Tafuta

Madhabahu ni kitovu cha uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Madhabahu ni kitovu cha uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. 

Papa Francisko: Madhabahu Ni Kitovu cha Uinjilishaji wa Kina

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Madhabahu ni mlango wazi wa uinjilishaji mpya unaokita mizizi yake katika moyo wa: Ukarimu kwa mahujaji; maisha ya sala, lakini zaidi kwa kuwasaidia waamini kujifunza kusali Sala ya Kanisa sanjari na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, hususan Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho, Mahakama ya huruma na upendo wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi Kuhusu Maana na Thamani ya Uzee, Jumatano tarehe 17 Agosti 2022, amewakumbuka mahujaji wanaoendelea kumiminika kwenye Madhabahu ya Jasna Góra huko Częstochowa, nchini Poland kwa ajili ya kuombea amani na upatanisho sehemu mbalimbali za dunia. Kati yao, wamo pia mahujaji kutoka nchini Ukraine. Baba Mtakatifu anawataka mahujaji kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea hatima ya Ulaya na Ulimwengu katika ujumla wake. Ikumbukwe kwamba, Madhabahu ni mlango wazi wa uinjilishaji mpya unaokita mizizi yake katika moyo wa: Ukarimu kwa mahujaji; maisha ya sala, lakini zaidi kwa kuwasaidia waamini kujifunza kusali Sala ya Kanisa sanjari na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, hususan Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu! Baba Mtakatifu anasema, Madhabahu yawe ni mahali pa sala na ukimya, ili kutoa nafasi kwa mahujaji kuzungumza na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yao! Madhabahu ni mahali pa kuonjeshana upendo na ukarimu, ili kila hujaji anapofika mahali hapa aweze kujisikia kuwa yuko nyumbani anakaribishwa, kuthaminiwa na kupendwa. Mara nyingi watu wanafanya hija kutokana na kuvutwa na Mapokeo, utajiri wa sanaa, uzuri wa mazingira pamoja na kufuata ushauri kutoka kwa jirani zao! Mahujaji kama hawa wanapoonja ukarimu, mioyo yao inafunguka na hivyo kuanza kujenga urafiki na hatimaye, kujiaminisha kwa Kristo na Kanisa lake! Watu wanaweza kukata tamaa, ikiwa kama hawataonja ukarimu kutoka kwa wenyeji wao!

Madhabahu ni kitovu cha uinjilishaji wa kina: kiroho na kimwili
Madhabahu ni kitovu cha uinjilishaji wa kina: kiroho na kimwili

Madhabahu kimsingi ni mahali pa: Sala na Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, anayetoa machozi ya faraja kwa wale wanaoteseka; ni mwombezi wa watu waliovunjika na kupondeka moyo; watu waliokata tamaa na kwamba, Bikira Maria anajaribu kujibu sala ya kila mwamini anayekimbilia ulinzi na tunza yake ya daima. Madhabahu ni mahali ambapo panapaswa kukuza na kudumisha ari na moyo wa Sala ya Kanisa, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa kama sehemu ya kazi ya ukombozi. Ni mahali pa shuhuda za imani, matumaini na mapendo, kielelezo cha Kanisa linalokesha na kusali daima! Madhabahu ni mahali pa ukimya unaopaswa kububujika kutoka katika undani wa mahujaji, tayari kuomba: baraka, neema na rehema pamoja na kuzidimisha upendo kwa Mungu na jirani! Madhabahu ni mahali pa kuonja huruma na upendo wa Mungu unaofumbatwa katika Sakramenti ya Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu. Maeneo kama haya yanahitaji wakleri waliofundwa barabara, watakatifu, vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, katika madhabahu, kamwe hawatakosekana Wamisionari wa huruma, mashuhuda wa upendo wa Mungu unaokoa na kuponya! Madhabahu yawe ni mahali pa kumwilisha upendo, kielelezo cha utekelezaji wa Amri ya Upendo kwa Mungu na jirani!

Madhabahu ni pa kumwilisha upendo na mshikamano wa kidugu
Madhabahu ni pa kumwilisha upendo na mshikamano wa kidugu

Baba Mtakatifu Francisko anasema, likizo ni muda muafaka wa kujipatia nafasi ya kupumzika: kimwili na kisaikolojia, ili kupyaisha tena nguvu za kuweza kusonga mbele katika mapambano ya maisha ya kila siku, ili hatimaye, kukutana na Kristo Yesu kwa karibu zaidi. Ni mwaliko wa kumatafuta na kumhudumia miongoni mwa wazee, maskini na wahitaji zaidi. Ni fursa makini ya kutenga muda kwa ajili ya sala na kujitahidi kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ni wakati pia wa kujenga, kudumisha na kuimarisha mahusiano na ujirani wema, kwa kuwashirikisha wengine muda, karama na mapaji ambayo Mwenyezi Mungu amewakirimia waja wake. Ni muda wa kutafakari kazi ya uumbaji inayoshuhudia na kutangaza upendo wa Mungu kwa waja wake. Likizo ni wakati muafaka wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa, shukrani, ukuu na uweza kutokana na kazi kubwa ya uumbaji. Mwanadamu katika ulimwengu mamboleo anayo kila sababu ya kulinda, kutunza na kuendeleza utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kwani mazingira bora na safi ni ufunuo wa: nguvu, wema, ukuu na utakatifu wa Mungu.

Papa Madhabahu
17 August 2022, 16:52