siku ile ya Ijumaa kuu atakavyosema yule Akida kwamba, “kwa hakika huyu alikuwa ni Mwana wa Mungu”. Katika maadhimisho ya Sherehe ya Kung’ara Bwana, Kanisa kwa mwaka huu, 2022, linafanya kumbukizi ya miaka 44 tangu Mtakatifu Paulo VI alipofariki dunia, “dies natalis” akiwa kwenye Ikulu ndogo ya Castel Gandolf, nje kidogo ya mji wa Roma na kuzikwa tarehe 12 Agosti 1978 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.
Mtakatifu Paulo VI anasema, Sherehe ya Kung’ara kwa Kristo Yesu inaangaza nuru ya ajabu katika maisha ya kila siku ili kufukuzia mbali giza la kifo linalosumbua akili ya mwanadamu. Mlimani Tabor, Yesu anaufunua utukufu na Umungu wake, mbele ya mashuhuda aliowateuwa mwenyewe ili kudhihirisha kwamba, kweli alikuwa ni Mwana mpendwa wa Mungu, Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya Nafsi yake. Tukio hili linautukuza ubinadamu unaofumbatwa katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu! Rej. Mk 8:31-34. Hapa Yesu anadhihirisha utukufu wa Fumbo la Pasaka, kielelezo makini cha sadaka na majitoleo yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, ili hatimaye, aweze kustahilishwa kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru. Mwili uliotukuka mbele ya Mitume wa Kristo Yesu ni mwili wa Kristo na kwamba, hata mwili wa binadamu utapata urithi wa mwanga wa uzima wa milele, kwa kushiriki katika utukufu na kwa njia hii wapate kushiriki tabia ya Uungu kwa kuokolewa na uharibifu ulioko duniani kwa sababu ya tamaa. Hii ni sehemu ya tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana, iliyokuwa imeandaliwa na Mtakatifu Paulo VI kwa ajili ya Sherehe ya Kung’ara kwa Yesu, tarehe 6 Agosti 1978, lakini kutokana na homa kali iliyomshika siku hiyo, hakuweza kutokeza mbele ya waamini na matokeo yake, jioni akafariki dunia katika amani.
Mtakatifu Paulo VI anakaza kusema, waamini wanasubiri kushirikishwa utukufu wa Mungu ambao walianza kuutafuta kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Mtakatifu Paulo VI katika tafakari yake, aliwakumbuka hata wale ambao kutokana na sababu mbalimbali walikuwa wanateseka, ili nao, hata katika hali na mazingira kama haya, waweze kupata walau mwanya wa mapumziko. Hawa ndio wale watu wasiokuwa na fursa za ajira, kiasi hata cha kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu katika familia na jamii katika ujumla wake. Ni watu wanaoteseka kutokana na baa la njaa sehemu mbalimbali za dunia pamoja na wale wote walioathirika kutokana na sera na mikakati tenge ya uchumi na maendeleo jamii. Kutokana na mahitaji msingi ya umati wote huu, Kanisa linapenda kumtolea Bikira Maria sala na maombi yake, ili aweze kusaidia kuombea umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu.