Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu tarehe 29 na Jumanne tarehe 30 Agosti 2022 ameongoza mkutano wa Baraza la Makardinali, kwa faragha Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu tarehe 29 na Jumanne tarehe 30 Agosti 2022 ameongoza mkutano wa Baraza la Makardinali, kwa faragha  

Mkutano wa Baraza la Makardinali: Ushuhuda wa Injili Ya Upendo

Makardinali wameridhika na jinsi ambazo mkutano huu umeendeshwa, kwa sehemu kubwa ya Makardinali kushirikisha mawazo yao, baada ya Baba Mtakatifu Francisko kutoa mwaliko. Tema kuu ni: ushirika kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ushuhuda wa Uinjilishaji unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Pili ni kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa watu wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu tarehe 29 na Jumanne tarehe 30 Agosti 2022 ameongoza mkutano wa Baraza la Makardinali, kwa faragha ili kufanya tafakari ya kina kuhusu Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.” Mkutano huu ni sehemu ya utekelezaji wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuanza kujifunza utamaduni wa kusikilizana katika ukweli na uwazi; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo. Baraza hili limekuwa na ushiriki mkubwa wa Makardinali, kati ya Makardinali 226, wanaohudhuria ni zaidi ya 200. Makardinali wameridhika na jinsi ambazo mkutano huu umeendeshwa, kwa sehemu kubwa ya Makardinali kushirikisha mawazo yao, baada ya Baba Mtakatifu Francisko kutoa mwaliko. Tema kuu ni: ushirika kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ushuhuda wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Pili ni mwaliko wa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili zinazofumbatwa katika Amri kuu ya upendo kwa Mungu na jirani. Katiba mpya ya Kitume ya “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu”  imeanza kutumika rasmi tarehe 5 Juni 2022, Sherehe ya Pentekoste na hivyo kuchukua nafasi ya Katiba ya Kitume “Pastor bonus” ya tarehe 28 Juni 1988 iliyoanza kutumika rasmi 1 Machi 1989. Sekretatieti kuu ya Vatican ni daraja kati ya Kanisa la Kiulimwengu na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki.

Makardinali wapya wamesimikwa tayari kutangaza na kushuhudia Injili
Makardinali wapya wamesimikwa tayari kutangaza na kushuhudia Injili

Kutangaza na kushuhudia Injili ni dhamana na utume ambao Kristo Yesu amewakabidhi Mitume wake. Huu ni utume wa kwanza unaopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa kila mtu na kwa ulimwengu mzima. Utume huu unatekelezwa kikamilifu na Mama Kanisa anapotangaza na kushuhudia Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma makini kwa binadamu wote: kiroho na kimwili. Upendeleo wa pekee ni kwa maskini, wagonjwa na wadhaifu ndani ya jamii. Katika muktadha huu, Kanisa linapaswa kujikita katika wongofu wa kimisionari, kwa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu. Kanisa lijitambulishe na kueleweka kuwa ni Fumbo la Ushirika unaomwilishwa katika dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Katiba hii mpya ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Baraza la Makardinali katika mikutano yake elekezi kabla ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro uliofanyika mwaka 2013. Haya ni matunda ya kazi kubwa iliyotekelezwa na Baraza la Makardinali Washauri kuanzia mwezi Oktoba 2013 hadi Februari 2022 na hatimaye, kuchapishwa tarehe 19 Machi 2022 chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko bila kusahau mchango uliotolewa na Makanisa mahalia kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Katiba hii kwa sasa inatekeleza mabadiliko makubwa yanayofanyiwa na Baba Mtakatifu tangu alipoteuliwa kuliongoza Kanisa Katoliki mwaka 2013. Kuna baadhi ya Mabaraza ya Kipapa yameunganishwa ili kuongeza tija, ubora na ufanisi katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu, sanjari na kuunda Mabaraza mapya ya Kipapa. Sekretarieti kuu ya Vatican inayojulikana kama “Curia Romana” inaundwa na Sekretarieti ya mji wa Vatican, Mabaraza ya Kipapa na Ofisi mbalimbali zenye haki sawa katika utendaji wake. Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo, lililokuwa linajulikana kama “Apostolic Elemosineria” yaani “Idara ya Sadaka ya Kitume” limeanzishwa ili kutoa kipaumbele cha kwanza kwa matendo ya huruma: kiroho na kimwili, yanayotekelezwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro sehemu mbalimbali za dunia. Katiba ya Kitume “Hubirini Injili” inayagawanya Mabaraza ya Kipapa katika makundi makuu matatu: Baraza la Kipapa Kwa Ajili ya Uinjilishaji.

Mkutano wa Baraza la Makardinali: ujenzi wa utamaduni wa kusikilizana
Mkutano wa Baraza la Makardinali: ujenzi wa utamaduni wa kusikilizana

Pili, Baraza la Kipapa kwa Ajili ya Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Tatu ni Baraza ya Kipapa kwa Ajili ya Huduma ya Upendo. Mabadiliko mengine makubwa ni kuhusu Tume ya Kipapa kwa ajili ya ulinzi kwa watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia ambayo kwa sasa itakuwa chini ya Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na itaendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zake pamoja na kuwa na Rais na Katibu wake. Sehemu kubwa ya Katiba ya Kitume ya “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu” inajikita katika sheria, kanuni na taratibu na kwamba, kila Mkristo kwa Ubatizo wake ni Mtume mmisionari anaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema. Ni katika hali na mazingira kama haya hata waamini walei wenye sifa zinazohitajika wanaweza kuteuliwa kuchukua nafasi za uongozi kwenye Sekretarieti kuu kadiri ya Mamlaka aliyokabidhiwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Katiba ya Kitume inabainisha vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa ili Mkristo aweze kuteuliwa kutoa huduma katika “Curia Romana.” Hii ni huduma kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro inayomwajibisha mwamini kujenga na kudumisha ushirika sanjari na kutoa huduma kwa utume wa Maaskofu, Makanisa Mahalia, Mabaraza ya Maaskofu na Miundombinu ya Makanisa ya Mashariki.

Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa.
Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa.

Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inapewa kipaumbele cha pekee. Sekretarieti kuu ya Vatican sanjari na dhana ya Mtume mmisionari ni hata kwa wale ambao wameteuliwa kufanya kazi kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Haya ni mambo makuu mawili yanayopaswa kuendelea kumwilishwa mintarafu Katiba ya Kitume ya “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili.” Hawa ni waamini wanaopaswa kuwa na tasaufi imara, maadili, ujuzi na weledi; mwenye uwezo wa kushirikiana na kwamba, uteuzi wa wafanyakazi wa Sekretarieti kuu, ni utambulisho wa Ukatoliki wa Kanisa na kwamba hauna budi kujidhihirisha bila shaka. Wakleri na watawa wataweza kutoa huduma yao kwa muda wa miaka mitano na mkataba huu, unaweza kurudiwa tena katika kipindi cha miaka mitano, baada ya hapo, mhusika atapaswa kurejea Jimboni au Shirikani mwake. Katiba hii mpya inaweka mkazo kwamba, hii ni “Sekretarieti ya Kipapa.” Kumbe, kuna uwezekano mkubwa kwa wafanyakazi wa Sekretarieri kuu ya Vatican kuhamishiwa kutoka Idara moja kwenda Idara nyingine, kadiri ya mahitaji na ufafanuzi kutoka kwenye Sekretarieti ya Uchumi, SPE au maelekezo yatakayotolewa na Msimamizi wa Urithi na Mali ya Kitume, APSA.

Katiba ya Kitume
30 August 2022, 15:15