Tafuta

Papa Francisko: anawataka waamini kuiga mfano wa maisha na sadaka kutoka kwa Mtakatifu Laurenti Shemasi mkuu na Shahidi wa Kanisa la Roma. Ushuhuda wa huduma kwa maskini. Papa Francisko: anawataka waamini kuiga mfano wa maisha na sadaka kutoka kwa Mtakatifu Laurenti Shemasi mkuu na Shahidi wa Kanisa la Roma. Ushuhuda wa huduma kwa maskini. 

Mtakatifu Laurenti Shemasi Mkuu na Shahidi wa Kanisa la Roma

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuiga mfano wa maisha na sadaka kutoka kwa Mtakatifu Laurenti Shemasi mkuu na Shahidi wa Kanisa la Roma, wa kutaka kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu inayomwilishwa katika huduma ya upendo hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, bila kuwasahau wenye kuhitaji msaada zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 10 Agosti anaadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Laurenti Shemasi mkuu na Shahidi wa Kanisa la Roma. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake kuhusu Maana na Thamani ya Uzee, Jumatano tarehe, 10 Agosti 2022, amewaalika waamini kuiga mfano wa maisha na sadaka kutoka kwa Mtakatifu Laurenti Shemasi mkuu na Shahidi wa Kanisa la Roma, wa kutaka kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu inayomwilishwa katika huduma ya upendo hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, bila kuwasahau wenye kuhitaji msaada zaidi. Ikumbukwe kwamba, Kanisa linawategemea sana maskini katika maisha na utume wake, kwani maskini ni amana na utajiri wa Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kimsingi, maskini ndio walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu. Mapato na faida inayopatikana kutokana na sanaa na vivutio vya kitamaduni vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa yanapaswa kutumika kugharimia shughuli na huduma ya upendo inayotolewa na Mama Kanisa. Ikumbukwe kwamba, maskini ni amana na utajiri wa Kanisa; wao ndio walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu.

Maskini ni amana na utajiri wa Kanisa, walengwa wa uinjilishaji mpya.
Maskini ni amana na utajiri wa Kanisa, walengwa wa uinjilishaji mpya.

Mtakatifu Laurenti, Shemasi anakumbukwa sana kutokana na ujasiri wake, kwa kuuza baadhi ya sanaa na malikale ya Kanisa ili kuwahudumia maskini! Kumbe, utunzaji wa sanaa na vivutio vya kitamaduni ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu, lakini zaidi maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Dhana ya umaskini inajikita katika umaskini wa hali na mali; maadili na utu wema; kwani wote hawa, Kristo Yesu amejisadaka kwa ajili ya kuwatangazia Habari Njema ya Wokovu. Wakristo wanapaswa kuwajali, kuwathamini na kuwapenda maskini na watu wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama afanyavyo mama mzazi kwa watoto wake. Kanisa linatoa huduma ya upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa maskini, kwa kujali na kuthamini utu, heshima na haki zao msingi, kwani hata wao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee, anawaalika Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujifunza kutoka kwenye shule ya maskini kwani kati ya maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum, humu humu kuna watakatifu na watu ambao wanaweza kuwafundisha wengine tunu msingi za maisha ya kijamii, kiutu na kiroho. Maskini si mzigo bali ni shule makini kwa watu wa Mungu.

Mtakatifu Laurenti Shemasi na Shuhuda wa Kanisa la Roma: Ushuhuda.
Mtakatifu Laurenti Shemasi na Shuhuda wa Kanisa la Roma: Ushuhuda.

Kumbe, kuna umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutetea ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Maskini ni kielelezo cha Kristo Yesu kati pamoja na watu wake. Katika shule ya upendo, watu wanatafuta faraja, mahusiano na mafungamano; utu na heshima ya binadamu na kwa njia hii, waamini wanaweza kujifunza kutoka kwa maskini kwa kuwakaribisha, kuwasikiliza, kuwakirimia na kuwahudumia kwa upendo na nidhamu ya hali ya juu. Kuna mambo makuu mawili yanayotishia amani, usalama na mafungamano ya kijamii: kwanza kabisa ni ukosefu wa fursa za ajira unaowakumba wafanyakazi na familia zao pili ni hali mbaya ya maisha ya wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi, lakini wanakumbana na kuta za uchoyo na ubinafsi! Kuna uhusiano wa karibu sana kati ya fursa za ajira na familia, kwani kazi ni sehemu ya utimilifu wa maisha na utu wa binadamu. Kazi inawawezesha wafanyakazi kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao, kwa kuhakikisha kwamba, familia zinapata mahitaji msingi. Pale mfanyakazi anapokosa fursa za kazi kutokana na sababu mbali mbali, utu, heshima, wajibu na dhamana yake kwenye familia na jamii iko mashakani na pole pole, familia inaanza kupoteza matumaini ya maisha! Huo unakuwa ni mwanzo wa magonjwa ya sonona!

Shemasi Laurenti ni mfano bora wa huduma kwa maskini.
Shemasi Laurenti ni mfano bora wa huduma kwa maskini.

Hii nii changamoto inayohitaji uwajibikaji unaomwilishwa katika Injili ya upendo kwa watu wanaohitaji: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete dhidi ya biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo kwa kujikita katika: kanuni maadili na utu wema; uwajibikaji, sheria na taratibu za nchi husika. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu bila kujitumbukiza katika ushirikiano na wafanyabiashara ya binadamu na utumwa mamboleo. Hapa kuna haja ya kukuza utamaduni na kujenga madaraja ya kukutana na watu, ili kuheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana kama binadamu. Jumuiya ya Kimataifa ina wajibu na dhamana ya kujenga utandawazi wa mshikamano na upendo, dhidi ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine; utandawazi unaojikita katika ubinafsi, uchoyo na mkono wa “birika.”

Mtakatifu Laurenti

 

10 August 2022, 15:37