Tafuta

Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa ni kielelezo na ishara ya ukaribu na uwepo wa Mungu kwa waja wake, mwaliko kwa waamini kujifunza uwepo wa Mungu kupitia kwa macho ya Bikira Maria. Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa ni kielelezo na ishara ya ukaribu na uwepo wa Mungu kwa waja wake, mwaliko kwa waamini kujifunza uwepo wa Mungu kupitia kwa macho ya Bikira Maria. 

Sherehe Kufunga Jubilei ya Miaka 100 ya Bikira Maria wa Altagracian

Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho ni kielelezo cha utimilifu wa Kanisa, tumaini hakika na faraja kwa watu wanaosafiri huku bondeni kwenye machozi. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Askofu mkuu Edgar Peña Parra, anasema, watu wa Mungu wanasali na kujisadaka, ili kujipatanisha na Mungu na kukoleza moto wa upendo kati yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria wa Altagracian, alipotangazwa rasmi kuwa ni Mama mlinzi na Mwombezi wa Jamhuri ya Wadominican, tarehe 15 Agosti 1922, Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua umuhimu wa maadhimisho ya Jubilei hii, ameamua kumteua Askofu mkuu Edgar Peña Parra, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican kuwa mwakilishi wake maalum katika sherehe za kufunga mwaka wa Jubilei. Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho ni kielelezo cha utimilifu wa Kanisa, tumaini hakika na faraja kwa watu wanaosafiri huku bondeni kwenye machozi. Baba Mtakatifu katika ujumbe aliomwandikia Askofu mkuu Edgar Peña Parra, anasema, watu wa Mungu wanasali na kujisadaka, ili kujipatanisha na Mungu na kukoleza moto wa upendo kati yao. Baba Mtakatifu anamtakia furaha, amani na utulivu wakati wa kilele cha Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria wa Altagracian, alipotangazwa rasmi kuwa ni Mama mlinzi na Mwombezi wa Jamhuri ya Wadominican. Bikira Maria anayo nafasi ya pekee sana kwa watu wa Mungu huko kwenye Jamhuri ya Wadominican. Kwa maombezi na tunza yake ya Kimama, watu wa Mungu wawake moto wa upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, tayari kuendelea kulitumikia Fumbo la Wokovu.

Baba Mtakatifu anasema, Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa ni kielelezo na ishara ya ukaribu na uwepo wa Mungu kwa waja wake, mwaliko kwa waamini kujifunza uwepo wa Mungu kupitia kwa macho ya Bikira Maria, ili hatimaye, waweze kumwona Kristo Yesu kati pamoja na jirani zao, daima wakitambua kwamba, wao wote ni sehemu ya familia kubwa ya binadamu. Bikira Maria wa Altagracian, amekuwa ni chanzo cha mshikamano wa udugu wa kibinadamu, wakati wa shida na magumu; amekuwa ni dira na mwongozo katika mapito yao ya kila siku. Kwa ulinzi na tunza yake ya daima anaendelea kuwasha moto wa matumaini, ambayo ni urithi mkubwa kutoka kwa wazee wao waliotangulia mbele za haki wakiwa na tumaini la ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele. Ni mwaliko kwa watu wa Mungu Jamhuri ya Wadominican, kuhakikisha kwamba wanaendelea hata wao kurithisha imani hiyo kwa kizazi cha sasa na vile vijavyo. Wajitahidi kushikamana katika ujenzi wa umoja, udugu wa kibinadamu na kutembea kwa pamoja, huku wakijitahidi kutafuta na kuyafanya mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Mwenyezi Mungu amejifunua kuwa ni Baba wa huruma na anawakumbatia wote pasi na ubaguzi.

Bikira Maria ana nafasi ya pekee katika maisha na utume wa watu wa Dominican.
Bikira Maria ana nafasi ya pekee katika maisha na utume wa watu wa Dominican.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwatia shime ili wawe ni watu wa shukrani, kwa Bikira Maria, Mama na Mlinzi wao wa daima. Katika shida na mahangaiko yao mbalimbali, kamwe wasivunjike wala kupondeka moyo, bali wasimame imara na thabiti kutangaza na kushuhudia imani na upendo wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, chini ya maombezi ya Bikira Maria. Nuru yake takatifu na angavu ni chanzo cha toba na wongofu wa ndani, unaowaelekeza kukutana na Mwenyezi Mungu. Watambue na kuamini kwamba, nguvu ya Roho Mtakatifu inawasukuma kufanya kazi kwa upendo, wema na furaha kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kristo Yesu, apende kuwabariki na Bikira Maria wa Altagracian, awalinde na kuwasindikiza. Baraza la Maaskofu Katoliki la Dominican “Conferenza Episcopale Dominicana (CED), tarehe 15 Agosti 2022 linahitimisha kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria wa Altagracian, alipotangazwa rasmi kuwa ni Mama mlinzi na Mwombezi wa Jamhuri ya Wadominican, tarehe 15 Agosti 1922. Katika mwaka wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 ya Bikira Maria wa Altagracian, watu wa Mungu walitaka kujiweka tena chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili awasaidie kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa Kitaifa, huku wakijitahidi kuishi kwa amani na utulivu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote wa Mungu nchini humo. Hii ni hija ya kutembea pamoja kiimani na kiutu, ili kuweza kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa mbalimbali kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Mshikamano wa umoja na udugu wa kibinadamu ni muhimu sana.
Mshikamano wa umoja na udugu wa kibinadamu ni muhimu sana.

Baraza la Maaskofu Katoliki la Dominican linabainisha kwamba, waamini wanaoshiriki kikamilifu katika maadhimisho haya wanaweza pia kupata rehema kamili kwa kufuata masharti yaliyowekwa na Mama Kanisa kwa watoto wake. Mafundisho ya imani na ibada ya rehema katika Kanisa Katoliki yameunganika kabisa na matunda ya Sakramenti ya Upatanisho. Kanisa linafundisha kwamba, Rehema kamili ni msamaha mbele ya Mwenyezi Mungu wa adhabu za muda kwa ajili ya dhambi ambazo kosa lao limekwishafutwa, msamaha ambao Mkristo mwamini aliyejiweka vizuri huupata baada ya kutimiza mashari yaliyotolewa na Mama Kanisa, kwa tendo la Kanisa ambalo likiwa ni mgawaji wa ukombozi hutumia kwa mamlaka yake hazina ya malipizi ya Kristo Yesu na ya watakatifu wake. Rehema imegawanyika katika sehemu kuu mbili: Rehema Kamili au Rehema ya Muda kutokana kwamba inaondoa au sehemu au adhabu yote kabisa ya muda inayotakiwa kwa sababu ya dhambi. Kila mwamini anaweza kupata rehema kwa ajili yake mwenyewe au kwa ajili ya marehemu wake kama atatimiza yafuatayo: Mosi, awe na nia thabiti ya kupata rehema katika kipindi kilichopangwa. Pili, apokee Sakramenti ya Upatanisho. Tatu, apokee Ekaristi Takatifu siku hiyo ya kutolewa rehema kamili. Nne; asali kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu. Mwishoni atembelee Kanisa au Kituo maalumu kilichotengwa kwa ajili ya kupatiwa Rehema Kamili.

Jubilei B. Maria
13 August 2022, 15:35