Papa Francisko: Watu Wanapoteza Maisha Somalia Kwa Baa la Njaa!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni, Dominika tarehe 14 Agosti 2022 ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuonesha mshikamano wa kidugu na watu wa Mungu nchini Somalia wanaotishiwa kifo kutokana na ukame mkubwa ambao umeathiri Somalia na Nchi za Pembe ya Afrika. Hawa ni watu wanaokabiliana na majanga makubwa yanayoendelea kupekenyua utu, heshima na haki zao msingi. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itaonesha mshikamano wa udugu wa kibinadamu ili kutoa msaada unaohitajika kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu wa Ukanda wa Pembe ya Afrika. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, kiasi kikubwa cha rasilimali fedha ambazo zingeweza kutumika kwa ajili ya kuokoa maisha ya wananchi wa Somalia kutokana na baa la njaa, na kusaidia mchakato wa maboresho ya afya na elimu zinatumika kwa ajili ya vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Somalia.
Wakati huo huo, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, linaloundwa na Nchi 8 ambazo ni: Zambia, Malawi, Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan, Ethiopia na Eritrea, kuanzia tarehe 10-18 Julai 2022 liliadhimisha mkutano wake mkuu wa 20 Jijini Dar es Salaam na kunogeshwa na kauli mbiu: “Utunzaji wa Mazingira kwa Ajili ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu.” Hii ni kauli mbiu inayochota maudhui na utajiri wake kutoka katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” unatoa kipaumbele cha pekee katika ulinzi na utunzaji wa mazingira nyumba ya wote.
Ibada ya Misa Takatifu katika kufunga Mkutano Mkuu wa 20 wa AMECEA, Dominika tarehe 17 Agosti 2022 kwenye Viwanja vya Msimbazi Centre Jimbo kuu la Dar Es Salaam na kuongozwa na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam. AMECEA katika ujumbe wake kwa Watu wa Mungu inasema, “Sisi Maaskofu wa Kanisa Katoliki Ukanda wa Mashariki mwa Afrika tunajizatiti kuitika kilio kwa dunia na kilio cha maskini katika kutekeleza wajibu ule wa Mungu tuliokabidhiwa. Mungu alipenda mwanadamu ailime ardhi na kuitunza (Mw. 2:15) na kwa kutambua mwito huu mkuu ninawahimiza wahudumu wote wa uchungaji wa Kanisa Katoliki na watu wote wenye mapenzi mema kuwa walinzi wa mazingira na rasilimali asili siyo tu kwa kizazi hiki bali pia kwa kizazi kijacho ambacho kwa niaba yao tunawajibu wa kuyaendeleza mazingira.
MSHIKAMANO: Tunapenda kuwahakikishia ndugu zetu kaka na dada katika ukanda wetu na kwingineko waliokubwa na athari baya za mabadiliko ya tabia ya nchi kama vile mafuriko kwamba hawapo peke yao. Katika moyo wa sala na kujali tunasimama nao kwatika mahangaiko yao. Sala zetu za amani tunazielekeza kwa Mabaraza wanachama walio katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na mafarakano ikiwemo Ethiopia, Sudan, Sudan ya Kusini na jamii zote zilizo katika mafarakano katika Bara la Afrika na kokote duniani.”