Tafuta

Papa Francisko: Mazungumzo katika ukweli na uwazi, yanaweza kufanyika na kuleta matokeo chanya na madhubuti, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Papa Francisko: Mazungumzo katika ukweli na uwazi, yanaweza kufanyika na kuleta matokeo chanya na madhubuti, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.  

Papa Francisko Mazungumzo katika Ukweli na Uwazi Chanzo cha Amani ya Kudumu Duniani

Makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya Urussi na Ukraine kwa kuratibiwa na Umoja wa Mataifa ili kuiwezesha Ukraine kuanza kusafirisha mazao ya nafaka ni hatua muhimu sana katika mchakato wa kukabiliana na baa la njaa duniani. Meli za Riva Wind, Mustafa Necati, Star Helena na Glory zikiwa zimebeba takribani tani 170, 000 za mazao ya nafaka zimeondoka nchini Ukraine.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mamilioni ya watu wanakabiliwa na hatari ya kukumbwa na baa la njaa duniani kutokana na vita inayoendelea kati ya Urussi na Ukraine, athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, ambao umepelekea madhara makubwa katika masuala ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kitamaduni. Itakumbukwa kwamba, Ukraine ni kati ya wazalishaji wakuu wa nafaka duniani, lakini kutokana na vita kati yake na Urussi, gharama ya kuagizia mazao ya nafaka kutoka Ukraine imepanda maradufu na hivyo kuendelea kuwatumbukiza watu wengi katika dimbwi la umaskini na baa la njaa. Makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya Urussi na Ukraine kwa kuratibiwa na Umoja wa Mataifa ili kuiwezesha Ukraine kuanza kusafirisha mazao ya nafaka sehemu mbalimbali za dunia ni hatua muhimu sana katika mchakato wa kukabiliana na baa la njaa duniani. Meli za Riva Wind, Mustafa Necati, Star Helena na Glory zikiwa zimebeba takribani tani 170, 000 za mazao ya nafaka zimeondoka nchini Ukraine.

Majadiliano katika ukweli na uwazi ni chanzo cha amani ya kudumu.
Majadiliano katika ukweli na uwazi ni chanzo cha amani ya kudumu.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 7 Agosti 2022 amepongeza hatua hii iliyochukuliwa na Jumuiya ya Kimataifa na kwamba, mazungumzo katika ukweli na uwazi, yanaweza kufanyika na kuleta matokeo chanya na madhubuti, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anakaza kusema, tukio hili ni ishara ya matumaini na kwa njia ya majadiliano, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kusitisha vita, kinzani na mipasuko ya kijamii na htimaye Jumuiya ya Kimataifa kuweza kufikia haki na amani ya kudumu. Baba Mtakatifu amesikitishwa pia na ajali iliyotokea Jumamosi tarehe 6 Agosti 2022 huko Poland ambako watu 12 walipoteza maisha katika ajali hiyo na wengine 32 kujeruhiwa ambapo taarifa zinaonesha kwamba kati yao majeruhi 19 bado wana hali mbaya. Hawa ni mahujaji kutoka Poland waliokuwa wanakwenda kuhiji huko Medjugorje. Wote hawa, Baba Mtakatifu amewaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria.

Nafaka Ukraine

 

08 August 2022, 15:05